21.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Magavana wa kiume Japan wanapoamua kubeba ‘mimba’

1NCHINI Japan, ambako wanawake hufanya kazi za nyumbani mara tano zaidi ya zile wafanyazo wanaume, wanasiasa wa kiume wameamua kuonja masahibu wanayokumbana nayo wake zao ikiwamo kubeba mimba bandia.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) mwaka 2014, wanaume wa Japan walishuhudiwa wakiongoza kutosaidia wake zao duniani.

Kwa mujibu wa OECD, wanawake watano wa Japan hufanya kazi za nyumbani kwa saa tano na wanaume saa moja tu.

Nchi hiyo pia imekosolewa kwa kutowajali kina mama wanaofanya kazi, kukiwa na karibu asilimia 70 ya wanawake wanaoacha kazi baada ya kujifungua mtoto wao wa kwanza.

Hivyo, wanasiasa hao Gavana wa Miyazaki Shunji Kōno, Gavana wa Yamaguchi Tsugumasa Muraoka na Gavana wa Saga Yoshinori Yamaguchi walishirikiana na Kampeni ya Kyushu Yamaguchi ya Uhamasishaji Maisha kutengeneza video inayowahamasisha wanaume wa Kijapan kujenga utamaduni wa kusaidia wake zao majumbani.

Katika video hiyo, magavana hao watatu wanaonekana wakiwa wamevaa tumbo bandia lenye uzito wa kilo 7.3 lenye umbo la mimba, uzito ambao ni sawa na ujauzito wa miezi saba.

Magavana hao wa maeneo ya kusini magharibi mwa nchi wanaendeleza hamasisho lenye kauli mbiu kuwa ‘gavana ni mwanamke aliye na mimba’.

Wanajichukua picha ya video wanamoonekana wakifanya shughuli za kila siku sawa na zile zinazofanywa na wanawake katika maisha ya kawaida ya nyumbani.

Katika video hiyo inayoonekana katika mitandao ya kijamii, wanaonekana wakipata tabu kupanda ghorofani, kubeba mizigo wakitoka sokoni au kusubiri mtu awahurumie na kuwaachia viti wanaposimama ndani ya basi.

Mara nyingi wanaonekana kusimama wakishika matumbo yao huku wakihema au kugugumia kwa uchovu.

Mmojawapo anaonekana akipata shida kuvaa soksi, na mwingine anaonekana akifuta jasho lililokuwa likitiririka usoni mwake baada ya kuanika nguo.

“Ninaona namna inavyokuwa shida kuwa mjamzito na kufanya kazi za nyumbani wakati huo huo,” anasema Gavana wa Miyazaki, Shunji Kono mwenye umri wa miaka 52.

“Kazi ni nzito mno na nahisi mabega na mgongo ukivuta,” baba huyo wa watoto watatu anasema kuhusu uvaaji wa vazi hilo.

Aliongeza: “Nadhani itabidi niwe mkarimu zaidi kwa mke wangu kwa namna nilivyobaini anavyopata shida.”

“Kwa kweli sikufahamu kuwa wanawake wanakumbana na hali hii,” anasema Tsugumasa Muraoka, Gavana wa Yamaguchi na baba wa watoto watatu. “Sasa nafahamu nini anachokumbana nacho mke wangu kwa miezi mingi, ninamshukuru sana.”

Mwishoni mwa video mmoja wa magavana hao anaonekana akiwa hajavalia tena vazi hilo. Akiwa na furaha na vicheko, anaonekana amembeba mtoto, akiwa ameigiza kana kwamba kashajifungua.

Kampeni ya magavana hao watatu imekuja huku wanawake wengi wa Japan wakiwa wanasema kuwa taifa lao hilo linapaswa kuboresha zaidi hali zao.

Mapema mwaka huu, wanawake wa Japan walitoa wito hadharani kwa waziri mkuu wa nchi hiyo, wakimtaka aboreshe mfumo uliodumaa wa vituo vya kutwa vya kulea watoto.

Vituo hivyo vimekumbwa na urasimu, unaowazuia wanawake wengi kupata kwa wakati mahali pa kuhifadhi watoto wao ili kuwawezesha kurudi kazini baada ya likizo ya uzazi kumalizika.

Kutokana na urasimu huo unaowafanya katika orodha ndefu ya kusubiri, wanawake wengi wa Japan wanalazimika kuacha kazi kabisa ili kulea watoto wao.

Waziri Mkuu Shinzo Abe aliahidi kufanya mabadiliko kadhaa yaliyolenga kuboresha mfumo wa utunzaji watoto.

Kitendo cha wabunge hao kinakumbushia kina baba watatu wa Uingereza, ambao mwaka jana wakati wa kuelekea Siku ya Kina Mama waliamua kubeba matumbo bandia yenye uzito wa kilo 15.8 kila moja kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Simulizi hiyo ambayo pia tuliitoa katika gazeti hili ilieleza kwamba kina baba hao walijaribu kuonja kile ambacho wake zao na wanawake wengine duniani hukutana nacho wakati wa kubeba mimba na wakati wa kujifungua.

Hatimaye, zoezi likafanyika, kina baba hao walishuhudiwa wakilalamika kuhusu matiti yao kuvimba, hitaji la mara kwa mara la kwenda haja ndogo na usingizi wao kukatishwa nyakati za usiku.

Lakini pia wanaume hao, ambao walikubali kuonja uchungu wa kubeba mimba, walienda mbali zaidi kupitia jaribio linalofanana na hali wanayokutana nayo wanawake pindi wanapojifungua.

Wakati wakurugenzi hao wa uchapishaji Jason Bramley, Steve Hanson na Jonny Biggins kupitia blogu yao ‘3pregnantdads.com’ walipowaambia mashabiki wao kuwa bado hawajafikia kilele cha uchungu ule wanaopata wanawake wajawazito walishauriwa kutumia mashine ya kielektroiniki.

Mashine hiyo huingiza vichocheo vinavyotengeneza mazingira sawa na anayopata mwanamke wakati wa kujifungua.

Baada ya zoezi hilo la pili, walikiri iwapo kubeba tumbo zito kutakufanya uone kile wanachokumbana nacho wajawazito kumbe ni ‘cha mtoto’, basi mashine hii itakuaminisha uchungu wa kujifungua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,656FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles