25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Watanzania wamekata tamaa

magufuli*Asema haiwezekani wachache wale kuku kwa mrija

 

Na Bakari Kimwanga, Iringa

 

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema amejipanga kulipa deni kwa Watanzania kwa kuleta mabadiliko ya kweli.

Amesema pamoja na hali hiyo, anatambua namna wananchi walivyokata tamaa ikiwamo kushindwa kubadili maisha yao, kutokana na ubinafsi wa watu wachache ambao wameamua kujimilikisha rasilimali za nchi.

Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, alipohutubia mikutano ya hadhara katika majimbo ya Kalenga, Kilolo na Iringa Mjini.

Alisema nchi haiwezi kuendelea kwa mfumo wa baadhi ya watu kujiona wao wapo daraja la kwanza, huku wananchi wa kawaida wakiendelea kuishi maisha ya kawaida.

Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali yake ya awamu ya tano itahakikisha inatoa fursa kwa Watanzania wote kunufaika na rasilimali za taifa.

Alisema Serikali yake, itakuwa ya watu waadilifu ambao watakuwa tayari kufanya kazi kwa masilahi ya watu.

“Ndugu zangu, mambo ni mengi ambayo nataka kuyafanya.. nataka kuleta maendeleo ya kweli na Tanzania mpya ambayo itawafanya wananchi wote wafurahie Serikali yao kuliko sasa.

“Ninajua kila zama na kitabu chake, Serikali ya Magufuli  inakuja kufanyakazi, ikiwamo ya kuwafunga mafisadi…kwa hili simung’unyi maneno Watanzania nitalitekeleza kwa vitendo kikubwa ninawaomba mniamini kwa kunichagua.

“Ninajua Watanzania wanataka mabadiliko ambayo ni M4C yaani ‘Magufuli for Change’ na kwa lugha ya kawaida ni Magufuli kwa mabadiliko tena ya kweli,” alisema Dk. Magufuli.

Akizungumza namna atakavyoubadili mji wa Iringa, alisema anajua changamoto zilizopo  katika mkoa huo, ikiwamo kero ya barabara hasa za ndani.

“Ninawashangaa watu wanasema eti CCM haijafanya kitu na wengine ni hapa hapa Iringa mjini tena mchungaji wa kondoo wa Mungu ambaye anazijua amri kumi za Mungu ikiwemo ya kutosema uongo.

“Tena amekuwa akitukana ovyo ndani na nje ya Bunge nataka kuwaambia mawaziri nao ni binadamu wana nyongo…nataka kuwauliza ikiwa kila siku unamtukana waziri hivi kweli anaweza kukupa fedha za maendeleo, nichagueni mimi na wabunge wa CCM,” alisema.

Alisema anahitaji ushindi wa asilimia 99 ili wapinzani waisome namba kupitia masanduku ya kura.

Dk. Magufuli ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Tingatinga’ alisema anajua kazi kubwa anatakayokuwa nayo ikiwemo kulinda amani na umoja wa Watanzania.

“Ninataka kuwaambia mimi, nimekuwa waziri  kwa miaka 20 sijawahi kukemewa wala kufukuzwa nawahakikishia Watanzania nitafanyakazi usiku na mchana kulinda amani ya nchi yetu,” alisema.

Alisema pamoja na yaliyotokea ya baadhi ya wana CCM kuhama, yeye yupo imara na huenda watu hao kuondoka kwao itakuwa salama kwa chama hicho ambacho tayari kilianza kuonekana hakifai mbele ya Watanzania.

Alisema Serikali yake itakuwa rafiki wa wafanyabishara na anaunga mkono kazi kubwa ya kukuza ajira inayofanywa na kada wa chama hicho Mkoa wa Iringa, Said Asas ambaye ameweza kuajiri vijana wa mkoa huo zaidi ya 400.

 

Abadili staili jukwaani

 

Katika kile kinachoonekana kubadili aina ya kuomba kura jukwaani, Dk. Magufuli kila alipokuwa anaitwa alikuwa akirukaruka jukwaani na kisha kuanza kuhutubia.

Akiwa wilayani Kilolo, baada ya kurukaruka jukwaani, alimpigisha ‘push up’ mgombea ubunge wa jimbo hilo, Venance Mwamoto huku akisema kufanya hivyo ni ishara ya wagombea wa CCM wako imara.

“CCM ipo imara pamoja na wagombea wake wote kuanzia urais, ubunge na  udiwani, ndiyo maana tunaanza hivi ili Watanzania waone tuna kiu ya kweli ya kuwaletea maendeleo,” alisema.

 

Nape: CCM si malaika

Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema CCM inaongozwa na watu na si malaika ambao wapo sahihi kila wakati na kwa kila kitu.

“Tunajua Watanzania wanahitaji mabadiliko, tunaamini hakuna wa kuyaleta zaidi ya Dk. Magufuli ambaye ataongoza Serikali na chama chetu ili kiwe imara zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, William Lukuvi, aliwataka Watanzania kutochagua rais wa mbwembwe, ispokuwa wachague rais kwa sifa zake hasa Dk. Magufuli.

 

Mwisho

 

Ajali yaua watano

Na Walter  Mguluchuma, Katavi

 

WATU watano wamefariki dunia papo hapo na  wengine kadhaa kujeruhiwa wilayani Mlele Mkoa wa Katavi, baada ya gari walilokuwa wakisafiria  kupinduka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi,  Dhahiri  Kidavashari alisema  ajali hiyo ilitokea jana saa 9 alasiri katika  Kijiji cha Matandalani.

Alisema  ajali hiyo, ililihususha gari aina ya Noah lenye namba  za usajili T451 DDP  lililokuwa likiendeshwa na Justine  Ndayele (24) mkazi  wa Mkoa wa Kigoma.

Alisema  gari hilo  mali ya  Adamu  Omary,  lilikuwa likitokea  Mpanda mjini kwenda Kijiji cha Sitalike.

Aliwataja waliofariki dunia kuwa  ni Lunyalaja  Nzugamrwa (50), Furaha  Edward (35), Eva Mwanisawa (25), Maiko  Jacob wote wakazi wa Kijiji cha Sitalike na Mwila Kifwewe (25) mkazi wa mtaa wa Kawajense mjini  Mpanda.

Alisema miili ya marehemu hao, imehifadhiwa katika  Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.

Kamanda Kidavashari,  aliwataja majeruhi kuwa ni Felista  Matunda (30) mkazi wa tarafa ya Inyonga,Thobias  Kisila (65) mkazi wa Kijiji cha  Sitalike, Velina Libaratu (9) mkazi wa Mpimbwe,Odila  Lenatusi (19), Ndila  Kameme (32) wote wakazi wa mtaa wa Nsemlwa.

Alisema majeruhi hao, wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda wakiendelea  na matibabu.

Alisema jeshi hilo, linamshikilia  dereva wa gari hilo na kwamba upelelezi wa tukio hilo  utakapokamilika dereva huyo atafikishwa mahakamani.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles