*Uongozi wahaha siku za mapumziko
* Sefue leo kufanya ukaguzi, kufuatilia maagizo
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
UAMUZI wa Rais Dk. John Magufuli kumng’oa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Hussein Kidanto, umesababisha wafanyakazi wa hospitali hiyo na viongozi wao kufanya kazi hadi siku za mapumziko.
Hatua hiyo imekuja wiki chache baada ya Dk. Magufuli, kufanya ziara ya kushtukiza hospitalini hapo, Novemba 9 ikiwa ni ziara yake ya pili baada ya ile aliyoifanya Wizara ya Fedha.
Katika ziara hiyo, Dk. Magufuli alichukua hatua kadhaa ikiwamo ya kumhamishia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Hussein Kidanto.
Dk. Kidanto alikaimu nafasi ya Ukurugenzi mapema mwaka huu baada ya aliyekuwa Mkurugenzi, Dk. Marina Njelekela, kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Vilevile alimteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa (MOI), Profesa Lawrence Mseru kuwa kaimu mkurugenzi kuanzia Novemba 10.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu Novemba 9 mwaka huu, ilieleza kuwa Rais Magufuli alikasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi.
Ilisema katika ziara hiyo, Rais alikuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa miezi kadhaa wakati mashine kama hizo zinafanya kazi katika hospitali binafsi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko.
Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alitoa maagizo ya Rais Magufuli ya kuvunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilikwisha kumaliza muda wake.
Taarifa kutoka ndani ya hospitali hiyo jana zilisema tangu Rais Magufuli afanye ziara hospitalini hapo, viongozi wa ngazi za juu wamekuwa wakifanya kazi pamoja na vikao vya mipango ya maendeleo hadi siku za mapumziko katika wiki.
“Ninapozungumza nawe hivi sasa wakubwa wote wapo kazini na hili naliona linafanyika wiki ya pili sasa.
“Jumamosi na Jumapili viongozi wote na Kaimu Mkurugenzi (Profesa Mseru), wanakuwapo kazini wakiendelea na majukumu yao ya kawaida.
“Nafikiri hili linatokana na mkakati wa Rais Magufuli wa kuhakikisha Muhimbili inakuwa kimbilio la kila Mtanzania na si vinginevyo.
“Jana (juzi) vililetwa vitanda hapa kwa agizo la Rais Magufuli na vyote leo (jana), tumekuwa katika kazi ya kuvifunga na kuwalaza wagonjwa waliokuwa wamelala chini,” alisema mtoa habari wetu.
MTANZANIA ilimpomtafuta Meneja Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Eligaesha, alisema suala la viongozi wa juu wa Muhimbili kufanya kazi hata katika siku za mapumziko ni la kawaida kwao.
“Hili la vikao na kuendelea na majukumu kwa viongozi wetu wa hospitali ni suala la kawaida katika kutekeleza majukumu … ila hili la vitanda siwezi kuzungumzia kwa sababu vimetolewa kwa upande wa MOI na si kwetu Muhimbili,” alisema Eligaesha.
Sefue kutua leo
Ratiba iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kuwa katika kuhakikisha maagizo ya Rais Magufuli yanatekelezwa, leo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue atafanya ziara kukagua na kuhakikisha kama vitanda vyote vilivyopelekwa hospitalini hapo vimefungwa na wagonjwa wanavitumia.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msingwa alisema Balozi Sefue atafanya ziara Muhimbili leo saa 4.00 asubuhi.
“Mnaarifiwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue atafanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kesho (leo), Jumatatu kuanzia saa nne asubuhi.