30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI AFICHUA SIRI NZITO YA URAIS

EVANS MAGEGE na DERICK MILTON


RAIS Dk. John Magufuli ametoa kile ambacho yeye mwenyewe amekiita kuwa siri kuhusu uamuzi wake wa kumteua Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka  akisema vyombo vyake vilimwambia hafai kuwa Mkuu wa Mkoa au Wilaya.

Kauli hiyo aliitoa jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Sarunda mjini Bariadi, wakati akimpongeza Mtaka na wasaidizi wake kwa jitihada zao za kuijenga upya Simiyu.

Akizungumzia uamuzi wake wa kumteua  Mtaka, Rais Magufuli alisema wakati mwingine watu wazuri huwa  wanapigwa vita.

“Nataka niwaeleze ukweli, wakati najaribu kutafuta wakuu wa wilaya  na  mikoa, Mtaka walisema hafai katika ripoti niliyopewa, naitoa hiyo siri hapa, walisema hafai hata U- DC (Ukuu wa Wilaya) ndio mapendekezo niliyoletewa na vyombo vyangu.

“ Nikajiuliza kama ni kweli Mtaka hafai hata U-DC nikambandika nikampa U-RC (Ukuu wa Mkoa) ili niwakomeshe kabisa wale waliokuwa wanazungumza hafai.

“Lakini nimeuliza tena waniletee ripoti ya wakuu wa mikoa wanaofanya kazi vizuri,  Mtaka ndiye namba one(moja) na namba mbili. Kwa hiyo saa nyingine watu wanaopigwa vita ndio wazuri na wazuri ndio wanawekewa maneno ya ajabu ili wakukatishe tamaa,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Akichanganya na utani kidogo Rais Magufuli alisema Mtaka yupo mkoani Simiyu na ameyataka yote vizuri ambapo kwa sasa mkoa huo umepata kiwanda cha chaki na cha maziwa.

Alisema mkuu huyo wa mkoa anajua kutafuta kutoka kwa mawaziri kwa ajili ya mkoa wake na kwamba hapigi kelele sana.

“ Mambo yake anayafanya silent (kimyakimya) ‘olo ulechola nkema, osizeyoga sana, jingaka duho polepole…kwani ukolizunya duho eligosha elo leleyoga  ng’wi barabara?.. Ale ayo kakajaga polepole lilebembeleza ng’wana mbhate nakutogwile , ango ukonyamke ng’wenekele doho,”.

Tafsiri ya maneno hayo ya lugha ya kisukuma kwa kiswahili kisicho rasmi ni kwamba; “ kama unatafuta mwanamke  usipige kelele sana, tongoza tu polepole …kwani utalikubali janaume linalopiga kelele barabarani?…kwa hiyo wanaume wanaokwenda polepole  akimbembeleza binti fulani , huyo binti si atageuka mwenyewe,”

Alisema Mkuu huyo wa Mkoa amefanikisha kutekeleza sera ya viwanda kwa vitendo, ambapo amewezesha kuanzisha viwanda mbalimbali vikiwemo chaki, maziwa, viatu pamoja na vya kusindika nafaka.

Rais Magufuli aliwasisitiza viongozi walio chini yake wajitahidi kujibu hoja za wananchi kwa vitendo.

Alisema serikali yake ina nia ya dhati ya kuwasaidia wakulima ndio maana wameondoa ushuru wa mazao ili kuwapa nafasi ya kusafirisha mazao yao.

Rais Magufuli pia alirejea kauli yake ambayo amekuwa akiitoa mara kwa mara kwamba hatagawa chakula kwa mtu yeyote hakulima wakati wa mvua.

“ Mvua nyingine zije uingie ndani ukafanye shughuli nyingine, alafu useme unaitegemea serikali. Kwenye vitabu vya Bibilia imeandikwa asiyefanya kazi na asile na asipokula maana yake afe, huo ndio ukweli. Ni lazima watu tufanye kazi , haiwezekani jirani yako kaivisha mawele halafu wewe huna hata hindi moja,” alisisitiza .

Katika hatua nyingine Rais Magufuli aliwataka viongozi wote katika mikoa na wilaya, kutowafukuza wafugaji na kuwanyanyasa wakiwemo wakulima, na badala yake waumize vichwa kutatua changamoto zinazowakabili.

Akizungumzia ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Bariadi hadi Maswa yenye urefu wa kilometa 49.7 inayojengwa kwa gharama ya zaidi shilingi bilioni 80 ambayo aliweka jiwe la msingi alisema itasaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Simiyu na kuongeza kipato kwa wananchi, ikiwa pamoja na kukuza pato la taifa.

Rais Magufuli pia aliwataka wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanatenga fedha za vijana, wanawake na walemavu kama sheria inavyotaka ili kuwezesha makundi hayo kujikwamua kiuchumi.

Akizundua jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu, Rais Magufuli alitoa kiasi cha shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuongeza majengo mengine kwenye hospitali hiyo ili kuweza kutoa huduma zote kwa wananchi wa Mkoa huo.

Awali akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Lamadi, Rais Dk. Magufuli alisema  suala la ulinzi wa rasilimali za nchi ni jambo la wananchi wote.

Kwamba tatizo la uvuvi haramu limesababishwa na maafisa uvuvi, ambapo alimtaka Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpiga, kuwakamata maafisa uvuvi wote ambao maeneo yao yatakutwa na uvuvi haramu.

Alimtaka Waziri huyo kuwamata viongozi wa vijiji hasa mwenyeviti kwenye eneo ambalo litakuwa limekithiri kwa uvuvi haramu, ili kuweza kuwataja wahusika wote wanaojihusisha na uvuvi huo.

Rais Magufuli pia alimtaka Mpina kuendelea na opereisheni hiyo ya kupambana na uvuvi haramu, huku akieleza kuwa zoezi hilo ni endelevu na wala halina mwisho.

Alisema viwanda vingi vya samaki vimekufa kutokana na kukosekana kwa samaki Ziwa Victoria kwa sababu ya kuongezeka kwa uvuvi haramu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles