31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli amaliza ngwe ya kwanza

NORA DAMIAN – GEITA

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amemaliza siku 12 za kwanza za kampeni, akiwa tayari amewafikia wapiga kura kwenye zaidi ya majimbo 20 ambapo ameelea mafanikio ya Serikali yake na kuwaomba Watanzania wamchague kwa mara ya pili.

Mikutano ya Rais Magufuli katika maeneo aliyopita kwenye awamu hii ya kwanza ya uzinduzi wa kampeni, Rais Magufuli ameendelea kunadi sera za chama chake kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 ambayo ameitumia kueleza mambo makubwa aliyotekeleza na atakayoyafanya kwa awamu nyingine.

Rais Magufuli alianza kunadi sera zake Agosti 29 wakati CCM kilipozindua kampeni katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kisha kuendelea katika mikoa mbalimbali kama vile Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza na kualizia safari yake ya kwanza mkoani Geita juzi, Septemba 9, 2020.

Hadi sasa Rais Magufuli ameshafanya mikutano katika majimbo ya Dodoma Mjini, Bahi, Ikungi, Manyoni, Singida, Iramba, Igunga, Nzega, Kishapu, Shinyanga Mjini, Maswa, Bariadi, Busega na Bunda.

Mengine ni Butiama, Musoma Mjini, Ilemela, Nyamagana, Sengerema, Buchosa, Geita Mjini na Busanda.

Kwa siku Rais Magufuli amekuwa akifanya hadi mikutano 10 ikiwemo ile ya njiani pindi anapotoka mkoa mmoja kwenda mwingine pamoja na mikutano mikubwa inayokuwa imeandaliwa katika mkoa husika.

Mfano alipokuwa akitoka Mkoa wa Mara kwenda Mkoa wa Mwanza alifanya mikutano katika maeneo 10 tofauti.

Siku hiyo Rais Magufuli alisimama na kuzungumza na wananchi wa maeneo ya Nyamikoma, Mtangakuona na Nyashimo yaliyopo Jimbo la Busega mkoani Simiyu pamoja na maeneo ya Kihangara, Magu, Nyanguge, Igoma, Nyakato, Buzuluga na Mabatini ya mjimbo ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza.

Rais Magufuli amekuwa akitumia mikutano hiyo kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kueleza atakayoyafanya kwa miaka mitano mingine sambamba na kunadi Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 yenye kaulimbiu ya ‘Tumetekeleza kwa Kishindo Tunasonga Mbele Pamoja’.

Amekuwa akieleza mafanikio yaliyopatikana katika kulinda amani, kukua kwa uchumi, kuimarisha utumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, uchumi wa viwanda, miradi ya kimkakati, usimamizi wa rasilimali kama vile ardhi, madini, gesi asilia, misitu, wanyama, bahari, maziwa na mito.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato, ujenzi wa miundombinu ya kisasa na fursa za ajira, kuimarisha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, sayansi na teknolojia pamoja na kuboreshwa kwa huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, umeme na makazi.

MIRADI YA TRILIONI 37.8

Rais Magufuli alisema mafanikio hayo yamewezesha kuongezeka kwa bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 26 hadi 40 ambapo kwa kipindi cha miaka mitano miradi yenye thamani ya Sh trilioni 37.8 imetekelezwa nchini.

Alisema pia kilomita 3,500 zimejengwa kwa kiwango cha lami pamoja na madaraja 10 yakiwemo ya Salender na Busisi ambayo ujenzi wake unaendelea.

“Hii yote ni kuifanya Tanzania waione kwamba ni nchi kweli imeingia uchumi wa kati, kama tumekuta nchi inahesabika uchumi wa chini leo uchumi wa kati…ndiyo wakati wa kutupa kura ili tufike uchumi wa juu na mbinu za kufika huko tunazo,” alisema Rais Magufuli.

Aidha alisema gawio kutoka katika taasisi ambazo serikali ina hisa limeongezeka kutoka Sh bilioni 161 (2014/15) hadi Sh trilioni 1.528 (2019/20).

MAMBO MAKUBWA YANAYOAHIDIWA

Katika mikutano inayoendelea Rais Magufuli amekuwa akieleza mambo mbalimbali yaliyopangwa kutekelezwa miaka mitano ijayo huku akisisitiza kwamba ilani ya mwaka huu imesheni mambo mengi mazuri na kwamba ni kubwa kuliko zilizopita.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli ilani ya mwaka huu yenye kurasa 303 inalenga kuleta ustawi wa Watanzania wote kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili ili kuhakikisha kuwa matarajio yao katika nyanja zote yanafikiwa kwa manufaa na ustawi wa taifa.

“Mlinipa dhamana ya kuliongoza taifa hili, mlinipa jukumu kubwa katika kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Ilani ya uchaguzi ndiyo mkataba mkuu kati ya wale wachaguliwa na wananchi unaowaongoza.

“Kuongoza ni kutoa lengo ndicho tunachokifanya kwa maendeleo mapana ya nchi yetu, mimi bado naamini tuna mambo mengi ya kufanya katika nchi hii na hasa kuibadilisha,” alisema Rais Magufuli.

Ahadi nyingine ni kutengeneza ajira milioni 8 na kuhakikisha uchumi unakua kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka.

Kuonheza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 511,383 hadi kufikia milioni 1.2 sambamba na kuimarisha huduma za ugani na vyama vya ushirika.

Maeneo ya ufugaji yataongezwa kutoka hekta milioni 2.7 hadi kufikia hekta milioni 6 na kwamba wataongeza vituo vya kuzalisha mbegu bora ili kuwa na tija ya mifugo nchini.

Kwa upande wa uvuvi alisema itajengwa bandari ya uvuvi katika ukanda wa Pwani, kuongeza uzalishaji wa vifaranga na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki.

“Kwenye madini tutaimarisha udhibiti na usimamizi wa uchimbaji madini ili uweze kunufaisha taifa, tutawezesha wachimbaji wadogo wafanye shughuli zao kwa tija. Tutaimarisha masoko kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji madini,” alisema Rais Magufuli.

Aidha alisema mapato yatokanayo ya utalii yataongezeka kutoka Dola bilioni 2.6 hadi Dola bilioni 6 huku idadi ya watalii ikitarajiwa kuongezeka na kufikia milioni 5.

Rais Magufuli pia aliahidi kujenga uwanja mkubwa katika Jiji la Dodoma ili kuwawezesha wananchi wote kushuhudia matukio yatakayokuwa yakifanyika badala ya wengine kukaa na kuangalia kwenye luninga.

“Sekta hii inakua kwa kasi na imeajiri vijana wengi, tutaimarisha usimamizi wa hati miliki ili wasanii wanufaike na kazi zao. Sekta ya sanaa na michezo tutaibeba kwa nguvu kubwa zaidi,” alisema Rais Magufuli.

USAFIRI, MAWASILIANO

Rais Magufuli alisema wataendelea kuunganisha barabara katika mikoa ambayo bado haijaunganishwa pamoja na kuimarisha usafiri wa reli, majini na anga.

Alisema watanunua meli ya kubeba mizigo katika Bahari ya Hindi, kujenga meli tatu na kununua meli ya kubeba mabehewa ya treni.

Katika usafiri wa anga alisema wanatarajia kununua ndege mpya tano na kati ya hizo mbili zitakuwa za masafa marefu, mbili za masafa ya kati na moja ya mizigo.

Pia alisema wataimarisha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kiwe na uwezo wa kutoa wataalam mbalimbali wa anga.

Katika sekta ya mawasiliano alisema wataongeza matumizi ya intaneti kutoka asilimia 43 hadi kufikia asilimia 80.

AFYA, MAJI

Rais Magufuli alisema watumishi mbalimbali wa kada ya afya wataongezwa kufikia 25,000 pamoja na kukamilisha ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na rufaa.

Katika sekta ya maji Rais Magufuli alisema watahakikisha asilimia 90 ya Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama.

“Ninajua wako baadhi ya watu wanaweza wasiamini kwamba tunaweza kuyatekeleza, naomba Watanzania watuaminia uwezo wa kuyatekeleza tunao kama ambavyo tumeweza kuyatekeleza yale mengine kwa kipindi cha miaka mitano,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema pia Jiji la Dodoma litaendelea kuboreshwa liwe la kisasa zaidi na kwamba tayari mkataba umeshasainiwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilomita 112 itakayokuwa na njia nne.

Alisema pia utajengwa uwanja wa ndege wa kisasa katika eneo la Msalato.

WILAYA MPYA

Rais Magufuli alisema pia ataendelea kujenga miji ya kisasa na kurathimisha makazi yasiyo rasmi huku akiahidi kuunda wilaya mpya katika mikoa ya Mwanza na Geita.

Alisema ataongeza wilaya moja katika Mkoa wa Mwanza na kuunganisha maeneo ya Katoro na Buselesele yaliyopo mkoani Geita kuwa wilaya.

“Tutatengeneza wilaya ambayo itakuwa ya mfano katika nchi hii, hapa pameshakuwa mji mkubwa hivyo tunataka kuleta mabadiliko ya kweli katika mji wenu,” alisema Rais Magufuli alipozungumza na wakazi wa Katoro juzi.

Rais Magufuli alisema uchaguzi wa Oktoba ni muhimu kwani ndiyo utakaoamua mwelekeo wa taifa kwa miaka mitano mingine na kuwataka Watanzania watafakari kwa ajili ya masilahi mapana ya nchi.

“Uchaguzi huu utaamua ama tuendelee na mageuzi tuliyoyaanzisha ama tusiendelee nayo, tunajua tumejenga msingi mkubwa, tumeanzisha miradi mingi…tuangalie mahali tulipotoka, tulipo na tunapoelekea.

“Nawaomba sana kura zenu mkipigie Chama Cha Mapinduzi ili haya niliyoyaeleza tuweze kuyatekeleza kwa kasi,” alisema Rais Magufuli.

 MATARAJIO YA WANANCHI

Wananchi wa maeneo mbalimbali nchini walipongeza mafanikio yaliyopatikana kipindi cha miaka mitano iliyopita na kumuomba Rais Magufuli aongeze kasi zaidi kumalizia changamoto zilizopo.

Akizungumza na MTANZANIA mkazi wa Katoro mkoani Geita, David Kulola, alisema licha ya kuwapo kwa changamoto ya ukosefu wa ajira lakini Rais Magufuli amewapa ujasiri vijana wa kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.

Kulola ambaye ni mhitimu wa taaluma ya famasia alisema baada ya kuhitimu masomo yake na kutafuta kazi kwa miezi sita bila mafanikio aliamua kujiajiri kwa kufungua duka la dawa.

“Sikufichi dada yangu (Mwandishi) kujiajiri kunalipa, mimi tangu nasoma malengo yangu yalikuwa ni kuja kuajiriwa lakini baada ya kutafuta kazi na kukosa nikaamua kufungua duka langu la dawa.

“Na wala sikuwa na mtaji mkubwa kwa sababu wengine wanadhani mpaka uwe na milioni 2 au 3 ndio unaweza kufanya biashara. Mimi nilianza kununua dawa kidogo kidogo, kama leo nanunua kiboksi kimoja cha dawa ya Malaria baada ya siku tatu au nne naongeza kingine mpaka unaona duka limefikia hapa.

“Kiongozi wetu (Rais Magufuli) ni jasiri na ametujenga wananchi wake ndiyo maana sasa hivi unaona watu wengi wanajishughulisha kufanya kazi kwa bidii,” alisema Kulola. 

Naye Magu Sita (73), mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, ambaye alikuwa mmoja wa wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Somanga alisema; “Mimi naona rais wetu ameongoza nchi vizuri hasa ukichunguza vitu vilivyolala na vikafufuliwa, tunaendelea kumuombea katika uongozi wake. Vitu vingi amefanya, Simiyu tulikuwa tuna hali mbaya ya umeme yaani watu walikuwa wananyanyasika sasa hivi wanatulia. Mkazi mwingine wa mkoa huo, Mandi Kulwa alisema; “Hapa Simiyu ametufanyia mambo mengi mazuri zahanati, shule, maji umeme yaani ametufanyia mambo mengi kweli hatuwezi tukamsahau.

Naye mkazi wa Mabatini jijini Mwanza, Benja Mwamungesha, alisema Rais Magufuli ameiongoza nchi vizuri hasa kwa kujali maisha ya wanyonge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles