26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atangaza mshahara wake

john-magufuliNA MWANDISHI WETU

RAIS John Magufuli ametangaza mshahara wake, akisema analipwa Sh milioni 9.5, huku akiahidi kuutolea ufafanuzi zaidi pindi atakapomaliza mapumziko.

Kauli hiyo aliitoa jana, kupitia ujumbe wake mfupi wa maneno aliotuma katika kipindi cha Clouds 360, kinachorushwa na Televisheni ya Clouds, ambacho pamoja na mambo mengine, kinachambua habari zilizoandikwa katika magazeti.

Rais Magufuli alilazimika kuchukua uamuzi huo akijibu hoja zilizotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na yule wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kupitia gazeti moja la kila siku wakimtaka kuweka wazi mshahara wake, hasa baada ya yeye mwenyewe kuonyesha dhamira ya kupunguza mishahara ya baadhi ya watumishi wa umma aliosema wanalipwa Sh milioni 40.

Habari hiyo ambayo ilizua mjadala wa dakika kadhaa huku watazamaji wakichangia kwa kutuma ujumbe mfupi wa kusisitiza kutaka kujua mshahara wa Rais Magufuli, ndipo kiongozi huyo alilazimika kutuma ujumbe huo mfupi na kutaja mshahara wake.

“Tumepata ujumbe kutoka kwa Rais Magufuli mwenyewe, siyo msaidizi wake wala mtu wa karibu, anasema mshahara ambao ameukuta na analipwa mpaka sasa ni shilingi milioni 9.5,” mmoja wa watangazaji wa kituo hicho, Baby Kabae alilithibitishia gazeti hili.

Kwa mujibu wa mtangazaji huyo, ujumbe huo pia ulieleza Rais Magufuli atakuwa tayari kuonyesha nyaraka za malipo ya mshahara (salary slip) kwa wananchi akitoka kijijini kwake Chato, mkoani Geita, alikokwenda kwa ajili ya mapumziko ya likizo.

Akizungumza mkoani Geita Machi 29 mwaka huu, Rais Magufuli alisema wataalamu wake wanafanyia kazi suala la kukata mishahara ya watu hao wanaoishi kama malaika kutoka Sh mil 40 kwa mwezi hadi kufikia Sh milioni 15.

Machi 6 mwaka huu, katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumapili, Zitto kwa mara ya kwanza alimtaka Rais Magufuli awe mfano kwa watumishi wa umma kwa kuweka wazi mshahara wake na kuulipia kodi kama wanavyolipa wafanyakazi wengine.

Pamoja na hayo, mwaka 2013 Zitto aliweka hadharani mshahara wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa mwaka, akisema ni mkubwa kulingana na uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa Zitto, Rais Kikwete wakati huo alikuwa akilipwa Sh milioni 32 kwa mwezi, huku Waziri Mkuu wake akilipwa Sh milioni 26 kwa mwezi ambazo hazikatwi kodi.

Mbali na Zitto, ripoti ya African Review ya mwaka 2015 ilimtaja Rais Kikwete kuwa miongoni mwa marais watano wa Afrika wanaolipwa mishahara mikubwa.

Marais hao ni pamoja na Paul Biya wa Cameroun aliyekuwa akilipwa Dola 610,000  (Sh bil 1.3) kwa mwaka, akifuatiwa na Mfalme wa Morocco, Mohamed VI aliyekuwa akilipwa Dola 480,000  (Sh bil 1.05) kwa mwaka, huku Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akishika nafasi ya tatu kwa kulipwa Dola 272,000  (Sh milioni 593 ) kwa mwaka.

Rais Kikwete alishika nafasi ya nne kwa kulipwa kitita cha Dola 192,000 (Sh milioni 419)  kwa mwaka, akifuatiwa na Rais wa Algeria, Abdel Aziz Bouteflika, aliyekuwa akilipwa Dola 168,000 (Sh milioni 366)  kwa mwaka.

Hata hivyo, taarifa hizo zilikanushwa na Ikulu ya Dar es Salaam, ambayo hata hivyo, haikuweka wazi mshahara wa Rais mstaafu Kikwete.

Katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumapili, Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, alimtaka Rais Magufuli kuwa mfano kwa kuweka wazi mshahara wake na aulipie kodi kama anavyohamasisha wengine kulipa kodi.

“Siyo sahihi mshahara wa Rais kuwa siri. Unapaswa kuwa wazi kwa wananchi na unapaswa kulipiwa kodi. Hivi sasa Rais halipi kodi ya mapato, lakini anahamasisha watu walipe kodi,” alisema Zitto na kuongeza:

“Rais Magufuli aonyeshe njia kama raia namba moja kwa kutangaza mshahara wake na pili kulipa kodi ya mshahara huo kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine.”

Akithibitisha kutokulipiwa kodi kwa mshahara wa Rais, Zitto alinukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 43(1) na (2) inayosema:

“(1) Rais atalipwa mshahara na malipo mengineyo na atakapostaafu atapokea malipo ya uzeeni, kiinua mgongo au posho, kadiri itakavyoamuliwa na Bunge na mshahara na malipo hayo mengineyo ya uzeeni na kiinua mgongo  hicho, vyote vitatokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.”

“(2) Mshahara na malipo mengine yote ya Rais havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Masharti ya Katiba hii,” alisema Zitto.

Kuhusu maadili ya viongozi wa umma, Zitto amemtaka Rais kuonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi kwa kuweka mali zake na madeni yake wazi.

“Rais aagize kila waziri kuweka wazi taarifa zao za mali na madeni walizotoa kwa Tume ya Maadili na aagize (presidential decree) kwa Tume ya Maadili iweke mali na madeni ya viongozi kwenye tovuti ya Tume, wananchi waweze kuona na kujua kama wamesema uongo au la,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles