Na Dennis Luambano, Dar es Salaam
KATIKA kisa mkasa cha wiki iliyopita kwa maana toleo la Desemba 4, mwaka huu niliakisi namna baadhi ya wateule wanavyoendelea kuugua homa ya kufurushwa. Kwamba wateule hao wa Rais Dk. John Magufuli wanapata usingizi wa mang’amung’amu kutokana na jinamizi la kufurushwa. Wanapata usingizi huo na kuishi kwa wasiwasi kutokana na mtindo wa ufanyaji kazi wa Magufuli kiasi kwamba hakuna anayejua kesho yake.
Nilisema kwamba wakati wateule hao wakipata usingizi huo, pia kuna baadhi ya watu wengine wakiwamo wanasiasa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanapata usingizi kama huo kutokana na kiwewe cha pengine watateuliwa kushika nyadhifa hizo baada ya wenzao kufurushwa.
Pia nilisema wanaoongoza kwa sasa kupata usingizi huo ni wakuu wa mikoa na wilaya kwa sababu hawana uhakika wa kuudumu katika nafasi zao kwa sababu anaweza kufanya mabadiliko muda wowote ule kwa kadiri atakavyoona inafaa na ndiyo maana wanajitutumua ili utendaji wao uonekane unaendana na kasi yake.
Sasa ili waonekane wanaenda sawa na kasi yake, Oktoba mwaka huu, baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya walitangaza kuanza mapambano ya kuwang’oa wamachinga katika maeneo yao ya biashara kwa kile walichodai kuwa hayakuwa rasmi.
Kimsingi, mapambano hayo yalipingana na agizo la Magufuli la kutaka wasisumbuliwe na waachwe waendelee na shuguli zao kama kawaida. Magufuli alitoa agizo hilo Agosti, mwaka huu katika mikutano yake ya hadhara aliyoifanya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa alipokwenda kujitambulisha baada ya Julai 23, mwaka huu kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Aliyeanza kutoa amri ya kuwaondoa, alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, baada ya kudai ni kutokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dar es Salaam kupoteza mapato ya zaidi ya Sh bilioni 100 kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanakwepa kodi kwa kuwapa bidhaa wamachinga ili kuziuza barabarani.
Siku moja baada ya Makonda kutoa agizo hilo, baadhi ya wamachinga walionukuliwa na vyombo vya habari walidai kuwa hawataondoka katika maeneo hayo hata kama watapigwa mabomu ya machozi kwa kuwa ndiko ambako bidhaa zao zinanunuliwa zaidi na wateja wao kuliko maeneo mengine waliyotengewa na Serikali.
Walichokisema wamachinga hao ndicho walichokimaanisha kwa sababu hawakuondoka katika maeneo hayo.
Si wamachinga wa Dar es Salaam peke yao, bali hata wa mikoa mingine mikubwa ikiwamo Mbeya na Arusha walishaambiwa waondoke, huku wale wa Mwanza walianza kuondolewa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Sasa kuthibitisha kwamba Magufuli hatafuni maneno yake, ni pale Jumanne wiki hii alipotoa agizo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mussa Iyombe, kusitisha mara moja utekelezaji wa mpango wa kuwaondoa wamachinga jijini Mwanza pamoja na mikoa mingine hadi hapo mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa.
Agizo hilo alilitoa Ikulu akiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, pia alionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo aachie ngazi.
“Kumeibuka tabia ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwafukuza wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya biashara, wakati mwingine wanawafukuza wachimbaji wadogo katika maeneo wanayofanya shughuli zao na pia wanawafukuza wafugaji katika maeneo wanayolisha mifugo yao, hili si sawa.
“Sipendi wamachinga wafanye biashara katika hifadhi ya barabara lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwa utaratibu wa namna hiyo, maana yake tunaanza kutengeneza madaraja ya Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa katikati ya mji, huo si mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo mimi na makamu wa rais tulipita kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na nataka kulirudia kwa mara ya mwisho,” alisema.
Pia ameelekeza kuwa wamachinga walioondolewa katika maeneo yao Mwanza, waachwe waendelee na shughuli zao hadi hapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
“Narudia na hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata wamachinga wa Mwanza warudi katika maeneo yao hadi watakapowatengenezea utaratibu mzuri, Kigamboni (Dar es Salaam) hapa palikuwa na wamachinga eneo fulani wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundombinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri na waliwashirikisha viongozi wa wamachinga, lakini Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa hapa kazi tu, mimi sikusema msemo wa hapa kazi tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa,” alisema.
Kimsingi, agizo la Magufuli kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ni hadhari kwao kwamba yeye hana ubia nao bali ana ubia na Watanzania wanyonge wakiwamo wamachinga ambao ndio wapiga kura na hakuna atakayemzuia kuwatumbua muda wowote atakaoona unafaa na kwa maana hiyo nadhani ule usingizi wa mang’amung’amu utaendelea kuwatesa kwa kuhofia kutumbuliwa.
Pia namshauri Magufuli aendelee ‘kuwafunga spidi gavana’ wateule wake wanaotekeleza majukumu yao kwa pupa, sifa na bila kutumia busara ili wasionekane mizigo, kwa sababu baadhi yao wanakwenda mbali zaidi kwa kuvuka mipaka ya utendaji wao na kujifanya ‘viumbe mungu’, wababe na kutisha watu kutokana na kutumia amri zao vibaya za kuwapeleka mahabusu watu kwa saa 24.
Vitendo hivyo viliifanya Tume ya Utumishi wa Umma kuibuka hivi karibuni na kutaja mamlaka sita tu zenye dhamana na madaraka ya kuwachukulia watumishi wa umma hatua za kinidhamu.
Mamlaka hizo ni Rais, Waziri wa Tamisemi, Katibu Mkuu Kiongozi, watendaji wakuu, wakuu wa idara na divisheni na mamlaka za Serikali za Mitaa (mabaraza ya madiwani).
Tume hiyo ilitaja mamlaka hizo baada ya mwenendo wa baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kutumia vibaya madaraka yao kwa kuwatisha watumishi wa umma na kuwatolea lugha za maudhi na udhalilishaji.
Kwa mujibu wa Katibu Msaidizi wa Tume hiyo, Enos Mtuso, alisema mamlaka hayo yanatokana na Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003.