RAIS Dk. John Magufuli, ameombwa kutoa nafasi kubwa zaidi ya mazungumzo kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, ili kujali na kuthamini uamuzi wa wananchi walioufanya wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Ombi hilo lilitolewa juzi na Mbunge wa Viti Maalumu Wilaya ya Magharibi A Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Raisa Mussa wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Mgogoro huo umekuja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo kwa madai kulikuwa na dosari nyingi.
Raisa alisema hakuna sababu ya kuipeleka Zanzibar kwenye machafuko na kumtaka Rais Magufuli achukue hatua haraka.
“Zanzibar itakapoingia katika machafuko, atakayelaumiwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenyewe ndiyo iliyobeba dhamana kubwa ya kupatikana suluhu ya tatizo hili,” alisema.
Alisema anashangazwa na Tanzania kuwa mstari wa mbele kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya kisiasa katika nchi nyingine, ikiwamo Burundi wakati Zanzibar bado kunafukuta.