24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Mafuriko yamzidi nguvu Lowassa

LOWASSA 1*Avunja mkutano Tanga kwa hofu watu kupoteza maisha

 

Fredy Azzah na Amina Omari, Tanga

 

WAKATI baadhi ya watu wakimshawishi kuwania urais kupitia  Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa, alisema hawezi kuzua mafuriko kwa mikono.

Lakini jana jijini Tanga mafuriko hayo (watu) yalitaka ‘kumsomba’ kutoka na maelfu ya watu kufurika katika uwanja Tangamano kwa ajili ya kumsikiliza.

Baada ya kuona watu wanazidi kuongezeka, huku wengi wakianguka na kupoteza fahamu, Lowassa alitangaza kuuvunja mkutaano huo kwa hofu ya watu kukanyagana na kupotea maisha.

 

Hali ya kuwapo watu wengi katika mkutano huo ilianza kuonekana mapema, kwani wananchi walianza kufurika uwanjani hapo kuanzia saa 3:00 asubuhi, licha ya  kutangaziwa wafike saa 5:00 asubuhi na mkutano ungeanza saa 8:00 mchana.

Ilipofika saa 5:00 uwanja huo tayari ulikuwa umefurika, hali iliyofanya watu wengine kukaa kwenye majengo yaliyo pembeni ya uwanja huo na wengine kupanda kwenye miti.

 

Ilipofika saa 7 mchana, barabara ya Taifa inayounganisha jiji hilo na vitongoji vyake, ilifungwa ili kuepusha ajali kutokana na watu wengi waliokuwa katika eneo hilo.

 

Lowassa kuvunja mkutano

 

Dalili za mkutano huo kuvunjika zilionekana pale, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye alipopanda jukwaani.

Sumaye alitumia muda wake kueleza watu namna ya kusaidia wale wanaopoteza fahamu na watoto waliokuwa uwanjani hapo.

“Sisi Ukawa ni watu wa amani na utulivu, naomba msisukamane,” alisema.

Pamoja na kauli hiyo ambayo haikuzaa matunda, hali ilizidi kuwa mbaya ambapo alilazimika kumkaribisha Lowassa ili azungumze.

Kitendo cha Lowassa kukaribishwa kilionekana wazi kuzidisha mkanyagano mkubwa.

Lowassa, aliposimama wananchi walianza kushangilia kwa sauti, huku wakisukumana jambo lililosababisha watu kuendelea kupoteza fahamu.

 

Lowassa

 

Lowassa aliposimama alisema. “Hali iliyopo hapa si nzuri, tutapoteza maisha ya watu,” asante sana kwa mapokezi mliyonipa, nimekuja kutafuta kura sikujua kama wengi hivi.

 

“Leo mnanikumbusha Sumbawanga (Rukwa), Songea (Ruvuma) na Ujiji  (Kigoma), sasa hapa tunaahirisha mkutano huu kwa sababu watu wanaweza kufa, kinamama na watoto watakufa,” alisema Lowassa.

 

Baada ya maelezo hayo, alijaribu kushuka jukwaani lakini watu walionekana wanakiu ya kutaka kumsikiliza.

Lowassa alikaa takribani dakika tano akisikiliza watu waliokuwa karibu na jukwaa na akachukua tena kipaza sauti na kuanza kuwatuliza.

Safari hii aliwaahidi kuwa, ndani ya miezi sita baada ya kuchaguliwa, atafufua bandari ya Tanga na reli ili kuinua uchumi wa wakazi hao.

 

Baada ya kusema hivyo, wananchi walio wengi walianza kutaja jina la Babu Seya, na Lowassa na kusema akipata nafasi ya kuwa rais, ataagiza vyombo vya sheria kuangalia upya suala hilo.

Wakati hayo yakiendelea, watu waliendelea kusogea karibu na jukwaa na kulizunguka huku wakisema wanataka ajira.

Baada ya kuzungumza na na kuwatangazia kuwa mkutano umefungwa hivyo waondoke, waliendelea kukaa kwenye eneo hilo hali iliyomfanya na yeye kukaa juu ya jukwaa kwa takribani dakika 10 akiwasikiliza.

Baada ya hapo, Lowassa alishuka jukwaani na kuondoka.

Hata baada ya kuondoka watu walibaki wakiwa wamekusanyika uwanjani hapo huku kukiwa na makundi ya vijana waliokuwa wakiimba ‘CCM mafisadi’ , ‘CCM imekufa, imezikwa’ .

 

Chopa

Ilipofika saa 8, umati huo ulitangaziwa kwamba helkopta inayotumiwa na Lowassa kwenye mikutano yake, haitatua kwenye eneo hilo kama ilivyokuwa imepangwa  awali kutokana na uwanja huo kufurika watu.

 

Kutokana na hali hiyo, helkopta hiyo ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Tanga na kisha mgombea huyo kutumia gari kwenda uwanjani.

 

Kadri muda ulivyosonga, watu walikuwa wakizimia kutokana na kukosa hewa hali iliyosababisha na wingi wa watu.

 

Mmoja wa maofisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu waliokuwa uwanjani hapo, alisema watu waliopoteza fahamu walikuwa zaidi ya 50.

 

Mabomu ya machozi

 

Watu waliokuwa uwanjani hapo, walipokuwa wakitoka walijaa kwenye barabara  ya Taifa na kufanya isitumike.

Hali hiyo ilidumu takribani dakika 20 hali iliyofanya polisi wapige mabomu ya machozi ili kuwatawanya.

Kabla ya mkutano huo, Lowassa alifanya mikutano Mombo wilayani Korogwe na Bumbuli wilayani Lushoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles