23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mafunzo ya usalama Osha ni zaidi ya darasa

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Saa nne za mafunzo ya usalama kazini kwa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta) zilionekana hazitoshi kutokana na wengi kuwa na shauku ya kutaka kujifunza zaidi.

Wako waliosikika wakisema ‘kumbe tunajimaliza wenyewe’, ‘nitanunua kiti changu niende nacho ofisini’, ‘nitaanza kubeba kipande cha mkaa kwenye mkoba wangu’ na wengine wakasema sasa wataweza kuchukua tahadhari wanapokuwa katika majukumu yao ya kila siku.

Mkufunzi wa Huduma ya Kwanza kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha), Moteswa Meda, akionyesha jinsi ya kumhudumia mtu aliyezimia wakati wa mafunzo kwa wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya habari nchini (Jowuta).

Wanachama hao wa Jowuta kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani walipigwa msasa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha) katika maeneo mbalimbali kama vile Sheria Namba 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, huduma ya kwanza, ajali katika mazingira ya kazi na athari zake kiuchumi na kijamii.

Wakufunzi wa Osha, Wakili Rehema Msekwa, Shaaban Mbaga na Moteswa Meda waliwanoa wanachama hao kinadharia na kivitendo hatua iliyowapa hamu ya kujua zaidi na kufanya darasa kuwa shirikishi kutokana na maswali yaliyokuwa yakiulizwa kila baada ya mada husika.

Meda ambaye ni Mkufunzi wa Huduma ya Kwanza wakati akifundisha kwa vitendo namna ya kumhudumia mtu aliyezimia, karibu wanafunzi wote walisogea mbele kumuangalia huku mfano ukitolewa kwa mmoja wao ambaye alilala chali kuonyesha amezimia.

Meda pia alitoa mafunzo ya namna ya kumuokoa mtu aliyekunywa sumu au kuumwa na wadudu kama vile nyoka, tandu, nge na wengine.

“Siyo nyoka wote wana sumu, nyoka wenye vichwa vya pembe tatu au macho ya duara hawana sumu, lakini wale wenye magamba kama ya samaki sehemu za kwenye mkia wana sumu. Sehemu iliyoumwa na nyoka isifungwe kamba, inatakiwa ining’inie chini ya usawa wa moyo na aliyeumwa na nyoka asitembee, anatakiwa abebwe. Ukiumwa na ng’e au tandu safisha jeraha kisha wahi hospitali…mawe ya nyoka hayafanyi kazi,” alisema Meda.

Mkufunzi huyo alisema kwa mtu aliyekunywa sumu hairuhusiwi kumpa kimiminika cha aina yoyote (mfano maziwa au maji), au kumtapisha bali anaweza kuokolewa kwa kutafuna kipande cha mkaa ambao husaidia kufyonza sumu husika.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha), Hadija Mwenda, akizungunza wakati wa mafunzo kwa wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari nchini (Jowuta). Kulia ni Mwenyekiti wa Jowuta, Mussa Juma na Wapili kushoto ni Katibu Mkuu wa Jowuta, Suleiman Msuya

Somo la ukaaji wakati wa kutumia kompyuta lililotolewa na Meneja Mafunzo na Uhamasishaji Osha, Shaaban Mbaga, liliwagusa wengi hasa ikizingatiwa kuwa kwa sehemu kubwa waandishi wa habari wanatumia kifaa hicho katika majukumu yao ya kila siku.

Mbaga alionyesha aina ya mkao ambao mtu anapaswa kukaa wakati wa kutumia kompyuta, mkao hatari na jinsi ya kufanya kukaa mkao unaoshauriwa kitaalam.

Mtendaji Mkuu wa Osha, Hadija Mwenda, akapigilia msumari kwa kusema magonjwa mengi kama ya misuli, viuno, shingo na mgongo ndiyo yanaenea kwa kasi huku aina ya ukaaji na viti vinavyotumiwa na wafanyakazi vikitajwa kuchangia hali hiyo.

Mwenda aliwaonyesha waandishi kiti kinachopaswa kutumika ofisini ambacho hakiwezi kumsababishia mtu tatizo la mgongo au kiuno.

“Hatua hii ya kuwapatia mafunzo ni kubwa inayoonyesha jinsi Jowuta inavyowajali, hakuna mazingira ya kazi ambayo hayana vihatarishi, lakini hata kama mwajiri hajanunua jijali…afya yako ni mtaji wako,” alisema Mwenda.

Alisema kazi ya Osha ni kuhakikisha vihatarishi havimuathiri mfanyakazi ili afanye kazi kwa tija na hata baada ya kustaafu aendelee kuishi ndiyo maana wananalinda nguvu kazi ambayo ni mtaji namba moja wa nchi yoyote ile.

Wakili wa Osha, Rehema Msekwa, anasema Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ilitungwa kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi wakiwa kazini ili wasipate majanga au magonjwa yanayotokana na kazi wanazofanya.

Sheria hiyo inaelekeza kuwepo kwa sanduku la huduma ya kwanza ambalo litakuwa chini ya mtu aliyepata mafunzo ya huduma ya kwanza, waajiri watengeneze sera ya usalama na afya mahali pa kazi, kutoa taarifa za magonjwa kazi ili Osha waweze kufanya ukaguzi katika taasisi husika.

Kulingana na Msekwa adhabu kwa kukiuka sheria hiyo ni kulipa faini ya papo kwa papo kuanzia Sh 500,000 au kifungo kisichopungua miaka mitano.

Kilichowasukuma Jowuta kuomba mafunzo

Katibu Mkuu wa Jowuta, Seleman Msuya, anasema wana wanachama zaidi ya 400 nchi nzima na kwamba walisukumwa kuiomba Osha iwajengee uwezo wa mafunzo ya usalama kazini ili wafanye kazi katika mazingira salama.

“Changamoto tunazopitia sekta ya habari zinaweza kupata muafaka kupitia ushirikiano baina ya wadau, mafunzo haya yatasaidia wafanyakazi wapate haki wanazostahili kama vile usalama kazini, masilahi na nyingine,” alisema Msuya.

Mwenyekiti wa Jowuta, Mussa Juma, alisema anaamini kupitia mafunzo hayo wanachama hao watakuwa na uwelewa wa kutosha na kuwaasa wakawe mabalozi kwa wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles