23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atangaza neema kwa walimu

Ramadhan Hassan -Dodoma

RAIS Dk. John Magufuli amesema Serikali itaendelea kulipa mishahara ya walimu licha ya janga la ugonjwa wa corona  huku akimwaga ajira mpya 13526 katika kada hiyo.

Kauli hiyo aliitoa jana Jijini hapa wakati akizungumza  katika Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambapo Rais Magufuli alisema kada ya ualimu ni muhimu hivyo Serikali ya awamu ya tano itaendelea kutoa kipaumbele katika sekta hiyo.

“Mmoja wa wanafalsafa mashuhuri duniani Aristotle  aliwahi kutamka maneno yafuatayo na naomba kumnukuu alitamka; ‘watu wanaotoa elimu au maarifa kwa watoto wanapaswa kuheshimiwa zaidi kuliko wazazi kwavile wazazi kazi yao ni keleta watoto duniani wakati wao wanatoa maarifa wanawapatia mbinu za kuishi duniani.

“Waheshimiwa walimu kutokana na hatua ambazo tumechukua mafanikio mengi yametokea, uandikishaji wanafunzi umeongezeka mara dufu kwa wastani wanafunzi milioni moja kwa mwaka 2015 hadi kufikia milioni 1.6 kwa mwaka huu,”alisema.

MISHAHARA LICHA YA CORONA

Rais alisema licha ya changamoto ya ugonjwa wa corona, Serikali itaendelea kuwalipa mishahara hata kama ugonjwa huo utaendelea kuwepo kwa muda mrefu.

“Nitumie fursa hii kuwashukuru walimu wote nchini kwa kuwezesha kupatikana kwa mafanikio haya ninawashukuru sana. Ndio maana tumeendelea kuwalipa mishahara yenu katika kipindi hichi licha ya shule kuwa zimefungwa.

“Tukumbuke katika wafanyakazi wote tunaowalipa walimu ni zaidi ya 266,905 na katika mishahara ambayo tunalipa tunalipa karibia bilioni 600 kwa hiyo nusu ya mishahara bilioni 300 zinaenda kwa walimu.

“Kwa hiyo unaweza ukajiuliza kila mwezi unatoa bilioni 300 kwa wafanyakazi ambao ni walimu ambao hawaendi kufundisha.Hii ni thamani kubwa kwa imani ya Serikali ya awamu ya tano kutambua  kazi kubwa inayofanywa na walimu.

Napenda kuwahakikishia walimu wote nitaendelea kuwalipa mishahara kwa sababu Corona haijaletwa na walimu,”alisema Rais Magufuli.

Alisema sekta hiyo ni muhimu na ndio ambayo imekuwa ikizalisha wataalamu katika sekta zingine hivyo Serikali yake itaendelea kuipa kipaumbele.

“Sekta ya elimu ni zaidi ya  sekta  zote na nyie walimu ndio wazalishaji wa sekta hizo hivyo hatuna budi kutambua umuhimu wa sekta hii.

Natambua kwamba changamoto bado zipo niwahakikishie walimu serikali inazifahamu na inaendelea kuzishughulikia,”alisema.

Rais aliwahakikishia walimu nchini kwamba Serikali haiwezi kuwatupa kwani anazifahamu shida zote za walimu kwani na yeye amewahi kuwa mwalimu.

“Sisi sote ni kitu kimoja na nataka niwahakikishie siwezi kuwatupa walimu wa Tanzania tunajenga nyumba moja ninafahamu shida za walimu kwa sababu hata mimi nimeishi, kuwakana walimu ni kujikana nafsi yangu jambo ambalo siwezi nikafanya ndugu zangu walimu.Kamwe hatupaswi kufanya kazi kwa uadui.”alisema Rais Magufuli.

AUMWAGIA SIFA UONGOZI ULIOPITA

Aidha,Rais alisema uongozi uliopita wa CWT umefanya kazi nzuri kwa kutetea maslahi ya walimu pamoja na kuwa kiunganishi kati ya Serikali na walimu.

“Ninafahamu mkutano huu ni kuwapata viongozi wapya na sipendi kuonekana napiga chapuo ila ukweli lazima useme uongozi huu ambao unamaliza muda wake umejenga uhusiano mzuri sana na Serikali inayoiongoza na hili nasema kwa dhati sana.

“Uongozi huu ambao umemaliza muda wake umejenga uhusiano mzuri na Serikali kwa kutatua changamoto na walikuwa wepesi kutafuta viongozi wa serikali kwa lengo la kujadiliana nao

“Na ndio maana hamkusikia misuguano yoyote nakumbuka wakati tunafunga shule na vyuo kwa sababu  ya ugonjwa wa corona siku ya kwanza, kesho yake nikapigiwa simu ikawa inapiga mara nyingi na baadae ikapokelewa na wasaidizi wangu.

“Wakaniambia  Rais wa Chama cha Walimu anataka kuongea na wewe, nikamsikiliza alichozungumza Mheshimiwa Rais kwa sababu sasa umefunga shule na vyuo inawezekana ukafunga kwa muda mrefu usifanye kama wanavyofanya nchi nyingine ukakata mishahara ya walimu.

“Nikajiuliza nikakumbuka wakati wangu nikiwa mwalimu na bahati nzuri mmoja wa walimu aliyenifundisha Saikolojia mwalimu Luimbiza yupo hapa alinifundisha Mkwawa ila bado kijana tu hizi ndio faida za kuwa mwalimu.

“Baada ya kuniomba hivyo nilitafakari na ndio maana baadae nikazungumza hata ingekaa mwaka mzima au miaka kumi sitafuta mishahara ya kuwalipa walimu hili, lisichukuliwe kama kampeni nimezungumza yale ya ukweli na msema kweli ni mpenzi wa Mungu kwahiyo msije mkampa kura eti kwa sababu aliwasemea,”alisema.

UBORESHAJI SEKTA YA ELIMU

Aidha, Rais Magufuli alisema wakati wa kampeni zake za mwaka 2015 na wakati akifungua Bunge aliahidi kuboresha sekta ya elimu kuanzia ngazi ya awali hadi Chuo Kikuu.

Alisema katika hilo anafarijika kuona kipindi cha miaka mitano amefanikiwa  kutimiza ahadi hiyo.

“Namshukuru Katibu Mkuu (Deus Seif) ametaja mambo ambayo tumeyafanya ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi  hadi  sekondari sio kwamba wanasoma  bila malipo kinachofanyika ni serikali kubepa jukumu hilo kutoka kwa wazazi,”alisema.

Alisema tangu  Desemba 2015 hadi Februari 2020 Serikali imetumia   zaidi ya shilingi trilioni 1.01 kugharamia elimu bila malipo.

Pia, alisema wamefanikiwa kuongeza   idadi ya shule za msingi kutoka shule 16899 mwaka 2015 hadi kufikia shule  17804 mwaka huu na shule za sekondari zimeongezeka kutoka  4708 mwaka 2015 hadi kufikia shule 5330 mwaka 2020.

“Pia tumekarabati shule kongwe za sekondari 73 kati ya 89, tumejenga mabweni 253 na nyumba za maabara 227, tumetoa vifaa kwenye maabara 2566 tumepunguza kiasi kikubwa tatizo la madawati ambapo idadi yake imeongezeka kutoka zaidi ya madawati milioni tatu mwaka 2015 hadi kufikia madawati zaidi ya milioni nane sawa ongezeko la zaidi ya asilimia 200,”alisema.

Kwa upande wa Vyuo vya Ualimu, Rais Magufuli alisema wamekarabati    18 na kujenga vipya viwili katika maeneo Mutunguru na Kabanga.

“Kali kadhalika tumepeleka Computer 1550 kwenye vyuo vyote 35 kwa lengo la kufundisha masomo ya Tehama.

“Tumeongeza Vyuo vya Ufundi (Veta) kutoka 672 mwaka 2015 hadi kufikia 712 mwaka  2020 tumekarabati pamoja na  vifaa na miundombinu ya kufundishia katika vyuo  54 vya Maendeleo ya Jamii na pia  tumejenga hosteli, kumbi za chakula kwenye Vyuo Vikuu,”alisema.

Pia, alisema  wameongeza    bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka  shilingi bilioni 341 mwaka 2014-2015 hadi kufikia shilingi bilioni 450 mwaka 2019 -2020

KUPANDISHA VYEO

Vilevile, alisema Serikali tayari imewapandisha vyeo watumishi 306917 ambapo walimu ni 106367 na mwaka huu inatarajia  kuwapandisha vyeo watumishi 290625 wakiwemo walimu  166548.

“ Ninaimani kuwa miongoni mwao walimu wenye sifa waliotarajiwa na wale waliopandishwa vyeo mwaka 2013-2014.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles