29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 18, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Magoti wa LHRC, mwenzake kortini kwa uhujumu uchumi

ERICK MUGISHA-DAR ES SALAAM

HATIMAYE mfanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (26) pamoja na mwenzake  ambaye ni mtaalamu wa Tehama, Theodory Giyani (36), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la uhujumu uchumi.

Magoti na mwenzake walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka matatu likiwamo la utakatishaji fedha cha Sh milioni 17.3 kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Wakisomewa mashtaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega pamoja na jopo la mawakili wanne wa Serikali.

Hata hivyo Hakimu Mtega, alisema kuwa washtakiwa hao  hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka  nchini (DPP).

Akisoma mashataka hayo mahakamano hapo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kuwa Magoti na Giyani, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 137/2019, huku akidai kuwa katika shtaka la kwanza, Magoti na Giyani wanadaiwa kushiriki genge la uhalifu.

Kosa hilo wote wawili wanadaiwa kutenda, katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi na Desemba 17, 2019 jijini Dar es Salaam katika maeneo mbalimbali ya ndani ya nchi, ambapo Magoti, Giyani na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani, kwa makusudi wanadaiwa walishiriki makosa ya uhalifu ikiwa ni kumiliki programu za kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kufanya uhalifu.

Hata hivyo Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai katika shtaka la pili, washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, wanadaiwa siku na eneo hilo, wanadaiwa kumiliki  programu za kompyuta kwa lengo la kutenda kosa la uhalifu.

Na katika shtaka la tatu, ambalo ni kutakatisha fedha, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude, alidai Magoti na Giyani, wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Februari Mosi na Desemba 17, 2019 katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ndani ya nchi.

Wanashtakiwa hao wanadaiwa katika tarehe hizo, wanadaiwa walijipatia Sh milioni 17.35 wakati wakijua fedha hizo ni zao tangulizi la kushiriki genge la uhalifu.

Hata hivyo upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika  ambapo Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 7, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

KUKAMATWA KWAKE

Magoti alikamatwa Ijumaa Desemba 20, mwaka huu eneo la Mwenge  huku Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kilazimika kutaka kujua alilipo mtumishi wao hasa baada ya kumkosa kwenye vituo vya polisi jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alikiri kushikiliwa kwa Magoti na wenzake watatu ambapo hakueleza yupo kituo gani.

Pamoja na jitihada mbalimbali za watendaji wa LHRC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wao, Anna Henga kuzunguka katika vituo mbalimbali ikiwamo na kituo kikuu walijikuta wakigonga mwamba.

Kutokana na hali hiyo juzi Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadami (THDRC) na Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu (WHRDs) walifungua kesi Mahakama Kuu kumshtaki Mambosasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutaka walazimishwe kumpa dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles