MAGEREZA KUFUFUA KIWANDA CHA SUKARI

0
604

Na Kulwa KarediaJESHI la Magereza limeanza kutekeleza mpango wake wa kufufua kiwanda chake cha Sukari na kilimo cha miwa katika Gereza la Mbigiri mkoani Morogoro, kwa lengo la kuongeza kiwango cha upatikanaji wa sukari hapa nchini ikiwemo kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.

Pamoja na kiwanda hicho kuongeza upatikanaji wa sukari hapa nchini, lakini pia kufufuliwa kwa kiwanda hiki kutatoa fursa ya ajira kwa wananchi ambao watafanya kazi kwenye kiwanda hicho kwa ujumla.

Katika kutekeleza mpango huo, hatua za awali za upembuzi yakinifu umeshafanyika na shughuli za kilimo tayari zimeanza katika eneo hilo kwa kutumia maktrekta matatu mapya ya kisasa ambayo hadi sasa yameshalima ekari 1000.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk. Juma Malewa, anasema katika kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda, Jeshi hilo limeainisha baadhi ya miradi inayoweza kuiweka Tanzania katika uchumi wa viwanda, ikiwamo ufufuaji wa kiwanda hicho katika Gereza lake la Mbigiri.

Dk. Malewa anasema kwa kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF, jeshi hilo limeanza kufufua kiwanda cha sukari na kilimo cha miwa.

Dk. Malewa anasema kiwanda hicho kilisitisha shughuli zake za uzalishaji mwaka 1996 kutokana na uchakavu wa miundombinu na teknolojia duni iliyokuwepo kwa wakati huo.

Anasema ubia kati ya Jeshi la Magereza na mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii, utawezesha kujengwa kwa kiwanda kipya cha kisasa ambacho kinategemewa kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 30,000 za sukari kwa mwaka, kiwango ambacho kitasaidia kuongeza upatikanaji wa sukari hapa nchini.

“Ni matumaini yetu hadi kufikia mwisho wa mwaka huu kiwanda hiki kitaanza kufanya kazi… ufufuaji wa kiwanda hiki utawaneemesha wakulima wadogo wadogo wa miwa (Outgrowers) waliopo maeneo yanayolizunguka gereza la Mbigiri… hivyo kuinua hali zao za kiuchumi kwa kuwa itakuwa ni fursa ya wakulima hao kupata soko la uhakika na karibu zaidi kwa ajili ya kuuza bidhaa zao baada ya kuvunwa kwenye mashamba yao’’. Dk. Malewa anasisitiza.

Anasema pamoja na ardhi yenye rutuba ambayo kwa jeshi hilo, linaiona ni fursa ikitumiwa vizuri, lakini pia ipo miundombinu mbalimbali inayoweza kusaidia kuanzisha viwanda na ardhi hii inaweza kutumika katika shughuli za kilimo na hivyo kuongeza uzalishaji wa chakula hapa nchini.

Anasema wafungwa wengi na wa kutosha waliopo ndani ya Jeshi hilo watatumika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji utakaofanyika katika maeneo ya viwanda na mashamba makubwa ya uzalishaji wa chakula yaliyopo kwenye Magereza mbalimbali.

Dk. Malewa anasema kuwa katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, Jeshi la Magereza tayari limeainisha baadhi ya Miradi inayoweza kuiweka Tanzania katika Uchumi wa Viwanda.

Jeshi hilo, lina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu na hivyo kufikia malengo yetu ya kuwa na uchumi wa viwanda. Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na ardhi nyingi yenye rutuba inayofaa kutumika kwa kushughuli za kilimo.

Dk. Malewa anasema pia Jeshi la Magereza lina mpango wa kuanzisha shughuli za kilimo cha kisasa cha umwagiliaji na kwa sasa lipo kwenye maandalizi ambapo umwagiliaji mkubwa unaandaliwa katika Gereza la Idete mkoani Morogoro.

Anasema kutokana na ukubwa wa eneo hilo lenye zaidi ya ekari 3,000 zinazoweza kutumika kwa shughuli za kilimo, litakuwa na uwezo wa kuzalisha tani za kutosha za zao la mpunga na hivyo kutosheleza mahitaji ya chakula cha wafungwa kwa wastani wa asilimia 50. Katika maandalizi ya awali tayari ekari 1,000 zimeshaandaliwa ikiwa ni sehemu ya maandalizi hayo.

Anasema mradi huo wa kuendesha kilimo cha kisasa na kulifanya jeshi hilo kujitosheleza kwa chakula cha kulisha wafungwa wanaotumikia vifungo vyao kwenye magereza mbalimbali nchini ulianza mwaka 2015 na kutarajiwa kukamilika mwaka 2020, utagharimu Sh bilioni 15 hadi utakapokamilika.

Anasema maandalizi ya awali ya upatikanaji wa mbolea na matrekta ya kisasa 50 yatasaidia kuboresha shughuli za kilimo hicho cha kisasa.

Anasema maboresho ya kilimo cha kisasa yanayoendelea ndani ya jeshi hilo yatalifanya kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2020,wakati shughuli za kilimo zinazofanyika kwa sasa katika maeneo mbalimbali ya magereza nchini yanaliweza jeshi hilo kujitosheleza kwa asilimia 20 tu.

Dk. Malewa, anasema mazao yatakayolimwa kwa wingi ni pamoja na mpunga, mahindi, maharage na alizeti kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta.
Anasema magereza ambayo yatatumika kwa ajili ya shughuli za kilimo cha kisasa, ni pamoja na Kitai mkoani Ruvuma, Kitengule mkoani Kagera, Molo Sumbawanga, Idete na Mbigiri mkoani Morogoro, Kwitanga mkoani Dodoma na gereza la Arusha.

Katika kujitosheleza kwa chakula, anasema jeshi hilo limejipanga kuendeleza ufugaji wa ng’ombe wa nyama, maziwa, kuku, nguruwe katika magereza mbalimbali,likiwamo gereza la Ubena- Morogoro, Pwani, Mugumu-Mara, Kitengule-Kagera na Mbigiri-Morogoro pamoja na gereza la KPF-Kingolwira Morogoro.

Anasema limeweka mkakati wa kupata matrekta na vyombo vya kisasa vya kilimo ambavyo vitatumika kuboresha shughuli za kilimo.

Kuhusu wataalamu, Dk. Malewa anasema wanao wa kutosha waliobobea katika shughuli za kilimo cha kisasa ambao watatumika kufanikisha mpango huo.

Anasema sasa lina hekta 130,000 na kati ya eneo hilo, hekta 60,540 ndizo zinazoweza zikatumika kwa shughuli za kilimo na ufugaji, eneo lililosalia ni eneo la makazi ya askari, mawe pamoja na miamba.

Katika utekelezaji wa mpango huo wa miaka mitano, litatumia wafungwa katika nyanja mbili moja ni kwa upande wa uzalishaji na nyingine ni ile kuwafundisha wafungwa wenyewe kilimo cha kisasa ujuzi ambao watautumia mara watakapomaliza kutumikia vifungo vyao kwenye magereza mbalimbali, jambo litakalosaidia wafungwa hao kutorudia kujishughulisha na matukio ya uhalifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here