24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI AAGIZA UCHUNGUZI KODI NDEGE ZA SAMAKI


Na CLARA MATIMO - MWANZA  |  

RAIS Dk. John Magufuli amemwagiza Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Ester Madale, kufanya uchunguzi ili kubaini sababu ya ndege za kusafirisha samaki nje ya nchi kusitisha safari zake katika uwanja huo na kwenda Kenya.

Agizo hilo amelitoa mjini hapa jana muda mfupi baada ya kutua uwanjani hapo akitokea nchini Uganda katika mkutano  wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuzungumza na wafanyakazi wa uwanja huo.

Wafanyakazi hao walisema kwa sasa ndege za kubeba samaki haziji katika uwanja huo kwa madai kuwa wanatozwa kodi kubwa kuliko Kenya.

Mmoja wa wafanyakazi wa uwanja huo, alisema kwa sasa ndege hazifiki tena uwanjani hapo kutokana na kutozwa kodi kubwa na samaki wanasafirishwa kwa magari hadi Kenya kisha kupakiwa katika ndege.

“Hapa uwanjani gharama ya kodi kwa ndege zinazobeba samaki imeongezwa, hivi sasa zinatua nchini Kenya, hata samaki wanaotoka Mwanza wanaenda kwa magari makubwa hadi huko jambo linalosababisha tukose mapato,” alisema.

Kutokana na kauli hiyo, Madale alisema awali ndege hizo za samaki zilikuwa hazitozwi kodi na Serikali (withholding  tax) na zilipoanza kutozwa walianza kusafirisha hadi Kenya na changamoto nyingine ilikuwa ni kuzuiliwa kwa ndege kubwa za mizigo kusafiri kutokana na kuwa na kelele na uchafuzi wa mazingira.

“Hizi ndege zilizokuwa zikibeba samaki ni zile za mizigo ambazo zilikuwa zikija na vipuli vya migodi na wakimaliza wanabeba samaki, zilizuiliwa kwa kuwa zilikuwa zina kelele kubwa na uchafuzi wa mazingira ndiyo sababu sasa haziji tena,” alisema.

Kutokana na taarifa hiyo, Magufuli aliagiza uongozi wa uwanja huo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufuatilia kujua wanatoza kiasi gani na kumtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuangalia jambo hilo.

Katika hatua nyingine, Magufuli aliwataka wananchi wanaoishi Kata ya Shibula wanaodaiwa kuvamia eneo la uwanja huo kutoendeleza makazi yao hadi hapo mgogoro baina yao na uwanja utakapoisha.

Aliuagiza uongozi wa uwanja huo kuanza kufanya tathmini ya gharama za kujenga majengo ya abiria (terminal) na Serikali itahakikisha inapanua uwanja huo hadi kufikia kiwango cha kimataifa ili kukidhi mahitaji ya abiria wa kimataifa.

Pia aliagiza kuangalia eneo linalohitajika kwa upanuzi wa uwanja huo, ikiwa linakidhi mahitaji basi wananchi waliopo watahamishwa kupisha uwanja na kwa wale waliopo eneo lisilohitajika wabaki.

“Serikali ya CCM haiwezi ikafikia hatua ya kuwafukuza wananchi wenye kaya zaidi ya 1,900 kwa sababu uwanja ni wetu,  wananchi ni wetu, ardhi ni yetu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula ni mwanachama tena wa hapa hapa na hao hao ndio walimpigia kura.

“Kwahiyo ni lazima tuangalie utaratibu ulio mzuri, lakini wananchi msiendeleze makazi yenu hadi hapo tathmini itakapofanyika, ambao watakuwa katikati ya uwanja wa ndege lazima wataondoka, lakini walio pembeni tutaliangalia hapa, nazungumza kwa ujumla, ni pamoja na wananchi wanaoishi maeneo ya jeshi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles