*Atangaza uamuzi mgumu kuhusu mitambo yao
*Aeleza siri ya kumteua Makonda Mkuu wa Mkoa Dar
Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amesema Tanzania haiko tayari tena kukodi mitambo ya umeme kama ilivyokuwa ya Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na kwamba itaendelea kujenga miradi yake ya umeme.
Amesema kutokana na hali hiyo, hivi sasa Tanzania inajipanga kuzalisha umeme wake unaotokana na gesi na katu haiko tayari kuwa na wawekezaji wanaoliumiza Taifa kutokana na kuwa na mikataba mibovu.
Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi II uliopo Manispaa ya Ilala, utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 240 za umeme, ambao utagharimu dola za Marekani milioni 344 sawa na Sh bilioni 740.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alisema Serikali yake haiko tayari kukodi tena miradi ya umeme ya aina yoyote.
“Hatutaki tena umeme wa kukodi, mara IPTL… tuachane na umeme usiokuwa wa uhakika wa kukodisha, tumechoka kufanya biashara na wawekezaji wa ajabu ajabu halafu tunalipia ma-capacity charges, tunalipia bei ya ajabu ajabu na umeme unakuwa juu tunawapa shida Watanzania… hapa nikiwauliza wananchi wa Kinyerezi, kila mtu anahitaji umeme, lakini wengine wanashindwa kuvuta umeme kwa sababu bei iko juu.
“Kila mtu anahitaji apikie gesi, umeme, afunge vifaa vyake vya umeme. Lakini bei ya chini haipatikani, huku tuna kila kitu. Hivyo ninawaomba Tanesco pamoja na Wizara ya Nishati mjipange vizuri, nendeni na ‘spidi’ ya ya Hapa kazi tu. Tukizalisha wenyewe tutafanikiwa sana.
“Tanzania tuna kila kitu, hata uranium inaweza kutumika kuwa vyanzo vya umeme, tuna makaa ya mawe, maji, gesi. Lakini kila siku tunalalamika hatuna umeme, wasomi nao tumewasomesha, lakini sijui wanaendaga kujifunza nini huko,” alisema huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo.
Alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuachana na wataalamu wanaomshauri kuhusu miradi ya kukodi, bali wawe na mawazo ya kujenga miradi mipya.
“Muachane na miradi ya kukodisha mitambo ya umeme. Sitegemei nikisikia kwamba mnaleta mapendekezo kwamba mnataka kuongeza mkataba huu au mnataka kukodi mtambo huu, suala la kukodi life kabisa na likalegee huko huko.
“Muhongo nakumbuka ulileta pendekezo la kuvunja bodi, nikakwambia ivunje tu. Ukateua mwenyekiti, nikakwambia huyo huyo kwa sababu wewe ndiyo umemtaka, lengo ili tuondokane na hao waliokuwa wakikushauri kukodisha waende huko wakakodishane mashamba.
“Tuwe na mawazo ya kujenga miradi yetu, siku zote cha kuazima ni mbaya, ni kama unavyoazima nguo ya rafiki yako halafu mnakutana kwenye harusi anakuona umevaa nguo zake na anaweza kukunyang’anya.
“Hivyo lazima tuachane na mambo ya kukodi kwa sababu tumechoka kuchezewa, hapa nchini tuna miradi ya ovyo kweli kweli, kila siku inazaa matatizo na ninakwambia Muhongo ukipata ushauri kutoka kwa wataalamu wako wakileta mawazo ya mitambo ya kukodi, huyo aishie huko huko,” alisema.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja ikiwa umepita zaidi ya mwaka mmoja tangu mzimu huo wa IPTL kusababisha aliyekuwa Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kumfuta kazi Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kumsimamisha kazi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, huku Sospeter Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Jaji Fredrick Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakijivua nyadhifa zao kutokana na kashfa ya fedha za Escrow.
Mzimu huo wa IPTL kupitia akaunti ya Tegeta Escrow ulizua mjadala ambapo lililokuwa Bunge la 10 lilitoa maazimio manane ikiwamo Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mengine ilikuwa ni kutaka Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa mujibu wa sheria za nchi pamoja na kupitia mikataba ya umeme.
Akaunti ya Escrow ilianzishwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhifadhi fedha, baada ya kuibuka mvutano kati ya Tanesco na IPTL kuhusu ongezeko la mtaji wa uwekezaji, huku Tanesco ikilalamika kuwa gharama za kununua umeme kutoka kampuni hiyo zilikuwa za juu mno. Fedha hizo zingeendelea kutunzwa katika akaunti hayo hadi wakati ambapo suluhisho la mvutano wa wabia hao wawili lingepatikana.
UUZAJI UMEME NJE
Rais Magufuli alisema Tanzania itaendeleza miradi ya aina hiyo kwa kuendelea katika maeneo mengine, huku mpango wa Serikali wa baadaye ni kuhakikisha umeme unauzwa nje.
“Tutakuwa na umeme kwa sababu tutaendeleza miradi kama hii maeneo mengine, na mpango wa Serikali wa baadaye tutaanza kuuza katika nchi jirani, na Kenya tayari imeshaomba, iko tayari kuuziwa.
“Tutaanza kujenga bomba la gesi lenye jumla ya kilomita 14,010 kutoka Tanga hadi Uganda kusafirisha mafuta, na itatengeneza ajira zaidi ya 21,500. Hivyo ninawaomba tuendelee kushikamana na kusapoti Serikali ya awamu ya tano,” alisema.
Rais Magufuli alisema mradi huo utakapokamilika vijana wa maeneo hayo ya Kinyerezi wapewe nafasi za ajira.
Alisema mradi huo unaogharimu dola za Marekani milioni 300, utajengewa Kituo cha Polisi kwa ajili ya usalama.
Awali akimkaribisha Rais, Mkurugenzi wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema mradi huo utakuwa na jumla ya mitambo sita aina ya Hitachi 25 itakayofua kiasi cha megawati 160 zitakazotokana na gesi na mitambo miwili ya mvuke itakayoongeza megawati 80.
BWAWA LA MTERA
Rais Magufuli alieleza kushangazwa kwa kitendo cha Tanesco kueleza kila wakati kukauka kwa bwawa la Mtera ambalo ndilo huzalisha umeme.
“Watani zangu Iringa huwa wanajinyonga, hivi karibuni yametokea mafuriko eti wakakimbia. Sasa nawashangaa Tanesco wakiniambia kuwa Mto Mtera maji yamepungua au umekauka.
“Siamini kama yametokea mafuriko kule Iringa baada ya siku mbili mniambie maji yamekauka, hayo yaliyofurikisha Wahehe kwanini hamkuyazuia, na yalikuwa yanapita mto gani, kwanini hamkuyakinga yaelekee Mtera, nadhani mmenielewa namaanisha nini. Ninasema kwa dhati kutoka moyoni kama ‘message sent’ na imepokelewa,” alisema.
AMSIFU MAKONDA, PROF MUHONGO
Alisema ameamua kumrudisha Profesa Sospeter Muhongo katika wizara hiyo ya nishati huku akimpa Paul Makonda ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na uchapakazi wao pamoja na kwamba wanapigwa vita.
“Siku zote vitu vizuri vinapigwa vita…hivyo nimeamua kumrudisha Profesa Muhongo. Na Makonda nikampa mkoa wa Dar es Salaam ili wabaya wao wawaone ni mabosi zaidi ni kwa sababu anayeamua ni mimi.
“Kwa hiyo nikishasali na kuswali Mungu ananiambia leo ni Makonda Dar na wenye chuki wajinyoge, ndiyo maana nikasema Muhongo hapa hapa kwa sababu sichagui mwanasiasa bali nahitaji mchapakazi kwa vile tunahitaji umeme na ndiyo maana nikachagua watu ambao ni wachapakazi.
“Leo Wizara ya Nishati mmenifurahisha huwa sipongezagi ovyo, lakini leo mmenifurahisha. Ninawaomba muende na ‘speed’ kubwa zaidi,” alisema na kuongeza:
“Wizara hii ina wasomi wazuri, mmeanza vizuri na nimepata taarifa kuwa mnataka kuongeza megawati 185 na kandarasi amesema kuwa mnahitaji dola milioni 20 za Kimarekani kwenye mradi huu wa Kinyerezi… kama tulitoa dola milioni 120 sasa hiyo tutashindwa kweli.
“Ninawaambia kwamba fedha hizo tutazitafuta, hata mwezi huu zitapatikana ili kusudi na yeye aanze kujenga. Tunataka umeme uwepo kila mahali kwa sababu vyanzo vya umeme vipo.”
Alisema Watanzania wamemchagua bure bila kutoa hongo yoyote, hivyo lazima atekeleze ahadi zake, na kwamba atakayejaribu kukwamisha maendeleo atakwama yeye kwa sababu wananchi wamechoka kusubiri.
“Mmetuchagua bure, hatukuwahonga, hivyo lazima tuwafanyie kazi na tuondoe hizi kero kwa Watanzania wote, na yule atakayejaribu kutukwamisha atakwama yeye na ataondoka yeye kwa sababu Watanzania wamechoka kusubiri tangu tupate uhuru.
“Tuna tanzanite, dhahabu, almasi, bahari ya hindi lakini watu wake ni masikini. Ninawaambia haiwezekani, tutatumia nguvu zote.
“Kama tatizo liko ndani ya Serikali mniachie mimi nitawanyoosha walioko ndani ya Serikali. Kila mtu ajipange kufanya kazi, lazima tutumie nguvu zetu zote. Na ninyi wananchi muisaidie Serikali kwenda mbele, wale wanaochelewesha maendeleo tuwapuuze,” alisema.
WANANCHI WA KINYEREZI
Aliwashukuru wananchi wa Kinyerezi kwa kukubali mradi huo na kwamba wale ambao bado hawajalipwa fidia zao watalipwa.
“Ninafahamu kuna matatizo madogo madogo, wapo watu waliolipwa fidia kama bilioni 30/-, wapo wachache ambao hawakulipwa fidia kama bilioni 2/-, hivi tutawaletea hela zenu tutawalipa, lakini wale waliolipwa wasifanye ujanja wa kusema walipwe mara mbili, hakuna hela ya bure, ni lazima niwaaambie kweli hili si shamba la biashara.
“Lakini wale ambao hawajalipwa, watalipwa kwa sababu kwa mujibu wa sheria ya vijiji namba tano ya mwaka 1999, sheria ya ardhi namba nne ya mwaka 1999 kifungu namba tatu pamoja na sheria ya mipango miji na matumizi bora ya ardhi ya mwaka 2007, inasisitiza mtu kulipwa fidia kama mradi fulani umewakuta.
“Kwa wale ambao hawajalipwa wala msipige kelele, hela zenu tutazileta. Wapo wawili walikataa kuzipokea hela, hao shauri lao lazima nisieme kweli na msema kweli ni mpenzi wa Mungu, lakini hao wawili wakitaka waje wapokee, wakitaka kwenda mahakamani waende ziko wazi,” alisema.
Uzinduzi huo wa mradi wa umeme wa Kinyerezi II ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, mabalozi mbalimbali, wabunge pamoja na Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko.