22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

MAFUNDISHO YA YESU NA HOJA YA WANAFUNZI WAJAWAZITO SHULENI

Na Jackson Malugu


NILIFIKIRI wabunge wanapojadili mambo yanayowahusu wananchi, kisha wakatumia mitazamo ya kidini kujenga hoja zao, kwanza wangekuwa wanapata uelewa wa kutosha juu ya muktadha wa kinachoelezwa kuhusu hilo wanalokusudia kulifungamanisha na hiyo mitazamo ya kidini.

Hii ni kwa sababu dini zetu tunazoziamini ndio mwongozo halisi wa maisha yetu ya kila siku. Kwamba wengi wetu tumeweka dini zetu kuwa ndio mwisho wa kuhoji. Maana yake hapa ni kuwa, kwa mfano, mbunge anaposimama kujadili jambo kisha akahitimisha kuwa anachokizungumza ni matakwa ya dini zetu, huyo anataka hoja yake ipite na isipingwe! Ni nadra kusikia waumini wakipinga kile wanachofundishwa au kuhubiriwa na wachungaji au mashekhe wao.

Wanaopinga au kuwa kinyume huonekana kuwa ni waasi. Na uasi katika dini ni jambo baya mno.

Wiki iliyopita wabunge watatu (niliowasikia na kuwaona) waliopata nafasi ya kujadili hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 waliamua kutumia mitazamo ya kidini katika kushawishi kuwa wanafunzi wa kike wanapopata ujauzito wasirejee shuleni kuendelea na masomo. Wabunge hao ni: Salma Kikwete, Mbunge wa kuteuliwa; Ally Kessy, Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM); pamoja na Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Katika mchango wake mbunge Salma pamoja na mambo mengine alisema, “ili kudhibiti ubora wa elimu serikali iboreshe maslahi ya walimu, itilie mkazo elimu ya awali, ifanye ukaguzi wa mara kwa mara kwa walimu na pia haungi mkono kuwarudisha shuleni wanafunzi wa kike wanaopewa ujauzito.”

Alidai kuwa kuwarejesha shuleni wanafunzi hao ili waendelee na masomo yao itakuwa ni kuendekeza hilo suala (kushiriki ngono wakiwa shuleni) wakati linakatazwa na dini zote, mila na desturi zinakataza kupata mimba kabla ya wakati.

Alishauri badala ya wanafunzi hao kurejeshwa shuleni, zitafutwe mbinu nyingine za kuwasaidia.

Kessy, yeye alidai kuwa anapinga vikali wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kurejea shuleni kuendelea na masomo kwa kuwa kwa kuchanganya mapenzi na shule elimu yao inashuka na dini yake ya Uislamu inapinga vikali jambo hilo (kujamiiana kabla ya ndoa).  Alisema kuwa Waislamu wanaounga mkono wanafunzi hao kurejea shuleni wanaunga mkono kuongezeka kwa watoto wa mitaani. Mbunge Kessy alisema kama kuna mbunge yeyote ndani ya Bunge ambaye alianza kushiriki mapenzi akiwa shuleni atoe ushuhuda kama aliweza kuendelea vizuri na masomo.

Mchango wa Mwigulu ndio ulionekana kuwagusa wabunge wengi. Nimeona namna mchango wake ulivyojadiliwa katika mitandao ya kijamii. Inaonekana wengi; wabunge na wachangiaji wa mitandaoni, walikubaliana na hoja za mbunge na waziri huyo ambaye mwaka 2015 alijitosa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM.

Miongoni mwa mengi aliyozungumza, Mwigulu alisema kuwa wao kama wabunge na viongozi wenye wajibu wa kutunga sheria ni lazima walibebe jambo hilo kwa umakini mkubwa ili wasijikute wanatunga sheria zinazopingana. Alidai kuwa wao wenyewe wabunge walitunga sheria inayotambua umri wa kuolewa kuwa ni miaka 18 na kuendelea na mtu akithibika kuwa amebaka anafungwa miaka 30 na kuendelea.

Mwigulu alisema anashangaa kuona wabunge wale wale ambao walikaa bungeni kupitisha sheria hizo, leo kwa kutumia kigezo cha huruma tu wanataka wasichana wanaopata mimba wakishajifungua warudi shuleni kuendelea na masomo. Alikifananisha kitendo hicho ni sawa na kuipa dhambi jina zuri na kisha kuitukuza. Maneno hayo ya mwisho ya Mwigulu yalionekana kuwagusa mno wabunge kiasi cha kumshangilia waziri huyo. Hata katika mitandao maneno hayo ndiyo yaliyopewa nafasi ya kuibua mjadala ambao mwelekeo wake ulikuwa ni kukubaliana na alichokizungumza Mwigulu.

 

Dini ya Kikristo inavyosema

Kwa kuwa Mbunge Salma alisema wazi wazi kuwa dini zote mbili (Ukristo na Uislamu) zinapinga uzinzi na Mwigulu akatumia neno ‘dhambi’ kama neno moja linaloweza kutumiwa kuzungumzia wasichana wanaobeba mimba wakiwa shuleni kwa upande mmoja na wazo la kutaka wanafunzi hao warudi shuleni kuendelea na masomo wakishajifungua kwa upande mwingine, nimeona nishiriki mjadala huu nikitumia mtazamo wa dini ya Kikristo.

Wakati wabunge hawa wakitoa maoni yao bungeni, ni wiki hiyo hiyo mtu mmoja amemuuliza mhubiri maarufu duniani, Billy Graham kuwa ni dhambi gani kubwa ambayo Mungu hawezi kuisamehe?

Mtu huyo amemweleza Graham kuwa ana hofu kubwa kuwa amefika mahali hawezi tena kusamehewa maana amefanya maovu mengi na amewaumiza watu wengi.

Graham, baba mzazi wa Mwinjilisti Franklin Graham, ambaye ndiye ametoa ndege iliyokuja kuwachukua wale watoto watatu walionusurika katika ajali iliyotokea Karatu, mkoani Arusha hivi karibuni na kuwapeleka kwenye matibabu zaidi nchini Marekani, alijibu hivi:

“Kuna dhambi moja tu ambayo Mungu hawezi kuisamehe na hiyo ni dhambi ya kukataa msamaha wake!

Haijalishi sisi ni watu wa namna gani au kitu gani tumefanya, Mungu bado anatupenda na anaahidi kutusamehe kabisa kama tutamgeukia yeye kwa toba na imani.

Je, jambo hili ni gumu kulipokea?

Ndiyo, ni kwa sababu si kwa namna tunavyochukuliana. Kama mtu fulani akituumiza katika mambo madogo au anashindwa kuwa mtu mwema kwetu (kwa mfano), tunakasirika, lakini wakati mwingine tunaweza kuacha tu jambo hilo, au kusamehe. Lakini kama mtu fulani akituumiza au kutudanganya au kutunenea mabaya, tunakuwa na wakati mgumu na inatuwia vigumu kusahau au kumsamehe. Kadri tunavyoumizwa zaidi ndivyo tunavyokuwa wagumu kusamehe.

Lakini Mungu si wa namna ile! Ndiyo, tumemkosea kwa dhambi zetu kwa kweli, tumemuumiza zaidi kuliko ambavyo tunaweza kumuumiza mtu yeyote. Lakini bado Mungu anatupenda na ana shauku ya kuona tunatambua tulichokifanya, kisha turejee kwake kwa toba na imani. Mungu anachukulia kwa umakini mkubwa kusamehewa kwetu dhambi na ndio maana alimtuma Mwanawe ulimwenguni ili afe kwa ajili ya dhambi zetu.

Usiendelee kubeba mzigo wako wa dhambi. Badala yake mgeukie Yesu Kristo na kwa imani mkabidhi mzigo wako.

Ahadi ya Mungu iko kwako: “Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote” (1 Yohana 1:9).

Hayo ndiyo majibu ya mhubiri Graham kuhusu dhambi ambayo aliyatoa kupitia tovuti yake ya www.billygraham.org wiki iliyopita.

Pengine tunaweza kusema, ah! huyu naye si ni binadamu kama sisi. Hebu tumsikilize Yesu katika tukio halisi ambalo ndio msingi wa hoja iliyokuwa bungeni: “Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda hadi mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa anawafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? …Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, akajiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe.” (Yohana 8:1-7).

Ukiendelea kusoma mistari inayofuata katika sura hiyo utakuta kwamba wale watu, wakiwamo wazee, waliondoka mmoja baada ya mwingine hadi akabakia Yesu na yule mwanamke peke yao. Ndipo Yesu alipojiinua asimwone mtu mwingine isipokuwa yule mwanamke, akamwambia: “Wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.” ( mstari wa 10-11).

Ukitafakari majibu ya Graham kuhusu dhambi na ukimsikiliza Yesu alipokutana na kisa cha mwanamke mzinzi ni rahisi kuona mtazamo wa Mwigulu na wabunge wenzake juu ya dhambi ya watoto wetu wanaopata ujauzito wakiwa shuleni na rejea walizokuwa wakifanya kwa kutumia mtazamo wa dini, kuwa ni sawa na giza na nuru.

Majibu ya Graham kuhusu dhambi tafsiri yake ni kwamba, watoto wetu wanapopewa ujauzito haina maana tuwasuse au tuwakatae. Kuwanyima fursa ya kuendelea na masomo ni kuwasusa au kuwakataa. Graham anasema Mungu bado anawapenda, wanayo nafasi ya kutubu dhambi waliyotenda na kuingia mbinguni. Na tukimsikiliza Yesu tunapata ujumbe unaobainisha kuwa kupata ujauzito kabla ya ndoa japokuwa ni kosa mbele za Mungu na jamii ya mahali fulani, kumbe mhusika hastahili kutengwa bali kujengewa mazingira ambayo yatamfanya amsongelee Mungu na kisha atubu dhambi zake. Na kuendelea na masomo inaweza kuwa sehemu ya kumjengea hayo mazingira.

Tumeshuhudia wasichana wakijinyonga baada ya kupata ujauzito wakiwa shuleni na baadaye kutengwa na wazazi au jamaa zao. Tunaona wasichana wakitupa vichanga kwa hofu hiyo hiyo ya kutengwa au kutokuwa na uhakika wa matunzo ya mtoto baada ya kujifungua.

Yesu aliangalia mazingira. Alijua mwanamke yule hakujizini mwenyewe, sasa aliyezini naye mbona hakuletwa mbele yake?

 

Wabunge hawahusiki?

Akina Mwigulu wanasema wanaowapa ujauzito mabinti zetu wanawafunga jela. Sawa, lakini ni kweli kwamba jamii wakiwamo wabunge na viongozi wa kisiasa na serikali hawahusiki kwa namna yoyote na mazingira yanayosababisha mabinti zetu kupata ujauzito wakiwa shuleni? Tunafahamu kuporomoka kwa maadili katika jamii ni miongoni mwa sababu zinazochangia mimba kwa mabinti zetu wakiwa bado wakiwa shuleni. Kama hilo lina ukweli je, viongozi wetu wanaweza kujiweka kando kwamba wao hawahusiki na kuporomoka kwa maadili katika nchi yetu? Je, uendeshaji wa siasa zetu hauna mchango wowote katika kuporomoka kwa maadili ya jamii zetu? Maswali yako mengi mno.

 

Tatizo ni kubwa

Tatizo la mimba kwa wanafunzi ni kubwa na wala haionyeshi kwamba kuwazuia wanafunzi wanaopewa ujauzito kurudi shuleni baada ya kujifungua kunapunguza tatizo hilo. Na ukweli ni kwamba kuwazuia ni kuongeza matatizo zaidi. Hata hoja ya Mbunge Kessy kwamba kuwaruhusu wanafunzi wanapojifungua waendelee na masomo inasababisha ongezeko la watoto wa mitaani ni kinyume cha ukweli kwa kuwa unapomruhusu binti aliyejifungua kuendelea na masomo unamjengea uwezo wa  kumtunza mtoto wake akiishaelimika.

Tangu mwaka 1978 Bunge lilipopitisha sheria inayomnyima haki ya kuendelea na masomo mwanafunzi aliyepata mimba hata baada ya kujifungua, idadi ya wanafunzi wanaopewa ujauzito imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Kifungu cha 35 na kanuni zake za mwaka 1978 cha sheria hiyo, na marekebisho ya mwaka 1995 na 2002, kinaeleza kuwa mtoto wa kike akipata mimba ni ushahidi tosha kwamba amefanya vitendo vya ngono ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na hivyo kustahili kufukuzwa.

Sasa pamoja na sheria hiyo, takwimu za Wizara ya Elimu za mwaka 2013 (wakati huo ikiitwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi) zinaonyesha kuwa wanafunzi wa kike walioacha shule kutokana na ujauzito kwa shule za msingi walikuwa 297 na sekondari ni 3,045. Takwimu hizo ndizo ziliisukuma Serikali kuwa na wazo la kuangalia utaratibu utakaowezesha wanafunzi wanaopewa ujauzito baada ya kujifungua waendelea na masomo kwani elimu ni msingi wa kila kitu. Wazo hilo la serikali lilitokana pia na msukumo wa maombi ya wadau mbalimbali. Sina uhakika kwa mtazamo huo mpya wa ‘kidini’ wa akina Mwigulu na wenzake kama serikali italiendeleza wazo hili ambalo hasa ndilo lenye mtazamo wa kidini.

Utafiti kuhusu mimba shuleni

Ukiacha takwimu hizo za serikali, ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch  iliyopewa jina la ‘Nilikuwa na ndoto za kumaliza shule’ inasema utafiti uliofanywa na shirika hilo mwaka 2016 ulibaini kuwa zaidi ya wasichana 8,000 waliacha masomo baada ya kupata ujauzito au kuolewa kwa nguvu.

Taarifa kutoka vyanzo vingine zinasema mwaka 2009 pekee wasichana 300 mkoani Tanga walikatishwa masomo kutokana na mimba, mwaka 2010 wasichana 880 walikatishwa masomo mkoani Kagera kwa sababu hizo hizo; na mkoani Pwani mwaka huo wa 2010 walikuwa 880.

 

Kuwaruhusu kuendelea na masomo si kubariki uzinzi

Wabunge wanapaswa kutambua kuwa kumruhusu msichana aliyepewa ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua, haina maana kuwa ni kubariki kufanya ngono akiwa shuleni, bali ni kusaidia kumrejesha katika hali ambayo inaweza kumsaidia kuendeleza maisha yake na ya mtoto wake. Shambulio la kisaikolojia analolipata baada ya kupata ujauzito akiwa shule ni adhabu tosha kwake. Kama tunaona ametenda dhambi, ambayo ni kweli, basi tumsaidie kumtengenezea mazingira yatakayomsaidia kuondoka katika dhambi hiyo, badala ya kumsusa jambo ambalo linaweza kumsababishia kuzama zaidi katika dhambi hiyo milele kutokana na kukosa mwelekeo wa maisha kwa sababu ya kukosa elimu. Na kufanya hivyo si kubariki dhambi.

Mwandishi wa makala haya ni mwanahabari mwandamizi, kwa miaka mingi amekuwa Mhariri katika magazeti mbalimbali ya Kikristo. Ni mmliki wa tovuti ya habari za Kikristo ya mwanzonews.com simu 0784942443/0754649941.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles