31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli aagiza mkandarasi wa maji akamatwe

*Ni aliyepewa mradi wa maji wa bil 1.7/-, ashindwa kuukamilisha

*Kamanda ya Polisi chupuchupu kutumbuliwa, OCD  asimamishwa kazi kwa kukaidi agizo la Waziri Lugola

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

Rais Dk. John Magufuli, ameagiza kukamatwa kwa mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa miradi ya maji mkoani Rukwa na uchunguzi ufanyike ili kubaini waliokuwa wakimpa miradi hiyo.

Akizungumza katika ziara yake mkoani Rukwa jana, kabla ya ufunguzi rasmi wa barabara ya Tunduma-Sumbawanga, Rais Magufuli aliagiza kukamatwa kwa mkandarasi huyo kwa kushindwa kutekeleza miradi ya maji yenye thamani ya Sh bilioni 1.7.

Alisema mradi huo uliotolewa kwa mkandarasi huyo kutoka kwa fedha za walipa kodi masikini wa Tanzania hadi sasa wananchi hawajapata maji, wakati mkataba wa Serikali na mkandarasi huyo akimaliza wananchi wapate maji na yeye apate fedha.

Alisema anashangazwa kuona mkandarasi huyo kupitia Kampuni ya Faric Contractors akiendelea kuwepo uraiani huku kukiwa hakuna juhudi zozote za kumchukulia hatua za kisheria.

“Hadi sasa maji hayapo na ninasikia mradi ukachomwa kabla hata haujakamilika, sola zaidi ya 150 zikaungua, vyombo vya dola vipo, PCCB ipo, Polisi wapo wala sijasikia wamepelekwa mahakamani, au wameshapelekwa mahakamani yeyote aliyechoma? Au kuna upelelezi bado unaendelea?” alihoji.

Mkuu huyo wa nchi, alitaka wahusika wote wakiwemo wa ubadhirifu wa mradi huo ambao wako nje kwa dhamana wakamatwe na warudishwe rumande na upelezi ukamilike ndani ya siku saba, kisha watuhumiwa wafikishwe mahakamani.

Aliwataka viongozi wa Polisi na PCCB kufanya uchunguzi haraka na kutoa muda wa siku saba

“Inachukua muda gani kuwapeleka mahakamani? Waghusika waliokamatwa wako wapi? kwa nini wakae nje kwa dhamana wakati hizi fedha bilioni 1.7 zimepotea wananchi hawa wanakosa maji, inawezekana wengine wamekunywa maji yenye magonjwa wanakufa, huyu yuko nje kwa dhamana tu anatembea, tuma askari wako sasa hivi wamkamkamate wamweke ndani.

“Nawapa siku saba, wewe wa PCCB RPC na wengine wote wanaohusika muhakikishe haya munayamaliza, kama ni kupelekwa mahakamani wapelekwe, miezi miwili mnapeleleza tu? Msinifanye nichukue hatua za ajali, na nitafuatilia mwenyewe,” alisema

Alimtaka Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, kuwafuatilia watu wote wanaohusika kumpa miradi hiyo mkandarasi huyo ambaye amekuwa akipata miradi hiyo na kwamba watu wa manunuzi na Bodi ya Wakandarasi wahakikishe miradi yote inatathminiwa upya.

“Na katika hili nitaondoka na mtu, nawahakikishia,” alisistiza

Alisema mkandarasi huyo amepewa miradi katika maeneo mbalimbali yenye thamani ya zadi ya Sh bilioni 10 ikiwemo ya Wilaya za Nkasi na ya Kalambo, ambapo inaonekana haijakamilika na wananchi hawajapata maji.

Alisistiza kwa kutoa maagizo kwa Waziri wa Maji, Profesa Mbarawa kuhakikisha kuwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kumpa mkandarasi huyo miradi hiyo ya maji nao wakamatwe na waunganishwe naye, kwa kuwa inaonekana kuna mtandao mkubwa kuanzia wilayani hadi wizarani.

“Kwa hali hii, kwa hiyo mnaweza kuona kilio cha watu wa Rukwa, nataka waziri wa maji uwe na timu yako maalumu ya kufuatilia hili. Na ikiwezekana wewe ubaki huku huku kulishughulikia.

“Na tena inawezekana ameshalipwa hata vyeti (certificates) zote na kama ameshalipwa na huyo aliyemlipa awekwe ndani. Haiwezekani ukamlipa certificates zote kabla miradi haijakamilika,” alisema.

Rais Magufuli, alisema kuwa fedha zinatafutwa na Watanzania, ambao wanatakiwa wapate maji, haziwezi kuachwa zipotee hivi hivi.

Kutokana na hali hiyo aliitaka Wizara ya Tawala za  Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nayo ifuatilie aliyekuwa akilipa fedha hizo zaidi ya Sh bilioni 10 wajulikane wote, na asibaki hata mtu mmoja.

Alisema zaidi ya Wizara ya Maji, jukumu hilo pia litatekelezwa na Wizara ya Tawala za  Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Halmashauri, Mkuu wa Polisi Mkoa (RPC), Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) na mwakilishi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa pamoja wanatakiwa kufuatilia suala hilo.

RPC aponea chupuchupu

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alionyesha kukasirishwa na hatua ya kutotekelezwa kwa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kutaka askari tisa wahamishwe katika kituo cha polisi cha Majimoto mkoani humo, akisema hiyo inaonesha dharau kwa wateule wake.

Akiwa ziarani mkoani Katavi, Jumapili Septemba 29, mwakhuu, Lugola alitoa siku saba kwa Polisi Mkoa wa Katavi kuwahamisha askari wote wa kituo cha Polisi ambao walikuwa wakituhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa na kubambikizia watu kesi.

Katika mahojiano yake na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa (RPC), George Kyando , Rais Magufuli alimtaka aeleze iwapo maagizo hayo ya Lugola yametekelezwa au la, ambapo alielezwa na RPC huyo kuwa bado hajayapata majina yao kwa kuwa wakati wa tukio hilo alikuwa safarini.

Kyando alimweleza Rais kuwa bado hajapata taarifa rasmi kutika kwa msaidizi wake, OCD Pilycarp Urio ambaye alimwachia ofisi na kwamba aliuliza aliporudi kutoka safarini lakini hakupata majibu yanayoeleweka.

Kyando alisema alisikia agizo hilo kupitia kwenye vyombo vya habari na kwamba alipofuatilia alimtaka msaidizi wake, ambaye ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kumpa orodha ya askari hao lakini hadi jana hakuipata kwa kuwa alielezwa kuwa bado hajapata majina ya askari hao.

“Mimi huyu ni mteule wangu, nimemteua mimi, anatoa maagizo nyie hamtekelezi, hii ni dharau, ukatekeleze,” alisema Rais Magufuli.

Alisisitiza kuwa akitoka mjini hapo hapo jana atakuwa safarini kuelekea Sumbawanga na akifika huko anahitaji apate taarifa kuwa tayari jukumu hilo limeshatekelezwa.

“Wewe kamanda wa polisi mpaka leo (jana) hujachukua hatua, unataka mimi nikufanye nini, unadhani nikitamka utabaki salama, sikuja kutumbua watu lakini mambo mengine mnanilazimisha, haiwezekani waziri atoe maagizo halafu yanapuuzwa tu na wewe ukabaki salama.

“Nikitika hapa ninaelekea Sumbawanga na akifika Sumbawanga nataka nipate majibu ya hatua zilizochukuliwa, la sivyo nitachukua hatua zangu mimi mwenyewe,” alisema Rais Magufuli.

Katika agizo lake Septemba 29, Waziri Lugola aliagiza kuchukuliwa hatua polisi tisa wa kituo cha polisi Laela lakini hadi jana Oktoba 6, ikiwa ni siku ya saba tangu kutolewa kwa agizo hilo hakukuwa na hatua yoyote iliyochukuliwa.

Pia waziri huyo aliiagiza Takukuru mkoani Rukwa kuchunguza miradi hiyo ya maji lakini mpaka sasa bado hatua hazijachukuliwa, kitendo ambacho Rais Magufuli alisema hakivumiliki kuona kuwa wanapuuza maagizo ya mawaziri.

Simu kwa IGP

Hata hivyo, Rais Magufuli aliendelea kufuatilia suala hilo na alimpigia simu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro na kumuamuru amsimamishe kazi OCD huyo aliyekaidi kutekeleza agizo hilo la Lugola.

Katika amzungumzo hayo ya simu, Rais Magufuli alimuagiza IGP Sirro, kumsimamisha kazi OCD huyo ahadi atakapompa maelekezo mengine.

“Kuna Asistat Kamishna wa Polisi anaitwa Pilycarp Urio yuko huku Rukwa, msimamishe kazi hadi nitakapokupa maelekezo mengine,” alisema Rais Magufuli katika maagizo yake kwa IGP Siro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles