MWANDISHI WETU-RUBONDO
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, huenda akauanza mwaka mpya vibaya baada ya Rais Dk. John Magufuli kutaka amalize tofauti zake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda vinginevyo atatengua uteuzi wao.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na maofisa na askari wanyamapori wa Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, ambako ametembelea na kujionea vivutio vya utalii.
Rais Magufuli alieleza kusikitishwa kwake na uhusiano mbaya uliopo kati ya Waziri Dk. Kigwangalla na Katibu Mkuu wake Profesa Mkenda hali ambayo inasababisha baadhi ya shughuli za wizara kusuasua.
“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, Katibu Mkuu na Waziri kila siku wanagombana na ninawatazama taratibu, nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite awaeleze, lakini wasipobadilika nitawaondoa, hili ni lazima nilizungumze kwa dhati.
“Siwezi kuwa na watendaji wa kuteua mimi halafu kila siku wanagombana, kuna mambo mengi hayaendi, Katibu Mkuu hamheshimu Waziri na Waziri nae hataki kwenda na Katibu Mkuu, siwezi kuvumilia hilo.
“Kwa hiyo nalizungumza hili siku ya leo (jana) tarehe 31 ya mwezi wa 12 (2019) kwamba wajirekebishe na ikiwezekana wajirekebishe ndani ya siku tano, wawe wanasalimiana, wanazungumza, mimi ninafahamu nina vyombo ninajua nani hafai zaidi,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kazi nzuri ya uhifadhi, kukuza utalii na kuchangia mapato ya Serikali.
Pia Rais Magufuli alitangaza kuingozea muda Bodi ya Tanapa iliyomaliza muda wake chini ya Mwenyekiti Jenerali mstaafu George Waitara, kutokana na kuridhishwa na kazi nzuri zilizofanywa na Tanapa chini ya uongozi wa bodi hiyo ikiwamo kuunda Jeshi Usu la Askari Wanyamapori na Hifadhi ya Misitu huku akilitaka shirika hilo liendelee kupiga hatua kwa masilahi ya taifa.
Alisema Tanzania yenye hifadhi za taifa 22 imetoa zaidi ya asilimia 32.5 ya eneo la ardhi yake kwa hifadhi na kwamba imefanya hivyo kwa masilahi ya Watanzania na watu wote duniani wanaotembelea hifadhi hizo.
Alimpongeza Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, Dk. Allan Kijazi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Fredrick Mofulu kwa kazi nzuri ya kudhibiti ujangili katika hifadhi hiyo na kutunza mazalia ya samaki pamoja na ndege ambao husafiri kutoka nchi mbalimbali duniani na kutunza uoto na wanyama waliomo katika hifadhi hiyo.
Rais Magufuli aliahidi kuwa Serikali itatoa Sh bilioni mbili kununua kivuko chenye uwezo wa kuchukua watu 100 na magari manne ili kurahisisha usafirishaji wa watalii wanaoingia na kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo wakiwa na magari yao.
Alisema kwa sasa Tanzania ina bustani za wanyamapori (zoo) 23, mashamba ya wanyama 20 na ranchi sita.
Alitoa wito kwa Watanzania wakiwamo wastaafu katika tasnia ya wanyamapori kujitokeza kuanzisha bustani za wanyamapori, mashamba ya wanyama na ranchi ambazo zitasaidia kuvutia watalii na kuongeza kipato.
Awali akimkaribisha Rais Magufuli, Kamishna Dk. Kijazi alimshukuru kwa juhudi zake za kutilia mkazo shughuli za uhifadhi na kupanua maeneo ya uhifadhi kutoka hifadhi 16 mwaka 2015/16 hadi kufikia 22 hivi sasa.
Dk. Kijazi aliahidi kuwa Tanapa itahakikisha hifadhi hizo zinatunzwa kwa manufaa ya taifa.
Naye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Kamishna Msaidizi Mofulu alisema hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 456.6 inao wanyama mbalimbali wakiwamo sokwe, pongwe, swala, tembo, twiga na pia ni mazalia ya samaki wa Ziwa Victoria na ndege mbalimbali.
Alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2014/15 hadi 2018/19 idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imeongezeka hadi kufikia 5,700 kwa mwaka, walioingiza Sh bilioni 1.4 katika pato la taifa.
Magufuli amekuwa rais wa kwanza kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo akiwa madarakani.
HIFADHI YA TAIFA RUBONDO
Hifadhi ya Taifa Rubondo ni kisiwa kilichopo pembezoni mwa Ziwa Victoria, ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani, likiwa linaziunganisha nchi tatu; Tanzania, Kenya na Uganda.
Kisiwa hiki kinaundwa na mkusanyiko wa visiwa tisa vidogo vidogo.
Rubondo ni makazi na mazingira mwafaka ya kuzaliana samaki wakiwamo sato na sangara ambao huweza kuwa wakubwa na kufikia uzito wa hadi kilo 100.
Hifadhi hii ina ukubwa wa kilomita za mraba 457 na iko kaskazini magharibi mwa Tanzania na inafikika kwa ndege za kukodi kutoka, Arusha, Ziwa Manyara, Serengeti na Mwanza; kwa njia ya barabara kutoka Mwanza – Sengerema – Geita – Nkome kisha kwa boti hadi hifadhini; kwa meli ndogo kutoka Muleba na Bukoba; vile vile kwa njia ya barabara kutoka Wilaya ya Biharamulo na Muleba kupitia Kijiji cha Mganza.
Hifadhi hii ni maskani makuu ya ndege wala samaki kama zumbuli (Kingfisher), chechele (Flycatcher) na tai samaki (Fish eagle).
Mbali na ndege hao, kisiwa hiki ni makazi ya aina nyingine nyingi ya ndege wa majini na mimea ambayo hutoa harufu nzuri ya kuvutia.
Wanyama wakazi wa hifadhi hii kama viboko, pongo, nzohe, fisi maji, mamba na pimbi wanashirikiana makazi na wanyama waliohamishiwa katika hifadhi hii kama sokwe, tembo, mbega weusi na weupe na twiga.
Shughuli za utalii katika hifadhi hii ni pamoja na safari za miguu msituni, safari za boti na uvuvi wa kutumia ndoano.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni wa kiangazi, Juni – Agosti.
Aidha, wakati wa masika, Novemba hadi Machi (kuona maua na vipepeo) na vilevile Desemba – Februari (kuwaona ndege wahamiaji).