30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli awapa rungu mabalozi wanayoiwakilisha Tanzania nje

Mwandishi wetu-Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amewataka mabalozi wa Tanzania wanaoiwakilisha nchi maeneo mbalimbali duniani, kuhakikisha wanafanya kazi ikiwa ni pamoja na kuleta nchini wawekezaji na wakikwamishwa na mtendaji ama wizara wamweleze.

Alisema hayo alipokutana na mabalozi 43 wa Tanzania walio nchini tangu Agosti 13 walipokuwa wakizungumza Ikulu, Dar es Salaam jana.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana, ilisema pamoja na Rais kuwaeleza hali ya uchumi wa nchi na maendeleo yanayopelekwa kwa wananchi, aliwataka kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika miradi yenye manufaa hapa nchini.

“Nataka mabalozi mtuletee miradi ya maendeleo, ifike mahali balozi ujiulize kwa kuwa kwangu balozi nimepeleka nini nyumbani? Nimewezesha kujengwa kiwanda? Kujengwa barabara? Kujenga daraja au jengo fulani?” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia kwa karibu masuala wanayoamini yana manufaa kwa nchi, ikiwemo uwekezaji na wasikubali kukwamishwa na viongozi ama wizara yoyote.

“Nataka muwe ‘very aggressive’, na ukiona mtu anakukwamisha mimi nipo, niandikieni uone kama hatakwama yeye, mimi nataka kuona vitu sio maneno maneno,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, mabalozi hao walimpongeza Rais Magufuli kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini.

Mabalozi hao wametembelea miradi ya ujenzi wa bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 katika Mto Rufiji, mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR) unaoanzia Dar es Salaam hadi Dodoma, jengo la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma (Ubungo Interchange).

Miradi mingine waliyoitembelea ni, mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, mradi wa usambazaji wa gesi (Taifa Gas), mradi wa udhibiti wa mawasiliano Tanzania na mradi wa ujenzi wa daraja la Tanzanite (New Selander Bridge) katika Bahari ya Hindi.

Kwa upande wa Zanzibar, wametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la biashara na makazi eneo la Michenzani, mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume, mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa wa Fumba Wilaya ya Magharibi, mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kaskazini – Bububu – Mkokotoni na mradi wa ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi katika eneo la Manga Pwani.

Mabalozi hao wameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo na juhudi nyingine kubwa zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali za huduma za jamii, zimeleta heshima kwa nchi na machoni mwa jumuiya ya kimataifa, na zimedhihirisha kufikiwa kwa malengo ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles