30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Siendi ikulu kusaka utajiri – Magufuli

256 NA BAKARI KIMWANGA, KILIMANJARO

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema haombi nafasi ya urais kwa ajili ya kutafuta utajiri.

Akizungumza na wananchi katika mikutano yake ya kampeni iliyofanyika wilaya za Siha, Hai na Moshi mkoani Kilimanjaro jana, Dk. Magufuli alisema lengo lake ni kutaka kuleta mabadiliko ya kweli ya maendeleo kwa Watanzania.

Dk. Magufuli alisema suala la utajiri na kujilimbikizia mali, si utamaduni wake, na kama angeutaka, angeupata kupitia Wizara ya Ujenzi anayoiongoza, ambayo hutengewa mabilioni ya fedha kwenye bajeti ya kila mwaka.

Alisema akiwa Waziri wa Ujenzi, amefanikiwa kusimamia fedha za umma na kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa, hasa ujenzi wa barabara nchi nzima.

“Mimi siombi urais ili nipate utajiri, kama utajiri ningeupata Wizara ya Ujenzi ambayo hutengewa mabilioni ya fedha kila mwaka, nilisimamia kwa uadilifu, kazi yangu inaonekana kwa kila Mtanzania.

“Jamani msema kweli ni mpenzi wa Mungu, sitaki kusema uongo, sitaki kwenda Ikulu kwa jambo jingine, ila nataka niwafanyie kazi iliyotukuka Watanzania. Mimi kwangu ni kazi tu,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema Serikali yake itaimarisha ajira kupitia sekta ya utalii kwa vijana katika mikoa hiyo ya Kanda ya Kaskazini ili waweze kunufaika na kazi yao ikiwamo upagazi.

Akiwa wilayani Arumeru, alizungumzia upanuzi wa barabara ya Arumeru hadi Arusha Mjini.

Alisema tayari Serikali imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya fidia kwa watu ambao maeneo yao yatapitiwa na barabara.

“Ninataka kuifanya Usa River kuwa ya kisasa zaidi, tutaanza na kujenga kilometa 42.4 kwa lami na kazi hii tutaanza nayo mapema mwaka kesho,” alisema.

 

JIMBONI KWA MBOWE

Dk. Magufuli akiwa katika Jimbo la Hai lililokuwa chini ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe aliyemaliza muda wake, aliwataka wananchi kuchagua mbunge makini na si mtalii na mfanyabiashara.

Alisema kutokana na hali hiyo, jimbo hilo halina maendeleo zaidi ya wananchi kukamuliwa kwa kodi na ushuru wa kila aina.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Stendi ya Bomang’ombe, Dk. Magufuli, alisema jimbo hilo limekuwa halina uwakilishi mzuri na hata kushindwa kutetewa katika vikao vya halmashauri na bungeni.

Alisema anataka Hai ipae juu ndiyo maana  akiwa Waziri wa Ujenzi alihakikisha anapeleka mbele maendeleo na kuhakikisha anaweka lami katika barabara ya Masama.

Dk. Magufuli aliwataka wananchi hao wa Hai kuhakikisha wanampa kura za kutosha ili awe rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumchagua Danstan Mallya kuwa mbunge.

 

  1. NCHIMBI

Akizungumza katika mkutano uliofanyika wilayani Siha, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC), Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema nchi aihitaji rais nyoronyoro, legelege na mpole.

Alisema Watanzania wamechoshwa na uzembe, ubadhirifu ambao unaweza kukomeshwa na Dk. Magufuli.

“Kwa miaka 10 iliyopita tuliahidi kutenga asilimia tano ya fedha kwa vijana, lakini hazifiki, mtu mmoja anajifungia ndani na kula fedha. Sasa hawa kiboko yao ni Magufuli.

“Watanzania wanapata faraja kutokana nawe Magufuli, haya yanatokana na uamuzi wake wa kuchukua hatua kwa wakati,” alisema.

Kwa upande wake mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, Christopher Ole Sendeka, alisema Magufuli ni kielelezo cha uadilifu, uaminifu na uchapakazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,391FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles