MAFANIKIO YA MUZIKI 2016 YASIPOTEE 2017

0
901

darasa

MWAKA 2016 umekuwa mwaka wa mafanikio katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya ambapo kwa mara ya kwanza tumeshuhudia wasanii wengi wakitajwa kwenye tuzo kubwa duniani.

Licha ya wasanii kutajwa kwenye tuzo hizo pia wasanii waliokuwa wamepotea kwenye gemu walirudi kwa kasi na kufanya kazi ambazo zimefanya vizuri kiasi.

Naweza kusema Bongo Fleva imeendelea kuimeza tasnia ya filamu ambayo imepata tuzo mbili kubwa za kimataifa kwa mwaka huu kupitia Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Single Mtambalike ‘Richie’.

Lakini kwa upande wa Bongo Fleva baadhi ya wasanii wametwaa tuzo mbalimbali za kimataifa wakiongozwa na Ali Kiba na Diamond Platnumz.

Licha ya mafanikio hayo makubwa ya muziki huo baadhi ya wasanii wamekuwa wakitumia madawa ya kulevya kwa lengo la kupata stimu kwenye shoo jambo ambalo limekuwa likiwashusha.

Mfano mzuri ni Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambaye alitumbukia tena kwenye dimbwi la utumiaji wa madawa hayo baada ya kupata msaada kutoka kwa Rais Msataafu, Dk. Jakaya Kikwete, kumpeleka katika Hospitali ya Mwananyamala ili kupata matibabu licha ya kuwepo tetesi za kuacha kutumia kabisa kwa sasa.

Pia marapa David Genzi maarufu Young D mwaka huu aliingia kwenye hesabu za wasanii wanaotumia madawa ya kulevya jambo lililomfanya ashuke kimuziki.

Hivi karibuni Young D aliwaomba msamaha mashabiki wake ambapo alieleza kuwa amepitia katika kipindi kigumu na kwamba kuna mambo mengi ameyafanya ambayo hajivunii na anajutia hivyo kuahidi kubadilika na kuwa mfano mzuri kwa jamii.

Ushauri wangu kwa wasanii wote nchini bila kujali ni wa muziki au filamu ni kwamba muda wa kufanya masihara kwenye sanaa umekwisha na sasa ni wakati wa kutulia na kufanya kazi kwa weledi mkubwa.

Na kwa bahati nzuri sanaa imerasimishwa baada ya Rais Dk. John Magufuli kuunganisha katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hivyo basi wasanii hawana budi kutumia nafasi hiyo vizuri mwaka ujao.

Naamini mwaka 2017 hautakuwa mwaka wa Basata kuendelea kufungia nyimbo kama ilivyokuwa kwa mwaka huu ambapo baadhi ya wasanii walifungiwa video zao kutokana na kwenda kinyume cha maadili ya Mtanzania.

Bila shaka sasa wasanii watazingatia maadili katika kazi zao ili kuepuka vikwazo ambavyo kwa namna moja au nyingine hushusha tasnia.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here