Magufuli atoa siku 60 kwa mashirika, taasisi zisizotoa gawio bodi zake zijivunje zenyewe

0
682

Mwandishi Wetu, Dodoma

Rais John Magufuli ametoa siku 60 kuanzia leo Novemba 24, kwa mashirika na taasisi za serikali ambazo hazijakabidhi gawio kwa serikali kufanya hivyo la sivyo bodi hizo zaijivunje zenyewe.

Akizungumza katika hafla ya upokewaji wa gawio kutoka kwa taasisi 79, jijini Dodoma leo Jumapili Novemba 24, Rais Magufuli amesema serikali haiwezi kuwavumilia watu wanaochelewesha maendeleo kwa Watanzania.

“Waziri Mpango ninatoa siku 60 kuanzia leo wawe wameshakabidhi kwako gawio wasipokabidhi ndani ya siku hizo bodi hizo zijivunje zenyewe waandike barua, mwenyekiti kama ni wakuteuliwa na mimi maana yake siku hiyo si mwenyekiti tena, watendaji wa bodi hizo wajihesabu hawapo.

“Kuna watu wanalipwa mpaka milioni 15 kwa mwezi sasa, CEO unalipwa milioni 15 kwa mwezi halafu huna gawio, hufai kuwepo, kwa hiyo Waziri Mpango uwaandikie barua wote ambao hawapo na orodha yao ninayo umewachongea hii damu ikakumwagikie wewe siyo mimi,” amesema.

Rais Magufuli amesema kuna watu wamefanya kazi nzuri wakiwamo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao wametoa gawio la Sh bilioni moja huku pia akimtolea mfano Mkuu wa Majeshi,  Jenerali Davis Mwamunyange ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), ametoa gawio, ambapo amehoji wengine wanaokuwa na viburi hivi ni wakina nani.

“Nasema Katibu Mkuu na Wizara yako baada ya siku 60 ambaye hataleta gawio lolote ajihesabu hayupo, siyo kila siku unasema unapata hasara vyakula unavyo, unanunua magari, kila siku hasara, kila mwaka hasara na wewe upo tunakuvumilia tu.

“Serikali hata kama ina asilimia tano lazima ulipe. Nchi nyingine zinajiendesha kwa kutumia magawio zina watu waaminifu kama ninyi 79 hapa. Lakini inabidi tuanze kupitisha hata sheria bungeni ukipewa shirika ukishindwa ufungwe hufai kuwepo hapo kwa sababu umewacheleweshea maendeleo Watanzania,” amesema Rais Magufuli.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here