21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

MAGUFULI AWAPA SOMO MABALOZI

NA ANDREW MSECHU,  DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli, amewaeleza mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao na mashirika ya kimataifa sababu tano za kutekeleza mradi wa maji wa Stigler’s Gorge, huku akigusia mafanikio ya mazungumzo ya makinikia na kutaka uwekezaji zaidi kwenye madini.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam, alipokuwa akishuhudia ukabidhiwaji wa hati 62 za viwanja vya makazi na ofisi kwa balozi mbalimbali na tano kwa mashirika ya kimataifa. Kila kiwanja kina ukubwa wa ekari tano.

 UZALISHAJI UMEME

Rais Magufuli alisema kwa sasa uzalishaji umeme kwa nchi nzima kwa kutumia vyanzo vyote vilivyopo ni karibu megawati 1,560, wakati viwanda vinavyohitaji kutumia nishati hiyo vikiongezeka.

Alisema hadi wakati alipokuwa akizungumza jana, kumekuwa na ongezeko la viwanda vidogo 3,306 lakini umeme bado ni ule ule, ukitarajiwa kuongezeka kwa megawati 300 katika mradi wa Kinyerezi kwa msaada wa Japan, ambao pia bado hautoshi.

“Ndiyo maana tumeamua kujenga Bwawa la Stigler’s Gorge ambayo ni ndoto ya Baba wa Taifa tangu mwaka 1975 na litazalisha megawati zaidi ya 2,100 ambayo ni karibu mara mbili ya tunaozalisha sasa.

“Itakapokamilika, tutawezesha kuharakisha viwanda, kusaidia umwagiliaji na kusaidia wanyama waliopo kule kupata maji ya uhakika na kwa urahisi, kwahiyo tutaua ndege karibu watano kwa jiwe moja,” alisema.

Rais Magufuli alisema katika tathmini ya athari za mazingira iliyofanywa, inaonyesha eneo litakalotumika ni asilimia 3.5 pekee la eneo la Hifadhi ya Taifa ya Selous na wanyama waliopo kwenye hifadhi hiyo wakiwamo tembo watasalimika kwa kuwa na uhakika wa maji.

Alisema kwa sasa tembo hao wamekuwa wakizunguka na kuzurura hovyo kwenye maeneo ya hifadhi hiyo kutokana na kutawanyika kwa maji, hivyo kuuawa hovyo na majangili, lakini mradi huo utakapokamilika utawafanya wawe kwenye eneo moja salama lenye uhakika wa maji ya kutosha kila mwaka.

Rais Magufuli alisema kukamilika kwa bwawa hilo kutasababisha bei ya umeme kushuka, hivyo kuvuta wawekezaji zaidi katika viwanda, hatua itakayosababisha kuzalisha ajira kwa watu wanaozunguka bila ajira na zaidi itasaidia Serikali kuongeza mapato yake ya kodi kutokana na uzalishaji kuongezeka.

 MADINI YA TANZANITE

Alisema Tanzania ina madini kila mahali na jana, kabla ya hafla hiyo alibahatika kukutana na balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu na kuzungumza naye, akimuhoji kuhusu nchi yake kuwa kinara wa uuzaji wa madini ya Tanzanite wakati haina hata mgodi mmoja wa madini hayo.

Rais Magufuli alisema Kazungu aliyewahi kuwa waziri wa madini wa Kenya kama miaka saba kabla hajawa balozi, alimweleza kuwa jibu ni jepesi kwamba ‘hatulindi Tanzanite yetu, hivyo watu huiba, kuvuka mpaka na kwenda kuuza huko (Kenya)’.

Alisema alimweleza kuwa ‘sasa muda umefika wawekezaji wa Tanzanite wa Kenya waje wawekeze nchini, hata kama ni kuchimba ili nasi tupate asilimia yetu’.

Rais Magufuli alisema kwa India inayoongoza kwa kuuza madini hayo kwenye soko la dunia lakini hawana hata mgodi mmoja wa Tanzanite, nao wawekezaji wake waje nchini wayaongeze thamani hapa ama wachimbe na kulipa kodi.

“Hiyo ndiyo Tanzania ninayoitaka mimi. Tumeingia makubaliano na kampuni zilizokuwa zikichimba dhahabu hapa na maendeleo si mabaya, ninamshukuru balozi wa Canada kwenye hili,” alisema.

Alisema anataka kila kitu kwenye uwiano sawa wa mafanikio – “win win situation” na kwamba kuna almasi ziko Shinyanga ambazo pia anataka kabla haijasafirishwa kwenda kwenye soko, ukubwa wake ujulikane na gharama yake ili kinachotakiwa kulipwa kilipwe.

“Hatuhitaji makubwa, tunataka sehemu tu ya kile tunachostahili,” alisema.

Rais Magufuli alisema kuna wakati mwingine anapojaribu kufanya hivi kwa sababu watu walitaka kuchukua vyote lazima walalamike, ila aliwataka mabalozi wawaelekeze watu wao kwamba Tanzania inahitaji kufanya biashara na kila mmoja kutoka Afrika, Asia, India, Ulaya, Marekani ila tu biashara iwe wazi.

Alisema hana shida na kampuni za nje kuwekeza na kupata faida kubwa, lakini anahitaji Serikali ipate haki yake ili iweze kusaidia kutoa huduma za jamii kwa uhakika na kusaidia watu masikini wa nchi hii.

 URANI NA MAKAA YA MAWE

Rais Magufuli alisema wameanza kutafuta uhakika wa umeme kwa chanzo hicho cha maji huku kukiwa na utajiri wa urani, ambayo inatarajiwa kutumiwa kama chanzo kingine cha nishati kwa siku zijazo, akitumia nafasi hiyo kukaribisha wawekezaji katika urutubishaji wa madini hayo.

“Kwahiyo, kwa yeyote anayehitaji kuja kuwekeza kwenye urani anakaribishwa, kwa kuwa sasa hivi tuna urani ambayo bado haitumiki, makaa ya mawe pia bado hayatumiki na sisi tuliona suala la haraka ni kuanza kutumia vyanzo vya maji kwanza,” alisema.

 UZURI WA DODOMA

Alitumia hafla hiyo kuwahamasisha mabalozi kwamba Dodoma inazidi kuwa sehemu nzuri ya kuishi na kuendesha shughuli zao, kwa kuwa Serikali imeamua kuifanya kuwa mji mkuu halisi.

Rais Magufuli alisema pamoja na kuunganishwa kwa miundombinu, uhakika wa umeme na maji, kuna shule za uhakika na ujenzi wa mji huo unaendelea ili kuboresha mazingira yake.

Alisema katika manispaa 21, halmashauri za miji 22, halmashauri za wilaya 137, halmahauri na majiji sita, unapozikusanya zote pamoja, Manispaa ya Mji wa Dodoma ndiyo inayoongoza kwa makusanyo kwa Tanzania nzima.

“Kwa takwimu tu, Dodoma imekusanya Sh bilioni 24.2 katika mpango wa makadirio ya awali ya kukusanya Sh bilioni 19, kwahiyo tayari wameshavuka lengo kwa kukusanya asilimia 123.5 ya mapato,” alisema.

Inaendelea……….JIPATIE NAKALA YAKO YA GAZETI LA MTANZANIA SASA!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles