Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema haifurahishwi na kitendo cha Jamhuri kushindwa kutekeleza amri zake zaidi ya mbili za kutaka kigogo wa IPTL, Harbinder Sethi akatibiwe Hospitali ya Muhimbili kutokana na tatizo lake la puto tumboni.
Jamhuri imeshindwa kutekeleza amri hiyo ya Mahakama licha ya kufahamishwa hatari inayoweza kutokea endapo kigogo huyo hatatibiwa haraka.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema mahakama haifurahishwi na hatua hiyo ambayo Jamhuri inadai mshtakiwa huyo kuendelea kutibiwa gerezani badala ya Muhimbili kama ambavyo mahakama hiyo iliamuru.
Wakili wa mshtakiwa huyo, Joseph Makandege awali alidai mteja wake asipopatiwa matibabu puto lililowekwa tumboni linaweza kupasuka na kupoteza uhai wake.
Mbali na Sethi, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni James Rugemarila ambaye ni Mkurugenzi wa VIP Engineering na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni IPTL, ambao wanakabiliwa na mashitaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani milioni 22. 1 sawa na Sh. bilioni 309 na utakatishaji fedha.