Magufuli atuma salamu za rambirambi ajali Morogoro

0
848

Anna Potinus

Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa watu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ya moto iliyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro, ambapo ameitaka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu ili kuokoa maisha yao.

Rais Magufuli ametuma salamu hizo leo Jumamosi Agosti 10, ambapo amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 62 na majeruhi 70.

“Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za marehemu wote, ninawaombea marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wapone mapema,” amesema.

Aidha ameonesha kusikitishwa na kitendo cha watu wanaokimbilia magari yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa zilizobebwa na magari hayo ambapo ametaka vitendo hivyo vikome.

“Baadhi ya magari haya yanabeba mafuta ambayo ni hatari kama ilivyotokea Morogoro, yapo magari yanayobeba kemikali za sumu, yapo magari yanayobeba milipuko nakadhalika nawaomba sana tuache tabia hii,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here