25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Nilikataa vimemo vya uteuzi

magu

Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amefichua madudu ya namna mtandao katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ulivyokuwa ukipokea hongo ya fedha kwa ajili ya kutoa nafasi za uteuzi wa wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri.

Alisema mtandao huo wa watu watatu ulikuwa na kazi ya kupenyeza majina, lakini hawakufanikiwa kwa kuwa alihakiki jina moja baada ya jingine na kulazimika kulala saa nane hadi tisa usiku kwa ajili ya kazi hiyo.

Kutokana na kuwepo kwa mtandao huo, amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhandisi Mussa Iyombe, kuwashughulikia watu hao na kwamba tayari mchakato wa kuwaondoa umeanza.

Kauli hiyo aliitoa jana Ikulu Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na wakurugenzi wateule wa majiji, manispaa na halmashauri za wilaya kabla ya kula kiapo cha uadilifu katika utumishi wa umma.

“Nafasi hii ya ukurugenzi ni muhimu sana katika kujenga uchumi wa wananchi, lakini katika miaka ya nyuma ilikuwa inatumika kwa ‘robbing’ ya ajabu sana… kupata ukurugenzi ni mpaka watu wanahonga pesa.

“Palikuwa na watu fulani pale TAMISEMI walikuwa wamejipanga, na bahati nzuri nimeshamwambia Katibu Mkuu wa TAMISEMI na wizara wawatoe wote, nina uhakika wameshaanza ‘process’ (mpango).

“Nilipoamua TAMISEMI iwe chini yangu moja kwa moja, nilikuwa nina makusudi. Kutokana na taarifa zilizopo na mimi nimejiridhisha, kila mmoja jina lake nimelipitia na ninaweza kuwaita kwa majina mkashangaa.

“Wapo waliotaka kupenyeza majina, lakini yote nikayatupilia mbali, mimi ndiye ninayewafahamu, nataka ninyi mkawatumikie vizuri wananchi, imani izae imani… hamuhitaji kushangiliwa, wananchi watawashangilia mkitekeleza vizuri wajibu wenu.

“Ukiona unashangiliwa na adui, rudi nyuma jiulize umekosea wapi, ukiona unasemwa na adui ujue kuwa umewatwanga,” alisema.

Alisema mchakato wa kuwapata wakurugenzi hao ulikuwa mgumu na kwamba hakubahatisha kuwachagua.

“Kati ya wakurugenzi 185, wa zamani waliorudi ni 60, 120 wote wamebaki, wale 60 ni majembe. Nikisema nimechagua, nimechagua kweli kweli na ndiyo maana mimi sitembei, wakati mwingine nalala saa nane hadi tisa usiku nikichambua majina yenu.

“Nimewaamini mkaitumikie vizuri, watachonga weee mwishoni watachoka na Mungu akatimize mapenzi yake. Wananchi wamechoka, wanateseka, yapo majaribu yatakayokuja mbele yenu na wapo wanasiasa watakaowajaribu,” alisema Rais Magufuli.

Aliwatahadharisha wakurugenzi hao kuwa wasipokuwa makini na fedha za Mfuko wa Barabara, kila diwani atakuwa mhandisi.

FEDHA ZA ELIMU BURE

Akizungumzia kuhusu fedha za elimu bure, alisema wamekuwa wakitoa Sh bilioni 18.7 kila mwezi, lakini wako wakuu wa shule ambao wameona ni nyingi huku wengine wakizitumia vibaya.

“Kuna wakuu wa shule wameshaona hizo fedha ni nyingi, wengine wameshaanza kutumia vibaya wanaandika majina feki sasa haya ni majukumu yenu mkasimamie,” alisema.

WALIMU KUKATWA MISHAHARA

Rais Magufuli pia aliwaagiza wakurugenzi hao kuwakata mishahara walimu ambao madawati katika shule yatavunjwa.

“Mkahakikishe shule zote katika halmashauri zenu zinakuwa na madawati na mtengeneze orodha, endapo madawati yataharibiwa au kuvunjwa yule mwalimu husika akatwe mshahara,” alisema.

Alisema kuna wakurugenzi wamekuwa wakiingia mikataba na wafanyabiashara wanaowafahamu huku wakitoa tenda kushinda zabuni.

Aliwataka wakurugenzi hao kupinga kodi za ajabu wanazolipishwa wananchi wa maisha ya chini.

“Kumekuwa na kodi na kero za ajabu ajabu, mkapinge hizo kodi ndogondogo; utakuta kina mama wauza mchicha wamepanga barabarani nao wanalipishwa kodi, wakati analima na kumwagilia hukumsaidia mbolea wala maji… ninawaomba mkazuie hizo kodi,” alisema.

KIAMA KWA MIUNGU WATU

Kiongozi huyo wa nchi aliwataka wakurugenzi hao kutumia madaraka yao kuwaondoa watumishi ambao wanajifanya miungu watu kwenye vijiji, kata, tarafa na wilaya.

‘SITAKI KUJUTA’

Alisema hataki siku moja aumie na kujuta kuwa alifanya makosa kuwachagua.

“Sitaki siku moja niumie, nijute kuwa nilifanya kosa au nilimweka huyu kimakosa, nitaumia sana, nimewaacha wengi nikawachagua ninyi,” alisema.

HAANGALII UZOEFU

Alieleza kushangazwa kwa kitendo cha baadhi ya watu kulalamika kuwa aliowachagua hawana uzoefu.

“Kwenye mitandao ya kijamii nasikia kuna watu wanalalamika nachagua watu wasio na ‘experience’, mimi sitaki mambo ya ma-experience, experience tu, siwezi kuchagua mtu mwenye experience wakati ni mwizi.

“Ukiona katibu tarafa ha-move mtoe, Tanzania tuna wasomi wengi tuachane na haya ma-experience hata Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), hajawa hata waziri kwani hawakuwepo waliotaka uwaziri mkuu, tuachane na hizi historia, ni wakati wa kufanya kazi, dunia imebadilika lazima tuende kwenye speed ya sasa… wadhihirisheni kuwa ninyi mnaweza kuliko walivyofikiria.

“Kuna watu walijipanga na kutuma vimemo ili watu wao wachaguliwe kwenye nafasi hizo, nikawafutilia mbali wote waliotumwa na waliowatuma. Lengo kubwa sisi tuna ahadi ya kuwatumikia wananchi wetu kwa miaka mitano, tuna ilani yetu ya uchaguzi,” alisema.

MKURUGENZI ALIYEZUSHIWA

Alisema amekuwa akifuatilia taarifa zinazoandikwa katika  mitandao ya kijamii na alishangazwa alipoona aliyemteua kuwa Mkurungezi wa Itigi mkoani Singida, Pius Luhende kuwa anafanya kazi hotelini.

“Wakati mwingine nikiona comment zingine mitandaoni huwa nacheka wee, mwingine anauliza jina la fulani afanya kazi hotelini ana certificate ya hoteli wakati ana diploma na ana masters na alikuwa mkaguzi wa kanda,” alisema huku akimsimamisha Luhende na kuwataka waandishi wa habari wapige picha vyeti vyake.

HAKUCHAGUA VILAZA

Alisema yeye hakuchagua vilaza na kwamba haikuwa ajabu alipowataka wapeleke vyeti vyao Ikulu.
“Wengine wanahoji kwanini tumewaambia mje na vyeti, kwani kuna ubaya gani kuomba vyeti, hatukuchagua vilaza najua hili jina hawalipendi,” alisema Rais Magufuli.

EFDs

Aliwataka wakurugenzi hao kwenda na mashine za kielektroniki (EFDs) kwenye halmashauri zao ili wazitumie kukusanya mapato.

Pia aliwaagiza  makatibu wakuu wote wa wizara kutumia mashine hizo katika kukusanya mapato serikalini.

“Vyombo vya Serikali lazima vianze kutumia mashine za EFDs, pia makatibu wakuu wote wa wizara mtumie mashine hizi katika kukusanya mapato ya serikali. Haiwezekani tunahamasisha halafu hatutumii lazima tukatoe mfano.

“Kuna watu wanalalamika fedha zimepotea. Fedha zitafunguka mkifanya kazi. Kuna waliozoea fedha za bure na uwizi, kuna ambao walikuwa wakienda baa wanalipiwa kiti chake hata kama hajafika, hiyo itaisha sasa, no work no money, hazitapatikana bila kufanya kazi,” alisema.

ATUMBULIWA KIMYA KIMYA

Wakati wakurugenzi hao wanatakiwa kuapishwa na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda, inadaiwa kuwa Hidaya Usanga aliyepangiwa Tarime Mji, alitolewa kwa madai kuwa uhakiki wake haukukamilika.

Gazeti hili lilipomtafuta Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mussa Iyombe ili kuzungumzia juu ya hilo, alisema hana taarifa hizo.

SITA HAWAKUJITOKEZA

Hata hivyo, Iyombe aliliambia gazeti hili kuwa anachofahamu ni kuwa wakurugenzi sita hawakuhudhuria hafla hiyo ya uapisho.

“Sina taarifa hizo, ninachofahamu ni kwamba wakurugenzi sita hawaku-appear  kwenye uapisho na hatuna taarifa zao,” alisema Iyombe.

MAJALIWA

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka wakurugenzi hao kusimamia fedha za maendeleo katika halmashauri zao.

SAMIA

Naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wakurugenzi hao kufanya kazi pamoja na madiwani kwa kuwa ni Bunge lao.

KAIRUKI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Angela Kairuki, aliwataka wakurugenzi hao kabla ya kwenda kwenye maeneo yao ya kazi, kukabidhi taarifa zao za benki pamoja na kuonyesha nyumba zao.

CHADEMA YAMVAA  JPM

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeshangazwa na kitendo cha Rais Magufuli kuwataka wakurugezi kuwakata mishahara walimu endapo madawati yatavunjwa.

“Kwani walimu hao wanajua ubora wa madawati hayo? Wanajua yametengenezwa wapi? Walihusishwa katika mchakato wa manunuzi?” alihoji Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji.

Alisema adhabu ya kumkata mtu mshahara katika utumishi wa umma ni kubwa sana, ni sawa na kumfukuza mtu kazi.

“Kwanini adhabu zingine kama kupewa onyo kali zinarukwa? Ni kama rais hatambui kuwepo kwa sheria au la awe anaandikiwa hotuba,” alisema Dk. Mashinji.

Pia alisema kitendo cha rais kubeza suala la uzoefu katika utendaji na ufanisi wa kazi ni jambo la hatari.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles