27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA: AMRI ZA KULIFUNGIA GAZETI LA MWANAHALISI NI BATILI

NORA DAMIAN Na MEZA FRIDE (SJMC), DAR ES SALAAM


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamuru gazeti la Mwanahalisi liendelee kuchapishwa kwani amri zilizotolewa wakati wa kulifungia ni batili.

Septemba 19 mwaka jana, Serikali ililifungia gazeti hilo kwa miaka miwili kwa madai kuwa limekuwa likikiuka misingi na sheria za taaluma ya uandishi wa habari.

Baada ya kufungiwa, Kampuni ya Uchapishaji ya Hali Halisi, ilifungua kesi katika mahakama hiyo ambayo wiki iliyopita ilitoa uamuzi kwa kuamuru gazeti hilo liendelee kuchapishwa.

Wakili wa Kampuni hiyo, Nashoni Nkungu, alisema uamuzi huo ulitolewa Julai 24, mwaka huu na Jaji Beatrice Mutungi.

“Mahakama katika uamuzi wake ilisema amri zilizotolewa wakati wa kulifungia gazeti ni batili, hazikufuata misingi ya kisheria na hakukuwa na haki ya usikilizwaji kwa upande wa mlalamikaji.

“Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo hana mamlaka yoyote, si tu ya kuwaomba watoe maelezo juu ya habari husika, hata ya kuwaomba walete utetezi wao.

“Na mahakama ilisema hilo si jukumu mojawapo katika yale majukumu ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Huduma za Habari,” alisema Nkungu.

Alisema hata waziri hana mamlaka ya kulifungia gazeti kama alivyofanya kwa kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.

“Mamlaka pekee ambayo anayo ni kuondoa ‘content’ ya habari ambayo inaonekana inahatarisha usalama wa taifa, kimsingi hata waziri hana mamlaka ya kufungia gazeti.

“Mahakama ilisikitishwa na kutotiliwa mkazo kwa amri ambazo zilitolewa mahakamani, kwani kulikuwa na amri zingine zilizotolewa, lakini mkurugenzi aliendelea kufanya kinyume, amekanywa kutoendelea kwenda kinyume na amri ambazo mahakama imekwishazitoa.

“Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo hana mamlaka yoyote si tu ya kuwaomba kama alivyofanya katika kesi hii, hana mamlaka yoyote ya kuandika barua kwa chombo cha habari na kukiambia kijieleze,” alisema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Uchapishaji ya Hali Halisi, Saed Kubenea, alisema wanakusudia kuwashtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura, kwa madai kuwa wameisababishia hasara kampuni hiyo ya Sh bilioni 2.2.

Alisema uamuzi huo wa mahakama umewasaidia kuonekana mbele ya jamii kwamba hawakuwa na makosa na kudai kuna watu wana hila na gazeti lao lisionekane mtaani.

“Mahakama imethibitisha hatukuwa na hatia, hivyo tunapanga kudai fidia kwa sababu tumepata hasara zaidi ya Sh bilioni 2, tumepoteza wafanyakazi, matangazo na wadau mbalimbali tuliokuwa tukishirikiana nao.

“Tutamshtaki AG na aliyekuwa Naibu Waziri (Wambura) tutamshtaki binafsi ili iwe onyo kwa viongozi wengine wanaotumia madaraka yao vibaya,” alisema Kubenea.

Mkurugenzi huyo alisema wanatarajia gazeti hilo litaanza kuchapishwa wiki ijayo na kuwataka waandishi wa habari na vyombo vya habari wasiogope kudai haki kwani mahakama bado ziko huru na zinatenda haki.

“Mwaka 2012 tulifungiwa kwa muda usiojulikana tukaenda mahakamani gazeti likarejeshwa Septemba 2015, twendeni mahakamani tukajenge hoja.

“Tunaamini mahakama zetu bado ziko huru na zinaweza zikatenda haki, isipokuwa kuna baadhi ya watu ndani ya Serikali wana kiburi cha kutotii maamuzi ya mahakama, pengine kwa masilahi yao binafsi ama kwa kutumwa,” alisema Kubenea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles