30 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Mafanikio Serikali awamu ya tano

Elizabeth Hombo -Dar eS Salaam

RAIS Dk. John Magufuli ameeleza namna Serikali yake ilivyofanikiwa kutimiza malengo na matarajio ambayo aliyatoa wakati akizindua Bunge Novemba,2015.

Rais Dk. Magufuli, alieleza mafanikio hayo jana bungeni jijini Dodoma, wakati akifunga Bunge la 11 kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kutoa fursa mchakato wa uchaguzi mkuu kuanza.

“Wakati nazindua Bunge nilieleza malengo na matarajio ya serikali ya awamu ya tano, nafarijika leo (jana) kwa sababu mengi yametekelezeka, kama ambavyo mawaziri waliwasilisha bajeti zao.

“Kwa ujumla naweza kusema tumeweza kutimiza wajibu wetu wa kuwatumikia Watanzania kwa kiasi kikubwa. Nawashukuru wabunge kwa kuishauri Serikali na kuisimamia utekelezaji wa maendeleo. Pia nawashukuru madiwani kwa kusimamia maendeleo katika maeneo yao,”alisema.

Alisema miongoni mwa ahadi kubwa ilikuwa, kudumisha umoja, amani, muungano na kwa kiasi kikubwa mambo hayo yamefanikiwa kwa Watanzania kuendelea kubaki kuwa wamoja bila kujali itikadi zao.

“Pia muungano wetu pia umeendelea kuimarika, tumeweza kushughulikia kero za muungano na kufikia mafanikio na makubaliano, ikiwemo kuhusu gharama za kushusha mizigo na malimbikizo ya kodi na kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya malimbikizo ya kodi Sh bilioni 22.9 ambayo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ilikuwa ikidaiwa na Tanesco.

“Pia tumefanikiwa kulinda mapinduzi matukufu ya Zanzibar. kuhusu ulinzi, amani na usalama nchi yetu imendelea kuwa kisiwa cha amani na mipaka yake imabaki salama.

“Wakati tunaingia madarakani kulikuwa na wimbi la uhalifu wa kutumia silaha kule Kibiti pamoja vitendo vingine vya uhalifu, ikiwamo matukio ya mauaji Kibiti na Rufiji kutokana na kazi kubwa ilivyofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama vitendo hivyo vilikomeshwa na nchi yetu kwa sasa iko salama,”alisema.

Alisema katika kuthibitisha kuna amani hapa nchini, Tanzania imekuwa ya kwanza kwa utulivu na amani  ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) huku ikishika nafasi ya saba kwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 “Ripoti ya Global Peace Index 2020, imeitaja Tanzania kushika nafasi ya kwanza kwa amani na utulivu eneo la Afrika Mashariki na nafasi ya saba kwa nchi zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa niaba ya Watanzania wote navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa,”alisema Rais Magufuli.

WATUMISHI 32,555

Rais Magufuli alisema katika kuimarisha maadili na nidhamu na utendaji kazi serikalini, watumishi wazembe walioshindwa kufanya kazi kwa weledi walichukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwamo kuwatumbua au kuwashusha vyeo na mishahara au kupewa onyo kali.

Alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo,watumishi 32,555 walichukuliwa hatua mbalimbali wakiwemo 15,508 ambao walikutwa na vyeti feki, ajira hewa 19,708 zilizokuwa zinaigharimu Sh bil 19.8 kila mwezi.

Alisema hatua hiyo, ilitoa fursa ya kuwaajiri watumishi wapya wenye sifa 74,173, waliwapandisha vyeo watumishi 106,917 na kulipa madeni ya mishahara na yasiyo ya mishahara Sh bilioni 472.6.

Alisema madeni hayo ya mishahara ilikuwa ni Sh bilioni 114.5 na yasiyo mishahara ni Sh bilioni 358.1.

“Tulifanya haya kwa lengo la kulinda heshima ya wafanyakazi na kuleta nidhamu kwenye utumishi wa umma. Sambasamba na kuimarisha nidhamu, tulizidisha mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu uchumi na ufisadi.

“Mtakumbuka wakati nikizindua Bunge, niliahidi kuanzisha Mahakama ya Uhujumu Uchumi ambapo ilianzishwa mwaka 2016 na mpaka sasa mashauri 407 na 385 tayari yamesikilizwa.

Alisema  katika kupambana na rushwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), imeweza kufungua mashauri 2,256, ambapo mashauri 1,926 tayari yametolewa uamuzi.

“ Serikali imepata ushindi kwenye mashauri 1,013, Takukuru imeokoa Sh bilioni 273.38 zikiwemo fedha zilizokuwa zimedhulumiwa wakulima Sh milioni 899,”alisema.

Aliipongeza Mamalaka ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za Kulevya kwa kuvunja mtandao wa biashara hiyo haramu.

 “Tani 97.99 za bangi, tani 85.84 za mirungi, kilo 567.96 za heroine, kilo 23.383 za cocaine zimekamatwa pamoja na watuhumiwa 37,104 wamekamatwa, hatua hizi ndizo zilifanya Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha masuala ya dawa za kulevya na uhalifu kuipongeza nchi yetu kwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa asilimia 90,”alisema.

MAPATO YAONGEZEKA

Rais Magufuli pia, alisema wakati anazindua Bunge alieleza kutoridhishwa na ukusanyaji wa mapato, baada ya kubana mianya mbalimbali ya kodi, ukusanyaji kodi ulipanda kutoka Sh bilioni 850 hadi Sh trilioni 1.3 hivi sasa.

“Desemba mwaka 2019, TRA ilikusanya Sh trilioni 1.987, kiwango ambacho ni cha juu kuwahi kukusanywa kwa historia ya nchi yetu. Mapato ya yasiyo na kikodi nayo yameongezeka kutoka Sh bilioni 688.7 hadi Sh trilioni 2.4.

Alisema mapato ya ndani ya Halmashauri nayo yameongezeka kutoka Sh bilioni 402.66 hadi Sh bilioni 661.

“Tumeunganisha pia mifuko yua hifadhi ya jamii, lengo ni kupunguza gharama za uendeshaji, mabadiliko yalifanyika baada ya baraka ya bunge hili,”alisema.

ELIMU

Kuhusu elimu, Rais Magufuli alisema wamepanua wigo kwa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo mpaka sasa imetumika Sh trilioni 1.01.

“Tumeongeza idadi ya shule za msingi 16,899 hadi 17,804, shule za sekondari 4,708 hadi 5,330, tumekarabati shule kongwe za sekondari 77 kati ya shule 89, tumejenga mabweni 253 na nyumba 227 za maabara, tumetoa vifaa vya maabara 2,956 na tumepunguza kiasi kikubwa cha uhaba wa madawati kutoka milioni 3.24 hadi milioni 8.95

“Tumekarabati vyuo vya walimu 18, tumejenga upya vyuo vipya tumetoa kompyuta kwenye vyuo vyote 35 vya ualimu lengo ni kuimarisha ufundishaji wa Tehama

“Tumeongeza vyuo vya Veta kutoka 672 hadi 712,  tumekarabati vifaa na miundombinu vya kufundishia 54 vyuo ya maendeleo ya wananchi.

“Tumeongeza pia bajeti ya elimu ya juu Sh bilioni 348.7 hadi Sh bilioni 450. kutokana na hatua hizo uandkishaji wa darasa la kwanza umeongezeka kutoka milioni moja hadi milioni 1.6 hivi sasa. Idadi wanafunzi kidato cha kwanza hadi nne pia imeongezeka kutoka milioni 1.648 hadi milioni 2.185.

“Idadi ya wanafunzi wa Veta nayo imeongezeka kutoka 117000 hadi 226767, vyuo vya maendeleo ya wananchi imeongezeka 69,300 hadi 9,736, idiadi ya wananfunzi wa vyuo vikuu wanaojiunga na mwaka wa kwanza imeongezeka kutoka 65,000 hadi 87,813, wenye kupata mikopo nao wameongezeka kutoka 98,300 hadi 130,000. Kwa taarifa hii nitakuwa sijakosea nikisema kazi kubwa imefanyika sekta ya elimu,”alisema.

AFYA

Kwa upande huduma za afya, Rais Magufuli alisema wamefanikiwa kujenga vituo vya afya 1,769 zikiwemo zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali za mikoa 10.

Alisema miongoni mwa hospitali hizo za mikoa ni pamoja na Mkoa wa Mara ambayo ni Mwalimu Julius Nyerere Memorial ambayo ujenzi wake ulikwama tangu mwaka 1970.

“Pia tumejenga hospitali za rufaa za kanda tatu, tumeajiri watumishi wapya 14,479,  madaktari 1,000 walioajiriwa hivi karibuni, hii imeongeza idadi ya watumishi wa afya kutoka watumishi 8,6152 hadi 163,100.

“Tumeimarisha pia vifaa tiba dawa ambao bajeti kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi bilioni 270 hivi sasa, tumenunua na kusambara magari ya kubebea wagonjwa 117

“Vilevile tumefanikisha kusomesha madaktari bingwa 301 ambapo wamewezesha kuimarisha matibabu ya kibingwa ya moyo, masikio, kansa, bongo.

“Kutokana na hatua hizo idai ya kina mama wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kutoka asmili 64 haid 83 hivi sasa, vifo vya watoto wachanga imepungua sana kutoka wastani wa vifo 25 hadi saba kwa kila vizazi hai 1,000, idadi ya rufaa kwenda nje ya nchi nayo imepungua kwa asilimia 95,wagonjwa kutoka mataifa jirani wamekuja kutibiwa nchini,”alisema.

MAJI

Kuhusu maji, alisema wametekeleza miradi ya maji 1423 ambapo miradi 1268 ni ya vijini na 155 ni ya mijini.

“Miongoni mwa miradi hiyo mikubwa ni wa Ziwa Victoria kwenda Nzega, Tabora na Igunga, mradi wa maji wa Arusha pamoja miradi ya kupelekea maji kwenye miji 28 nao unatekelezwa kwa gharama ya Sh trilioni  1.2

“Miradi mingine ya maji ilielezwa vizuri kwenye hotuba ya waziri wa maji na kutokana na mafanikio hayo vijijini maji yameongezeka kwa asilimia 47 hadi asilimia 70.1, mijini nako kumeongezeka kutoka asilimia 74 hadi asilimia 84,”alisema.

MAWASILIANO

Alisema wameimarisha pia huduma za mawasiliano kutoka asilimia 79 hadi kufikia asilimia 94, idadi ya watumiaji wa huduma za simu na data imeongezeka maradufu.

BARABARA

Kuhusu barabara, alisema barabara zenye urefu kwa kilomita 3,500 zimejengwa hivyo kuifanya nchi yetu kuwa na kilomita 13,000 za barabara za lami.

“Kwa mara ya kwanza pia tumejenga barabara za juu na hizi tumeanza kuzijenga Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa magari, tunahakikisha tunaiunganisha mikoa kwa barabara za lami,”alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,348FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles