29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli afunga kufuli TRA

Pg 1*Amsimamisha kazi Kamishna Mkuu Bade, amteua Mpango kukaimu

*Waziri Mkuu Majaliwa asimamisha watano, awakabidhi mikononi mwa polisi

 

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

RAIS John Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Rished Bade, kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya Sh bilioni 80 na kumteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Philip Mpango, kukaimu nafasi hiyo.

Sambamba na hatua hiyo, Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, amewasimamisha kazi maofisa watano na watumishi watatu wa mamlaka hiyo kwa kosa hilo hilo na kuagiza kukamatwa kwa hati zao za kusafiria na kuhakikiwa kwa mali zao kama zinalingana na kipato chao wakiwa watumishi.

Waziri Mkuu Majaliwa pia aliliagiza Jeshi la Polisi kuwatia nguvuni maofisa na watumishi hao ili wasaidie uchunguzi wa upotevu huo.

Hatua hizo zilichukuliwa jana na Waziri Mkuu Majaliwa, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam akiwa na nyaraka mkononi zinazoonyesha wizi wa kontena hizo na namna ulivyofanyika.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliambatana na Bade na Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Servacius Likwelile, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Awadh Massawe na viongozi mbalimbali kutoka TRA na TPA.

Baada ya kufichua mipango miovu inayotekelezwa katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataja watumishi aliowasimamisha kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.

Aliwataja wengine waliokumbwa na hatua hiyo kuwa ni Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari ambaye haikufahamika mara moja idara yake na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.

“Hawa wanasimamishwa kazi na IGP, ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia polisi, hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma. Wanasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na pia wawe mikononi mwa polisi,” alisema Wziri Mkuu Majaliwa.

Alisema Bade na Naibu wake, Lusekelo Mwaseba, washirikiane na polisi kufuatilia upotevu huo na wahakikishe makontena yaliyopotea yanapatikana na Sh bilioni 80 zilizotakiwa kulipwa serikalini zilipwe.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani. Aliwataja watumishi hao kuwa ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.

Agizo jingine lililotolewa na Waziri Mkuu Majaliwa lilielekezwa kwa Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Likwelile, aliyetakiwa kupeleka haraka wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-Govt) katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kukagua mifumo ya taarifa za ulipaji kodi ili kubaini jinsi wizi unavyotekelezwa.

“Ninataka uchunguzi uanze kufanyika mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini hadi kwenye ICDs, nataka makontena hayo yatafutwe hadi yajulikane yako wapi na fedha hizo zihakikishwe zinarudi serikalini,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kabla ya kufikiwa kwa hatua hiyo, Bade alilazimika kujibu maswali ya Waziri Mkuu kuhusu namna makontena hayo yalivyopotea, ambapo alieleza kuwa kweli kuna makontena yaliyopotea na uchunguzi umebaini wizi hufanyika kati ya bandarini na ICDs, hususan ya Ubungo.

Bade alisema uchunguzi uliofanywa na TRA ulionyesha kuwepo kwa upotevu wa makontena 54, lakini baadaye uchunguzi wa kina ulibaini kuwa upotevu huo ni mkubwa zaidi, ukihusisha makontena 327.

“Hata hivyo, tulipoendelea na ukaguzi namba iliongezeka na kufikia 327, tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), mmiliki wa ICD ametakiwa kulipa faini Sh bilioni 12.6 na ameshalipa Sh bilioni 2.4,” alisema Bade.

Alipoulizwa Bade na Waziri Mkuu Majaliwa kama anayo majina ya watumishi wanaojihusisha na wizi huo, alisema ipo lakini kwa wakati huo hakuwa nayo mpaka aipate kutoka kwa wasaidizi wake.

Jibu hilo halikumridhisha Waziri Mkuu Majaliwa, ambaye alitoa orodha inayoonyesha jinsi kontena 349 zilivyopotea, namba za magari zilizoyabeba na Bade alikiri kwamba orodha hiyo ni ya kweli.

Baada ya kutoa orodha hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema: “Kwa utaratibu huo hatuwezi kufika, labda baadhi ya watu waondolewe kazini.”

Taarifa nyingine iliyopatikana kutoka Ikulu muda mfupi kabla hatujakwenda mitamboni ilimkariri Katibu Mkuu Kingozi, Balozi Ombeni Sefue, akiagiza kuwa maofisa wote wa TRA hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya nchi mpaka uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles