27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI AIPA ANGALIZO SEKTA BINAFSI

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO


RAIS Dk. John Magufuli, ameitaka sekta binafsi katika ukanda wa Afrika Mashariki kujitathimini kama kweli iko kwa ajili ya kuzisaidia Serikali kuwaletea wananchi maendeleo ama iko kwa ajili ya kujitengenezea faida.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana nchini Uganda, wakati akizungumza kwenye mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki unaojadili masuala ya maendeleo ikiwamo miundombinu, uwekezaji na afya.

“Huwezi ukawa na sekta binafsi ambayo yenyewe inaangalia faida tu, bila kujali maisha ya watu wa eneo husika au bila kujali Serikali katika eneo hilo iko katika kipaumbele kipi.

“Sekta binafsi ambayo iko kwa ajili ya kujinufaisha yenyewe na haiangalii jinsi itakavyosaidiana na Serikali katika kupunguza kero za wananchi haina maana” alisema.

Rais Magufuli pia aliwataka wakuu wenzake wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa makini hasa na wawekezaji ambao wako kimaslahi zaidi.

Aliwataka wataalamu na sekretarieti ya jumuiya hiyo kuona jinsi watakavyozisaidia serikali zao kupambana na wawekezaji ambao hawataki haki sawa ya mgawanyo wa rasilimali za nchi baina yao na serikali husika.

“Uwekezaji  ama  ubia wa PPP (ubia wa sekta binafsi na serikali) ni win win situation (pande zote kufaidika), huwezi kuwa na uwekezaji ambao hauzingatii usawa katika mgawanyo.

“Wanakuja wanavuna rasilimali zetu wanatajirika na matokeo yake sisi tunaendelea kuwa maskini, tuhakikishe kwamba rasilimali zetu zinatunufaisha na sisi” alisisitiza.

Alisema kunapokuwa na miradi mikubwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi, Serikali zisisubiri kutafuta wafadhili, waanze wenyewe kwa fedha zao za ndani kwani inawezekana.

Alitolea  mfano wa Tanzania ilivyofanya kwenye miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa ya standard gauge kwa na mradi mkubwa wa umeme katika maporomoko ya stiglers gorge Rufiji Mkoani Pwani.

“Fedha za kulipia miradi hiyo mikubwa ya reli na umeme zipo hata wakandarasi wakitaka nitawalipa leo, hii tujifunze ndugu zangu, kusimama wenyewe bila kutegemea mtu ndio tutajijengea heshima na mwishowe tutaleta maendeleo katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki,” alisema.

Mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi za jumuiya hiyo unalenga kujadili na kutafuta majibu ya changamoto za kimiundombinu uwekezaji na afya katika nchi wananchama na pia kuona ni jinsi gani sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali wanaweza kushirikiana katika kuleta maendeleo.

Mbali na  Rais  Magufuli wengine waliohudhuria mkutano huo ni, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Salva Kiir wa Sudan Kusini na mwenyeji wao Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Rais Paul Kagame wa Rwanda na Pierre Nkurunzinza wa Burundi, hawakuhudhuria mkutano huo na badala yake walituma wawakilishi.

Kabla ya Rais Magufuli kutoa mchango wake, Marais walioshiriki mkutano huo wamepokea taarifa ya mkutano wa majadiliano ya kisekta (Round Table) kuhusu mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya miundombinu na afya.

Awali ilielezwa kuwa katika miaka 10 ijayo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitahitaji Dola za Marekani bilioni 78 kutekeleza miradi ya miundombinu inayopendekezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles