NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
RAIS wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, ametangaza Baraza la Mawaziri na kumteua Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo.
Awali kabla ya uteuzi wa jana wa Serikali ya Awamu ya Tano, wizara hiyo ilikuwa chini ya mbunge wa kuteuliwa Dk. Fenella Mukangara na Naibu Waziri wake Juma Nkamia ambaye ni Mbunge wa Chemba.
Akitangaza baraza hilo jana jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kutakuwa na jumla ya mawaziri 19 ndani ya wizara 18 ambapo baadhi hazitakuwa na Manaibu Waziri lengo likiwa ni kuwa na baraza dogo ili kupunguza gharama.
Nape ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kabla ya kuteuliwa kuwa waziri aliwahi kufanya mahojiano na MTANZANIA na kuwatoa hofu Watanzania wanaopenda michezo akiwataka wawe na imani na Rais wa Awamu ya Tano, akiamini ataweza kuinua michezo nchini tofauti na wanavyofikiria.
“Nawapa mfano, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, hakuwahi kuwa mwanamichezo wala kuwahi kukanyaga uwanjani, ila ametuachia alama ya uwanja,” alisema.
Nape pia katika mazungumzo hayo na gazeti hili, hakusita kuzungumzia matokeo mabovu ya soka hivi karibuni ambapo alisema hayo yamesababishwa na kutowekeza katika soka badala yake tunatengeneza timu kiujanja ujanja.
“Tukitaka matokeo makubwa inatubidi tufanye uwekezaji ili tufanye vizuri, tusifanye vitu kirahisi Serikali lazima iwekeze lakini badala ya kuwekeza tunaanzisha vitu kirahisi Azam B, Yanga B na Simba B, ndio maana tunakutana na wachezaji wenye umri mkubwa lazima tukubali kuwekeza,” alisema Nape.
Alieleza kuwa kuna wakati yalifanyika makosa makubwa ambapo Waziri wa Elimu, Joseph Mungai, alifuta michezo shuleni jambo ambalo lilichangia kuua michezo kabisa lakini sasa michezo inatakiwa kurudi.
Alisema ili kufikia mafanikio, zitungwe sheria zitakazowabana watu, sheria zitakazoongeza maslahi ya wachezaji.
Nape pia alitaka zitungwe sheria za michezo ambazo zitasaidia kuwabana wanamichezo ambao wanatumia vilevi kama pombe na dawa za kulevya.
Hatua ya kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Michezo kunaweza kusaidia kupunguza machungu ya Watanzania waliokata tamaa kutokana na kufanya vibaya katika michuano mbalimbali ya kimataifa na kutekeleza hayo aliyoyaongea wakati wa mahojiano alipotembelea ofisi za New Habari (2006) Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Rai, The African, Bingwa na Dimba.