Mafunzo kwa wataalamu wa saratani EAC wazinduliwa

Vivienne Yeda
Vivienne Yeda
Vivienne Yeda

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) na Ubalozi wa Uingereza kwa kushirikiana na Chuo cha Madaktari cha Royal (London), wamezindua mpango wa mafunzo na ushirikiano unaolenga kutoa mafunzo  kwa wataalamu 600 wa ugonjwa wa saratani katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Vivienne Yeda, mafunzo hayo yatakuza uwezo wa kitaalamu katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza hasa saratani na matatizo ya ubongo na mishipa ya fahamu katika ukanda wa  Afrika Mashariki.

“Mkazo utakuwa zaidi kwenye kutambua mapema, tafiti na matibabu ya saratani na matatizo ya ubongo na mishipa ya fahamu katika maeneo ambapo upatikanaji wa wataalamu wenye sifa bado ni changamoto,” alisema Yeda  wakati wa uzinduzi wa mpango huo hivi karibuni jijini Nairobi.

Mafunzo hayo yanakuja wakati ambapo idadi ya wagonjwa wa saratani duniani inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 75 katika kipindi cha miongo miwili ijayo kwa mujibu wa Utafiti wa Saratani wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Vifo vitokanavyo na saratani vimezidi kuongezeka katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo takribani watu 50 hufariki kila siku nchini Kenya kutokana na aina mbalimbali za saratani.

Mwenendo huo pia upo katika nchi nyingine za ukanda huo, huku sababu kuu ikihusishwa  na ukosefu wa vifaa vya matibabu na utaalamu kwa ajili ya matibabu, kuzuia na kutambua mapema.

Kwa mujibu wa Yeda,  Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)  kwa muda mrefu imeshindwa kuzuia na kutibu janga la saratani kwa sababu ya ukosefu wa madaktari waliopata mafunzo na ujuzi wa kutosha kukabiliana na ugonjwa huo.

Uwiano wa daktari kwa idadi ya watu katika ukanda huo upo chini sana ikilinganishwa na viwango vya Umoja wa Mataifa (UN).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here