25.4 C
Dar es Salaam
Thursday, January 20, 2022

Magufuli awanyooshea kidole polisi magereza

NA AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, ametoa ujumbe mzito kwa Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza kwa kuinyooshea kidole idara yake ya fedha kuwa inasababisha malalamiko miongoni mwa askari kutokana na kutowalipa baadhi ya stahiki zao kwa wakati zikiwamo posho.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kuwa tunuku vyeti askari 513 waliomaliza kozi za maofisa na wakaguzi wasaidizi wa polisi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini alichoahidi pia kukipa Sh milioni 700 wiki ijayo kwa ajili ya ukarabati wake, Magufuli, alisema idara hiyo ya Jeshi la Polisi ambayo maofisa wake walibadilishwa miezi michache iliyopita bado haijakaa sawa.

“Kitengo cha fedha hakijakaa vizuri tangu wale waliokuwapo tulipowabadilisha wakawa Ma-RAS.

“Hadi sasa hivi hakiendi vizuri, kuna malalamiko mengi, kwa hiyo niwaombe wakubwa ukiwemo wewe IGP na wizara mkakiangalie vizuri kitengo cha fedha,” alisema.

Magufuli alisema miongoni mwa malalamiko yaliyopo kwa sasa ni malipo ya fedha za askari waliopelekwa Kibiti kufanya kazi maalumu wakati kulipokuwa na matukio ya mauaji ya raia.

“Malalamiko yaliyopo yanawavunja moyo askari, mfano hadi sasa askari walioenda Kibiti mkoani Pwani hadi leo hawajalipwa posho zao, lakini majeshi mengine yote yameshalipwa, nawaeleza hivi ili mjue maana hawa watu mnapishana nao wanawapigia saluti tu lakini wana malalamiko,” alisema.

Pia alisema hafahamu tatizo hilo linasababishwa na nani katika idara hiyo, lakini taarifa alizonazo ni kwamba ndiyo chanzo cha malalamiko na hata fedha nyingi zinazotumwa na Serikali wakati mwingine hazifiki kwa wahusika.

“Nimeona huu ni wakati mzuri wa kulizungumza hili, sina mahala pengine pa kulizungumza na msema kweli ni mpenzi wa Mungu, nataka Jeshi la Polisi na majeshi mengine kusiwe na malalamiko,” alisema.

Magufuli alisema anataka watu wanaofanya kazi katika majeshi nchini waishi kwa kujivunia na kazi zao kwa kuwa uaskari ni kazi ya heshima na kujitolea.

Pia alilitaka kufanya kazi kwa weledi na kusimamia vigezo vyake wakati wa kuajiri kwa kuwa matatizo mengi ya jeshi hilo yameanzia katika ajira.

“Baadhi ya watu mnaowaajiri hawana sifa za kuwa askari, unakuta mtu ni ndugu yake au rafiki hii ilianza kupoteza mwelekeo wa Jeshi la Polisi, unakuta OCD au RPC ana ndugu yake kule alifeli mahali popote, anasema mlete huyo nitampeleka Moshi anaenda kozi ya upolisi.

“Akishamaliza kozi ya upolisi hana nidhamu kwa sababu anajua bosi wake aliyepo pale ndiye atakuwa anamlinda, mtu hata akipewa amri na viongozi wake waliopo mkoani au wilayani hajali kwa sababu anajua kuna Godfather  anayemtegemea,” alisema.

Pia alisema baadhi ya watu hao hawana hata wito wa kuwa polisi na waliingia kwa sababu walikosa ajira mahala fulani.

“Ndiyo maana kama mtakumbuka kwa hawa maaskari ambao wapo Moshi wapo mia nane, IGP aliniomba kwamba anataka ajira mpya nikasema ajira hii wanatoka walioko JKT, kwanza wameshafundishwa vya kutosha ili kusudi wale wenye ndugu zao wanaotaka kuwaingiza kwa mgongo wa nyuma wawapeleke JKT wakasulubiwe.

“Nilifuatilia kweli, nina uhakika hakuna mtu aliyepitishwa kwa sababu hata Naibu Waziri (Masauni) alileta watu wake 11 hawakuingia jeshini na usifikiri sijui, nilifuatilia kweli, nasema uongo wameingia kwa hiyo nina fahamu ninachokifanya, nataka mtu anayeenda Jeshi la Polisi awe kweli na wito,” alisema.

MAANDALIZI YA UCHAGUZI

Katika hatua nyingine, alilitaka jeshi hilo kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi ukiwamo wa Serikali za Mitaa utakaoanza mwakani ili kuhakikisha unamalizika salama.

“Uchaguzi wakati mwingine unakuwa chanzo cha vurugu, jitahidini kusimamia maadili kuhakikisha chaguzi hizi zinamalizika salama,” alisema.

Pia alisema anaamini vyombo vya ulinzi na usalama ndiyo chanzo cha amani na utulivu wa nchi ambao wanasiasa wamekuwa wakijivunia.

“Jeshi la Polisi ni chombo muhimu, sisi wanasiasa tumekuwa tukijidai nchi yetu ina amani lakini wanaofanya hivyo ni nyinyi, najua wapo wanasiasa wanaowakejeli kwamba hamfanyi kazi lakini nyinyi ni muhimu,” alisema.

NYUMBA ZA ASKARI MAGEREZA

Kuhusu fedha za ujenzi wa nyumba za askari magereza jijini Dar es Salaam alizozitoa mwanzoni mwa mwaka huu alisema hakuna kinachoendelea.

“Pale magereza nilivyoenda nilitoa fedha za ujenzi wa nyumba za askari lakini hadi sasa nyumba hazipo na fedha sizioni, ndiyo maana nimefanya mabadiliko haraka haraka pale, nisingeweza kuvumilia mtu nimempa fedha halafu sioni chochote,” alisema.

Magufuli alisema yeye ni mvumilivu lakini katika mambo ya fedha huwa unamshinda.

“Unatoa fedha kwa ajili ya nyumba za  askari magereza, hakuna zinazojengwa na fedha umetoa, hujui zimeenda wapi, nimeshamwambia kamishna wa magereza azifuatilie ajue hizo fedha zimekwenda wapi, kama zilipotelea TBA (Wakala wa Majengo) zitajulikana, kama zilipotelea magerezani na zenyewe zilifungwa basi zifunguliwe ili kusudi zikafanye jukumu lake kwa sababu kama ni kufungwa zimefungwa vya kutosha,” alisema.

Awali, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema jeshi hilo limejipanga kuimarisha usalama wa wananchi na mali zake na aliwatahadharisha wanaotaka kufanya maandamano na mikusanyiko isiyo na maana.

“Ole wao wanaotaka kuandamana na kufanya mikusanyiko isiyo na maana, tunataka watu waheshimu sheria za nchi na viongozi,” alisema Masauni.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, alisema wamejipanga vizuri na uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Pia alisema kasi ya ukusanyaji wa mapato ndani ya jeshi hilo imeongezeka kutoka Sh bilioni 63.2 kwa mwaka jana hadi Sh bilioni 68.5 kwa mwaka huu

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,434FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles