23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli aipongeza Kilimanjaro Queens

0d6a8489Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

RAIS wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ametuma salamu za pongezi kwa wachezaji wa timu ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens), kwa kuandika historia ya kuwa mabingwa wa kwanza wa michuano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Challenge) yaliyofanyika katika Mji wa Jinja, nchini Uganda.

Kilimanjaro Queens imefanikiwa kutwaa ubingwa huo baada ya kuibwaga Kenya (Harambee Starlets) kwa mabao 2-1, katika mchezo wa fainali uliofanyika juzi.

Timu hiyo iliyokuwa imepangwa Kundi B kwenye michuano hiyo pamoja na Rwanda, Ethiopia na Uganda, ilifanikiwa kutinga fainali baada ya kuchomoza na ushindi ya mabao 4-1 dhidi ya wenyeji Uganda katika mchezo wa nusu fainali.

Kilimanjaro Queens ilianza kung’ara kuanzia hatua ya makundi kwa kuifunga Rwanda mabao 3-2 kabla ya kupata sare ya bila kufungana na Ethiopia na kukata tiketi ya kuingia nusu fainali ambapo iliwatoa wenyeji Uganda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Dar es Salaam, Gerson Msigwa, Magufuli alitoa pongezi hizo kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ambapo alisema Kilimanjaro Queens imeandika historia ambayo inalipa heshima Taifa na inaamsha morali kwa wanamichezo kufanya vizuri katika mashindano.

“Mhe. Waziri Nape Nnauye, naomba unifikishie pongezi nyingi kwa wachezaji wa Kilimanjaro Queens, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), walimu, viongozi wa timu pamoja na wadau wote waliochangia kuiandaa timu yetu hiyo ya wanawake, ambayo hatimaye imepata ubingwa katika michuano hii mikubwa.

“Nimefurahishwa sana na ubingwa huu na nawaomba wachezaji wa Kilimanjaro Queens na wanamichezo wengine hapa nchini kuuchukua ushindi huu kama changamoto ya kuongeza juhudi katika michezo yetu ili nchi isiishie kupata ubingwa wa Chalenji, bali pia ipate ushindi katika michezo na michuano mingine mingi ambayo hushiriki,” alisema Rais Magufuli.

Rais pia amewaomba Watanzania wote kuendelea kuwaunga mkono wanamichezo na kuwatia moyo wachezaji kwa kuwa mafanikio yao yanaitangaza nchi na yana mchango mkubwa katika maendeleo.

Timu itawasili mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Fast Jet, mara baada ya kuwasili itaelekea moja kwa moja kwenye Hoteli ya Courtyard ambako wameandaliwa chakula cha mchana.

Kikosi hicho kilipita Bukoba kwa ajili ya kuwafariji waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10 mwaka huu.

“Waliondoka Uganda juzi kwa usafiri wa basi ambapo walitumia muda kama wa saa moja hadi Bukoba, baada ya kuwafariji ndugu zetu pale wanatarajia kuwasili kesho (leo) Dar es Salaam kwa usafiri wa ndege.

“Chakula cha mchana kitajumuisha kikosi cha Kilimanjaro Queens na viongozi mbalimbali wa Serikali na TFF ambapo pamoja na mambo mengine kikosi hicho kitapata fursa ya kuzungumza na viongozi hao,” alisema Lucas.

Katika hatua nyingine Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimeipongeza timu hiyo kwa kunyakua ubingwa huo.

Mwenyekiti wa DRFA, Almas Kasongo, amesema kitendo cha Kilimanjaro Queens kutwaa kikombe hicho kinaonesha ni kwa kiasi gani walivyo tayari kwa ajili ya mapambano na endapo nguvu kubwa itatumika katika maandalizi yao wanaweza kulitangaza zaidi taifa.

Kasongo amelipongeza pia benchi la ufundi kwa uvumilivu mkubwa waliouonesha tangu walipokabidhiwa kikosi hicho, licha ya kuwa muda na matayarisho yao hayakuwa rafiki kiushindani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles