26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Siwezi nikatawala nchi ya machozi

  • Asema hawezi kutawala watu wanaosikitika, wenye unyonge, aeleza machungu aliyoshuhudia gerezani Butimba, aagiza polisi wasiwaonee raia wanyonge kwa kuwabambikia kesi

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amesema hawezi kutawala nchi ya machozi na kuendelea kuona wananchi wanyonge wakionewa kwani walipomchagua waliamini anaweza kutatua shida zao.

Akizungumza jana na wananchi wa Kongwa mkoani Dodoma, alisema hali aliyokuta katika Gereza la Butimba jijini Mwanza ilimsikitisha na huenda ipo pia katika magereza mengine nchini.

“Mlinichagua kwa ajili ya watu wote, hasa wanyonge wanaopata shida, siwezi nikatawala nchi ya machozi, machozi haya yataniumiza, siwezi nikatawala watu wanaosikitika wako kwenye unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa.

“Nitaendelea kuwa mtumishi wenu, namuomba Mungu aendelee kunilinda kazi hii isinifanye nikawa na kiburi, nikawe mtumishi wa kweli bila kupendelea mtu na huruma ya kweli ya upendo wa Mungu ikanijae katika moyo wangu,” alisema Rais Magufuli.

Alitoa mfano wa mahabusi aliyefahamika kwa jina moja la Kulwa ambaye alibambikiwa kesi ya mauaji kwa sababu ya kushindwa kutoa hongo ya Sh milioni moja alipokuwa akienda kuuza mafuta yake.

“Nilimkuta kijana alishikwa na dumu la mafuta anataka kwenda kuuza akakamatwa njiani, akaombwa atoe hongo ya Sh milioni moja akasema hana, mafuta yenyewe akiuza hapati hata Sh 300,000 akawaomba awape Sh 200,000 abaki na 100,000 wakamwambia utakwenda kujifunza.

“Akapelekwa gerezani na kusomewa kesi ya mauaji, ana miaka yuko mle (Butimba). Mifano ni mingi.

“Nilisikitika sana na inawezekana hiyo hali niliyoiona kwenye gereza hilo ndiyo hali ya magereza yetu nchini, nilikuta wafungwa ni 1,000 lakini mahabusi walikuwa 925 karibu nusu kwa nusu.

“Nilikuta watu wengine wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka minane, ameshtakiwa kwa kesi ya kawaida tu, labda amegombana na mke wake au amesingiziwa wizi wa kuku.

“Kila siku wanasema upelelezi unaendelea na hawa watu wameendelea kuhangaika, kwenye magereza ni shida na wengine kesi zao ni kama hazipo,” alisema.

Aliiagiza Wizara ya Katiba na Sheria na vyombo vingine vinavyohusika na mahakama kuendelea kutembelea magereza na kuzungumza na watuhumiwa, hasa walioko mahabusu ili ambao hawapaswi kuendelea kukaa gerezani waachiwe kwa mujibu wa sheria.

“Leo (jana) walisema watakwenda katika Gereza la Kasungamile na Geita, wakimaliza kule nataka waende kila mkoa ili watu hawa maelfu ambao wako kwenye magereza wakisubiri hatima zao wanaowekwa kwa kuonewa waweze kutolewa.

“Niwaombe polisi wasiwaonee raia wanyonge kwa kuwabambikia kesi, si kitu kizuri, ni lazima tumwogope Mungu, sisi wote ni watoto wa Mungu,” alisema.

KUHAMIA DODOMA

Rais Magufuli alisema waliamua kuenzi ndoto ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1973 ambaye aliamua makao makuu ya nchi yawe Dodoma.

“Wakati huo mimi nilikuwa darasa la sita, mpaka nimemaliza sekondari, chuo kikuu ndoto hii ilikuwa haijatimia, ndiyo maana mliponichagua kuwa rais nilisema lazima ndoto ya Baba wa Taifa iweze kukamilika.

“Serikali yote imeshahamia hapa na mimi ni bahati mbaya wakati najiandaa kuhama mama yangu akaugua ghafla akapata ‘stroke’, kwahiyo inabidi nimhudumie,” alisema Rais Magufuli.

Alimpongeza Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa kazi nzuri anayoifanya ambapo kamati aliyoiunda kuchunguza sekta ya madini imewezesha kuongezeka kwa makusanyo kutoka Sh bilioni 191 hadi bilioni 311.

 “Inawezekana ana makosa yake, hatuchagui malaika na ukitaka kuchagua malaika kufa nenda mbinguni utawakuta malaika huko, lakini mimi nawaambia huyu (Ndugai) amelisaidia taifa,” alisema Rais Magufuli.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli pia alitoa Sh milioni 5 kusaidia Shule ya Msingi Sagala ambayo imeezuliwa mabati na kuwahamasisha viongozi mbalimbali ambao waliahidi kuchangia zaidi ya Sh milioni 6.

NDUGAI

Mbunge wa Kongwa, Ndugai alisema historia ya Kongwa inapaswa kutunzwa kwani ndiyo ilikuwa kitovu cha ukombozi wa Kusini mwa Afrika na kambi ya kwanza ya wapigania uhuru ilianzishwa hapo.

“Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Msumbiji waliishi hapa na kuondoka salama na walikomboa nchi zao kwa baraka za Kongwa, hivyo ina historia kubwa sana ambayo inapaswa kutunzwa isije ikapotea,” alisema Ndugai.

Aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo kama afya, maji na elimu ambayo imewezesha kuboreshwa huduma za kijamii jimboni humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles