27.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

MAGUFULI ASEMA CCM ITATAWALA MILELE

*Adai haina mbadala wanahaingaka watapata tabu sana

Na WAANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema chama hicho kitaendelea kutawala milele kwasababu hakuna mbadala wake na wanaohangaika ‘watapata tabu sana’.

Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi la Chuo cha Uongozi cha Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani jana, Rais Magufuli alisema CCM ipo na itatawala milele na kwa yeyote anayefikiri tofauti ‘atapata tabu sana’.

“CCM ni chama tawala na kitaendelea kutawala milele na milele. Kwa wanaohangaika watapata tabu sana siku zote, siku hakuna mbadala ni CCM hadi milele.

“Wanachama wa CCM tembeeni kifua mbele tumeamua kuleta Tanzania mpya inayowapigania wananchi  hasa wanyonge ili waweze kushiriki katika maendeleo,”  alisema Dk. Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alizitaka nchi sita zinazoshiriki kwenye ujenzi na usimamizi wa chuo hicho kuwa mfano katika kuwajenga viongozi wapya watakaoinua upya uzalendo barani Afrika.

Alisema chuo hicho kinachojengwa kwa ushirikiano baina ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na vyama sita vilivyoshiriki harakati ya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika kitakuwa na jukumu la kuwanoa vijana katika masuala ya itikadi na uongozi.

“Katika zama hizi, tunahitaji chuo hiki kitusaidie kuzalisha akina Julius Nyerere, Samora Machel, Agustino Neto, Sam Nujoma, Robert Kaunda na akina Robert Mugabe wengi.

“Chuo hiki kitakuwa kichocheo cha kujenga ushirika mpya wa kupigania maendeleo yetu ya kiuchumi. Suala hili linawezekana hasa ikizingatiwa vyama vyote washirika vina misingi ya kiitikadi inayofanana,” alisema.

Alieleza kuwa hana wasiwasi kwa kuwa kuanzishwa kwa chuo hiki kinachojumuisha vyama vilivyoshiriki harakati itakuwa ni kichocheo cha kushirikiana katika maendeleo ya kiuchumi na kisiasa.

Chuo hicho kinajengwa kwa ushirikiano wa vyama vya African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini, FRELIMO cha Msumbiji, MPLA cha Angola, ZANU-PF cha Zimbabwe na SWAPO cha Namibia.

Vyama hivyo vilipata msaada mkubwa kutoka Tanzania chini ya iliyokuwa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika, iliyoongozwa na marehemu Hashim Mbita.

“CCM chini ya Hayati Mwalimu Nyerere ndiyo iliyosimamia kuwahifadhi viongozi wa vyama hivyo na kuwapa mafunzo ya kiitikadi na kijeshi, hatimaye walifanikiwa kuzikomboa nchi zao kutoka kwa wakoloni,” alisema.

Alishauri pamoja na lengo lake kuu la kufundisha itikadi na uongozi mara kitakapokamilika miaka miwili ijayo, ni vyema chuo hicho kikaangalia namna ya kuongeza kozi nyingine zaidi za masuala ya maendeleo, ili kuhakikisha nchi zote zitakazonufaika zinafikia maendeleo ya kweli.

Ushiriki wa China

Akizungumzia ushiriki wa China katika ujenzi wa chuo hicho, Rais Magufuli alisema nchi hiyo chini ya chama rafiki cha Kikomunisti cha China (CPC) itatoa mchango wake katika kufundisha wakufunzi na wahadhiri.

Alisema anatoa shukrani kwa chama cha CPC ambao walikubali kujenga chuo hicho kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 45, ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 100 za Tanzania.

Alisema Tanzania ni wanufaika wa misaada ya China ikiwamo Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na mingine, akieleza kuwa huu pia ni msaada mkubwa wenye heshima kubwa na kuahidi kuendelea kuuenzi urafiki.

Majukumu 

Alisema kwa sasa chuo hicho kitakapoanza kitatoa mafunzo ya muda mfupi kuazia kozi za miezi mitatu, muda wa kati na kozi za muda mrefu za miaka mitatu.

Kwa habari kamili jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA hapo juu 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,327FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles