NaVeronica Romwald, Dar es Salaam
KITENDO cha kusalimia kwa kushikana mikono kilichofanywa na Rais Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa, kimeibua mjadala mzito.
Viongozi hao waliopambana vikali katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, walikutana kwa mara ya kwanza juzi katika hafla ya Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 ya ndoa ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe Anna.
Hafla hiyo ilifanyika katika Kanisa la Mtakatifu Peter, Oysterbay, Dar es Salaam ambako viongozi mbalimbali walialikwa.
Kutokana na tofauti za msimamo ya vyama vyao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliko Rais Magufuli na kile cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliko Lowassa hivi sasa baada ya kujiengua CCM, watu wengi hawakutarajia kitendo hicho.
Lowassa alihama CCM na kwenda Chadema kwa kile alichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na mchakato wa kumteua mgombea wa nafasi ya urais, huku Rais. Magufuli akiteuliwa wakati huo kuwania urais.
Siku kadhaa zilizopita, Chadema kilitangaza kufanya operesheni kubwa kiliyoipa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) ambayo itaambatana na maandamano na mikutano nchi nzima kuanzia Septemba mosi.
Hata hivyo, Serikali imepiga marufuku maandamano kupitia jeshi la polisi.
Wakizungumza na MTANZANIA jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya wasomi na wanazuoni walipongeza kitendo kilichofanywa na viongozi hao kwamba kimeonyesha ukomavu wa siasa, huku wakiamini huenda ni hatua nzuri ya kufikia mwafaka.
SEMBOJA
Mtaalam wa Masuala ya Uchumi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Joseph Semboja alisema kitendo kilichofanywa na viongozi hao kimemfurahisha mno kwa vile kimeionyesha dunia kuwa Watanzania ni watu wenye amani na upendo.
Alisema hatua hiyo imeonyesha Watanzania wanaweza kuwa na tofauti, wakaendelea kuishi pamoja na kushirikiana katika mambo mbalimbali ya jamii kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa lao.
Profesa Semboja aliwataka wananchi kujifunza kutokana na kitendo kilichoonyeshwa na viongozi hao.
Alisema si vizuri kutumia mfumo wa jino kwa jino kwa vile utaratibu huo ndiyo unaoweza kusababisha kukua zaidi migogoro na wakati mwingine unasababisha umaskini kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwa sababu muda mwingi wananchi hawana muda wa kushiriki katika shughuli za maendeleo kutokana na migogoro.
WANGWE
Profesa Samwel Wangwe alisema hatua hiyo ni ishara kwa Watanzania ambao wanapaswa kujifunza kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa ya kuleta muafaka katika mgogoro wowote kuliko kutunishiana misuli.
“Mazungumzo yana nguvu kubwa katika kuleta upatanishi katika migogoro mbalimbali inayotokea katika jamii kuliko kutumia njia nyingine ambazo zinaweza kusababisha vurugu na uharibifu wa mali za watu na upotevu wa maisha ya watu,” alisema.