UGONJWA huu una madhara mbalimbali, yapo yanayoonekana moja kwa moja na mengine yanakuwa ndani kwa ndani.
Moja ya madhara hayo ni figo kushindwa kufanya kazi, figo zinapochuja damu yenye sukari nyingi zinachoka mapema.
Hatua hiyo inachangia mhusika baadaye kushindwa kabisa kufanya kazi kama inavyopaswa.
Mbali na hilo, mgojwa pia anapata tatizo la mishipa ya damu kushindwa kufanya kazi, binadamu anapokuwa na sukari nyingi kwenye damu huharibu mishipa ya fahamu.
Hali hii husababisha mgonjwa kuanza kupata ganzi, hasa katika miguu na huweza kukanyaga vitu vyenye ncha kali bila kusikia maumivu.
Athari nyingine ni upofu, mgonjwa wa kisukari ana hatari ya kupata upofu kwa sababu ya kuharibika kwa retina.
Kitaalamu eneo maalumu kwa ajili ya kumfanya binadamu aone linajulikana kama retina, hii huharibiwa kwa uwepo wa sukari nyingi kwenye damu.
Pia ugonjwa kisukari una tabia ya kuleta kidonda mguuni, hiki kitaalamu huitwa diabetic foot, kidonda hiki huanza chenyewe bila maumivu yoyote na huwa kinakuwa chini ya nyayo.
Kidonda hicho mara nyingi ndiyo chanzo cha wagonjwa wa kisukari kukatwa miguu kwa kuhofia kwamba kinaweza kikapanda mpaka juu bila kuonekana.
Mgonjwa wa kisukari pia ana hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi, huu hutokea pale mishipa ya damu inapozibwa kichwani na kiasi kikubwa cha mafuta na cholesterol ambavyo vyote huambatana na ugonjwa huu pia.
Kwa wanaume pia hupata athari kubwa ya kuishiwa nguvu za kiume, nguvu za kiume zinategemea sana msukumo wa damu kukaa kwenye uume ili kuleta ule ukakamavu ama nguvu.
Mtu mwenye kisukari huwa na cholesterol ambayo huziba ile mishipa midogo midogo ya damu ya kwenye uume na kusababisha nguvu hizo kuisha kabisa na uume kuwa mdogo ama kushindwa kusimama.
Itaendelea wiki ijayo…