28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Magufuli atumia Sh trilioni 161

ELIZABETH HOMBO

HIVI karibuni Bunge linatarajiwa kukaa na moja ya majukumu yake makubwa ni kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka 2020/21, ambayo itakuwa ya tano ya Rais Dk. John Magufuli tangu aingie madarakani Oktoba 2015.

Machi 11 mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliwasomea wabunge mapendekezo ya ukomo wa bajeti ya mwaka 2020/21 ya Sh trilioni 34.88, ambayo kwa uzoefu wa miaka minne, haitakuwa na mabadiliko makubwa na bejeti halisi itakayosomwa Juni.

Bajeti ya kwanza ya Rais Magufuli ni ile ya 2016/17 iliyokuwa ya Sh trilioni 29.5, ya pili 2017/18 Sh trilioni 31.7, ya tatu 2018/19 Sh trilioni 32 na ya nne 2019/20 Sh trilioni 33.1.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, bajeti ya mwaka huu itajikita zaidi kufanikisha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, kuendeleza ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na mradi wa umeme wa maji wa Mto Rufiji.

Kwa ujumla bajeti zote ikiwamo hii ya mwaka huu, kama haitakuwa na mabadiliko makubwa, ikipitishwa itafanya jumla ya Sh trilioni 161 ambazo zimekusanywa na kutumiwa ingawa karibu miaka yote bajeti inayopitishwa na Bunge huwa makusanyo hayafiki asilimia 100.

WACHAMBUZI

Akitoa maoni yake kuhusu bajeti hizo tano, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Richard Mbunda alisema tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani, kaulimbiu yake ilikuwa ni uchumi wa viwanda, hivyo bajeti zote zilitakiwa zionyeshe katika lengo hilo.

Alisema ni bahati mbaya kwamba kuna mapungufu, kwa sababu kama nchi inatakiwa kufikia lengo hilo, kulitakiwa kuwepo muunganiko kati ya sekta ya kilimo na viwanda.

“Bajeti zote zilionyesha kuwekeza zaidi katika mambo mengine kama elimu, afya ambayo nayo ni muhimu, ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa ndege kitu ambacho huwezi kufikia lengo hilo la kufikia uchumi wa viwanda,” alisema Dk. Mbunda.

Katika hilo, alishauri Serikali kuanzisha uwekezaji kwa kutenga bajeti kwa ajili hiyo ikiwa ni pamoja na kuelekeza kwenye utafiti wa kilimo.

“Serikali ichukue jukumu la kuwekeza kwanza, na bajeti itengewe kwa ajili ya uwekezaji, pia fedha zitengwe kwa ajili ya utafiti wa kilimo.

“Kwa sababu changamoto zinazowakumbuka wakulima wetu ni soko, bodi za mazao mchanganyiko na NFRA ziwe zinanunua mazao mikoani halafu baadaye wanakuja kuuza. Bodi za mazao mchanganyiko hii ndiyo kazi yake, lakini lazima ziwezeshwe kwanza ziwe na mtaji wa kutosha.

“Vilevile viwanda vinavyohudumia kilimo, vifaa viwe rahisi ili kumpunguzia mkulima kazi kubwa.

“Nina imani kukiwa na muunganiko mzuri kati ya sekta ya kilimo na viwanda, nchi yetu itapiga teke umasikini,” alisema Dk. Mbunda.  

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mwenyekii wa Jumuiya ya Wanataaluma wa chuo hicho (Udasa), Dk. George Kahangwa alisema wangependa kuona bajeti ya Serikali ikiwa na nyongeza ya kila mwaka ya mishahara.

“Kama Udasa tungependa kuona bajeti ya Serikali inarejesha haki ya kila mwaka ya mfanyakazi, yaani nyongeza ya mshahara irejee sasa,” alisema Dk. Kahangwa. 

MIRADI

Katika bajeti nne zilizopita, Serikali imejikita kwenye miradi mikubwa 12 ambayo mingine inaendelezwa na bajeti inayotarajiwa kupitishwa Juni.

Miradi hiyo ni pamoja na ununuzi wa ndege ambazo hadi sasa zimeshanunuliwa saba na mbili zinatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote, ujenzi wa reli ya SGR, mradi wa umeme wa maji wa Rufiji, barabara za juu Ubungo na ujenzi wa barabara mbalimbali nchini, ikiwamo njia sita kutoka Ubungo hadi Kibaha mkoani Pwani.

Pia utoaji elimu bure kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha nne unaoigharimu Serikali Sh bilioni 23.8 kila mwezi, ujenzi wa vituo vya afya 352 na hospitali 67 nchi nzima, ununuzi wa meli Ziwa Victoria na Nyasa, Daraja la Busisi, Mwanza na Daraja la Salender, Dar es Salaam.

Pamoja na miradi hiyo ambayo inatoa ajira kwa Watanzania wengi, pia ndani ya miaka minne sasa watumishi wa umma wamekuwa wakiomba kuongezewa mishahara.

Wakati wa Sikukuu ya Wafanyakazi Mei mwaka jana, Rais Magufuli aliwaambia wafanyakazi kwamba muda wake haujaisha.

“Naomba muamini kuwa subira yavuta heri, ningeweza tu kusema nawapandisha mishahara Sh 5,000 ama Sh 10,000, ni lazima tujenge uchumi ulio imara.

“Kwa mambo yanavyoenda, ninaamini kwa miradi hii inayotekelezwa, uchapakazi unaofanywa na wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi, tunaelekea pazuri, nimeamua kuwaeleza ukweli, sikutaka kusema hapa nimepandisha alafu mtakachokipata hakipo, lazima tujipange vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Pia Februari mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria, Rais Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi, alisema mshahara wake na watumishi kutoka sekta zote nchini hautoshi kwa sababu Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa sasa.

“Kuna changamoto ya uhaba wa rasilimali fedha, sio tu kwa mhimili wa mahakama, lakini pia kwa sekta nyingine, mshahara wa watumishi wa sekta zote nchini hautoshi, hata mimi wa kwangu hautoshi,” alisema Rais Magufuli.  

BAJETI YA KWANZA

Bajeti ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli 2016/17 ya Sh trilioni 29.5, mwongozo wake ulijikita kwenye kukuza uchumi wa viwanda, ambayo ilikuwa imeongezeka kwa asilimia 23 kutoka Sh trilioni 22.5 mwaka 2015/16.

Katika majeti hiyo ya mwaka 2016/17, shughuli za maendeleo zilitengewa asilimia 40 tofauti na 2014/15 na 2015/16 ambapo fedha za maendeleo zilikuwa asilimia 32 kwa 2014/15 na asilimia 26 kwa 2015/16.

Katika kipindi hicho cha 2016/17, Serikali ilitarajia kuboresha ukusanyaji mapato ambapo kati ya Sh trilioni 29.5 ilikusudia kukusanya Sh trilioni 18.5 kutoka vyanzo vya ndani.

BAJETI YA PILI

Bajeti ya pili ya Rais Magufuli ya mwaka 2017/18 ya Sh trilioni 31.69, miradi mingi ya kipaumbele iliyopangwa kutekelezwa ilikuwa ni ya ujenzi.

Wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti 2017/18, Dk. Mpango alisema Serikali ilitarajia kukusanya Sh trilioni 31.69, kati yake mapato ya ndani yakijumuishwa ya halmashauri ni Sh trilioni 19.97 sawa na asilimia 63.

Hata hivyo, bajeti hiyo haikutekelezwa kwa asilimia 100 kutokana na mambo mbalimbali.

Dk. Mpango alisema kulikuwa na mwamko mdogo wa kulipa kodi, matumizi hafifu ya mashine za risiti za kielektroniki (EFDs) na kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje.

Kwa mwaka 2017/18, miradi ya kipaumbele ilikuwa ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma Liganga mkoani Njombe, ujenzi wa reli ya kati na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATC).

Miradi ya kielelezo ilikuwa ni ununuzi na ukarabati wa meli katika maziwa makuu na uanzishwaji wa shamba la miwa na kiwanda cha sukari cha Mkulanzi.

BAJETI YA TATU

Machi 13 mwaka juzi, Dk. Mpango aliwasilisha mapendekezo ya mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19 ambayo ilikuwa Sh trilioni 32.47.

Mapato ya ndani yalijumuisha makusanyo ya halmashauri Sh trilioni 20.89 sawa na asilimia 64 ya bajeti yote ambayo ilikuwa ya utegemezi wa nje kwa asilimia 36.

Kati ya mapato hayo, kodi ilipangwa kuchangia kwa Sh trilioni 18 sawa na asilimia 13.6 ya pato la taifa. Mapato yasiyo ya kodi yalitarajiwa kufika Sh trilioni 2.15 na vyanzo vya halmashauri Sh bilioni 735.6.

Mwaka 2018/19, Serikali ilipanga kutumia Sh trilioni 20.46 sawa na asilimia 63 kwa matumizi ya kawaida yanayojumuisha kulipa sehemu ya deni la taifa, mishahara na matumizi mengineyo.

Matumizi ya maendeleo yalipangwa kuwa Sh trilioni 12 sawa na asilimia 37 kwa matumizi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali. 

BAJETI YA NNE

Bajeti ya nne ya mwaka wa fedha 2019/20 Serikali ilitarajia kukusanya na kutumia Sh trilioni 33.1 ambapo mapato ya ndani yakijumuishwa na yanayotokana na halmashauri nchini yalitarajiwa kuwa Sh trilioni 23.

Dk. Mpango alisema kati ya fedha hizo Sh trilioni 20.8 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, matumizi anbayo ni pamoja na gharama za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Alisema kati ya fedha hizo za matumizi ya kawaida, mishahara itakuwa Sh trilioni 7.5 huku matumizi mengineyo (OC) yakiwa ni Sh trilioni 3.57.

Dk. Mpango alisema matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 12.24 ambapo Sh trilioni 9.73 ni fedha za ndani na Sh trilioni 2.51 fedha za nje.

BAJETI YA TANO

Machi 11 mwaka huu, Dk. Mpango aliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21, ambayo inatarajia kukusanya na kutumia Sh trilioni 34.88, ambazo kwa kiasi kikubwa zitajikita kwenye miradi ya ujenzi na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Dk. Mpango alisema kwa kuzingatia sera za bajeti kwa mwaka 2020/21, bajeti hiyo ambayo ni ya tano katika utawala wa Rais Magufuli, Sh trilioni 34.88 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika.

 “Mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya mwaka 2020/21 yamezingatia mahitaji halisi ya ugharamiaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ulipaji wa mishahara na deni la Serikali pamoja na utekelezaji wa vipaumbele vingine vya taifa.

 “Mapendekezo ya kiwango na ukomo yanajumuisha mapato ya ndani ya Sh trilioni 24.07 sawa na asilimia 69 ya bajeti yote, mikopo ya ndani Sh trilioni 4.90, mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara Sh trilioni 3.04 na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo Sh trilioni 2.87 sawa na asilimia 8.2 ya bajeti yote,” alisema Dk. Mpango.

Alisema katika bajeti hiyo, Sh trilioni 21.98 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida na Sh trilioni 12.90 za matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote.

“Bajeti ya maendeleo inajumuisha Sh trilioni 10.16 fedha za ndani, sawa na asilimia 78.8 na Sh trilioni 2.74 fedha za nje. Matumizi haya yanajumuisha gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020,” alisema Dk. Mpango.

Alisema katika mwaka 2020/21, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kuweza kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati. 

Dk. Mpango alisema katika kufanikisha azma hiyo, sera za mapato kwa mwaka 2020/21 zitajielekeza kwenye kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara na uwekezaji kwa kutekeleza mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi.

Alisema zitajikita pia kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiyari pamoja na upanuzi wa wigo wa kodi, kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato.

Dk. Mpango alisema pia zitajikita kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama, kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji.

Alisema zitajikita pia kuendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania (DCF) na kuendelea kukopa kutoka katika vyanzo vyenye masharti nafuu na mikopo inayotolewa kwa utaratibu wa udhamini kutoka taasisi za udhamini wa mikopo.

“Katika mwaka 2020/21, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, lengo kuu ni kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na miradi mingine muhimu. 

“Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la uzalishaji wa madeni ya Serikali,” alisema Dk. Mpango.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles