29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

MAENDELEO MAKUBWA YA MAURITIUS: Ni ‘muujiza’ wa kuigwa na nchi nyingi Barani Afrika

HILAL K SUED

HABARI za namna gani nchi ndogo ya kisiwa cha Mauritius kilivyoweza kupingana na tabiri hasi kadhaa kuhusu hali yake ya baadaye imewekwa vizuri.

Miaka michache kabla ya kupata uhuru wake mwaka 1968 James Meade, mtaalamu mmoja wa uchumi aliyewahi kushinda Tuzo ya Nobel katika fani hiyo aliandika kwamba kisiwa hicho katu kisingeweza kuendelea chenyewe.

Na miaka michache baada ya uhuru mtunzi mwingine wa vitabu, V. S. Naipaul alikifananisha kisiwa hicho kama “barracoom” – yaani kisiwa kidogo ambamo watumwa weusi hufungiwa kwa muda mfupi.

Lakini nchi hiyo imewasuta watu hawa na wengine wengi na kuwa nchi ambayo inasifika zaidi kuliko zote barani Afrika katika maendeleo katika kipindi cha nusu karne iliyopita. Kila mara nchi hiyo hujikita katika ngazi za juu katika orodha za nchi za Afrika katika masuala mbali mbali – ya uhuru wa kisiasa, utawala wa sheria na maendeleo ya watu wake (human development).

Kimaendeleo na kisiasa Mauritius imeziacha kwa mbali nchi nyingine za visiwa katika eneo hilo la Bahari la Hindi na ambazo zilijikomboa kutoka kwa wakoloni takribani wakati mmoja – kama vile Comoro, Madagascar, Seychelles na hata Zanzibar, nchi huru iliyoamua kujiunga na Tanganyika (Tanzania Bara) mara tu baada ya kujikomboa.

Ulinganisho na Zanzibar

Kuna wadadisi wanalinganisha hapa baina ya Mauritius na Zanzibar. Wanasema Mauritius

kina karibu idadi sawa ya wakazi kama Zanzibar (takriban wakazi 1.5 milioni) ilipata uhuru wake miaka minne baada ya mapinduzi ya Zanzibar, yaani mwaka 1968. Na zaidi ya hayo visiwa vyote viwili vilikuwa na wakazi wa asili ya mataifa mbali mbali.

Na visiwa vyote viwili vilikuwa na zao moja kubwa la uchumi, Zanzibar ni karafuu na Mauritius ni miwa. Leo hii ukilinganisha Mauritius na Zanzibar utashangaa jinsi kisiwa hicho kilicho karibu na pwani ya Afrika ya Kusini kilivyopiga hatua kubwa mbele kimaendeleo wakati Zanzibar ikiachwa nyuma kabisa ikiimba wimbo wake ‘Mapinduzi daima.’

Wadadisi wa mambo wanasema maendeleo ya Zanzibar yanakwazwa na siasa za hovyo hovyo, za chuki na za kibaguzi. Inashangaza hadi sasa ‘mapinduzi’ bado ndiyo mbiu kuu ya watawala wa Zanzibar kwa kuwakumbushia wananchi kuna watu wanataka kurejesha watawala wa Kiarabu.

Imebadilisha tawala mara saba Kidemokrasia

Nchi ya Mauritius imefanya chaguzi kumi zenye ushindani mkubwa na kuweza kubadilisha tawala mara saba kwa amani kabisa. Na siku zote imekuwa inatazamwa kama mfano mzuri wa uvumilivu na utulivu katika uwanja wa siasa na hapo hapo kuonesha umoja wa kitaifa pamoja na kuwa na wakazi wa asili ya mataifa na dini mbalimbali kama vile Wahindu, Waislamu, Waafrika, watu kutoka visiwa vya East Indies, Wafaransa na jamii za Wachina ambao wote wamekuwa wakiishi kwa amani na utulivu mkubwa.

Mwaka 2011, mafanikio mbalimbali ya Mauritius yalimsababisha Joseph Stiglitz, mshindi wa Tuzo ya Nobel katika Fasihi (Literature) kuiita nchi hiyo kama Muujiza wa Mauritius – “Mauritius Miracle.”

Stiglitz aliweza hata kutoa wito kwa Marekani na mataifa mengine makubwa yaliyoendelea kuiga mfano wa nchi hiyo na kujifunza kutoka kwake kuhusu masuala kama elimu bure, huduma za afya na uingiliano mpana wa jamii (social interaction).

Hatua kubwa za maendeleo kiuchumi

Na nchi hiyo inapojiandaa kusherehekea miaka 50 ya Uhuru ifikapo Machi 12, serikali ya sasa nayo imejiandaa vyema kujipanga katika kushikilia sifa zinazomiminiwa nchi hiyo na kuzidisha pale nchi ilipofikia kimaendeleo.

Utawala wa umoja wa vyama kadhaa unaoongozwa na Waziri Mkuu Pravind Jugnauth umesema unataka Mauritius ipige hatua kutoka nchi yenye uchumi wa kipato cha tabaka la juu-kati (upper-middle-income) na kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha juu (high-income) katika miaka ijayo. 

Kwa mtu yoyote wa nje, lengo hili ndilo hasa linahitajika kwa nchi hiyo. Lakini inavyojitayarisha kuingia katika muongo wake wa tano tangu uhuru, Mauritius itajikuta inalazimika kutafuta njia mpya za kupata fikra mpya ili iweze kuendelea na kasi iliyonayo – kiuchumui na kisiasa kuliko kujikuta inaingia katika mgogoro mkubwa wa uchumi wa kati.

Ukuaji kiuchumi wa nchi hiyo katika miaka mitano iliyopita ulikuwa wa wastani wa asilimia 3 hadi 4. Benki kuu ya Mauritius unatabiri ukuaji wa asilimia 4.2 kwa mwaka huu 2018.

Nchi nyingi nyingine katika bara hili zinaweza kuwa na wivu kwa mafanikio haya, ingawa wachumi wanasema mafanikio yenyewe ni udororaji ukilinganisha na ukuaji wa uchumi katika miaka ya 80 na 90 wakati uchumi ulikua sana kutokana na mbeleko ya sekta ya sukari, utalii, uzalishaji wa bidhaa za nguo na huduma za kifedha.

Tumaini kubwa kwa serikali ya sasa ni kwamba mbeleko ingine inatarajiwa kuwa ni uchumi wa baharini. Hapa kunatajwa shughuli kama vile uvuvi, uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, utalii wa baharini na uzalishaji wa nishati kutumia mafuta na gesi asilia ndivyo vitu vitakavyotoa chachu ya maendeleo kwa miaka kadha ijayo.

Janii za asili mbalimbali zaishi kwa utulivu

Katika ulingo wa siasa na jamii, Mauritius inasifiwa sana jinsi ilivyoweza kuwafanya watu wa jamii na asili mbali mbali kuishi pamoja kwa kushirikiana.

Huenda mafanikio haya yanatokana na sababu kwamba nchi hiyo ya kisiwa haina wakazi wake wa asili (indigenous population) kikilinganishwa na visiwa vingine. Yaani hakuna jamii moja inayoweza kuweka madai kwamba wao ndiyo wenye haki zaidi ya umiliki wa kisiwa hicho kuliko jamii zingine.

Sababu nyingine ni wingi wa wakazi katika eneo dogo – wakazi 1.3 milioni wamebanana ndani ya eneo la kilomita 2,040 za mraba na hivyo kuwalazimisha waishi kwa maelewano.

Lakini pia kuna suala la siasa ambalo halizungumzwi sana kuhusu mgawanyo wa mamlaka ya kisiasa. Kwa mfano Wamauritius  wa asili ya Ufaransa na China hawajishughulishi katika kupata madaraka ya kisiasa, wakiwaachia zaidi Wahindu, Waislamu na Waafrika wenye mchanganyiko wa watu kutoka Visiwa vya East Indies.

Hali hii huwa inaepusha mivutano na ushindani kwa sababu siasa nchini humo zaidi zinatawaliwa na wakazi wa tabaka la kati wa jamii ya Wahindu, jamii ambayo ina wakazi zaidi kidogo ya nusu ya wakazi wote kisiwani humo.

Kwa upande mwingine, ingawa kumekuwapo ubadilishaji wa tawala mara saba, ngazi za juu kabisa za siasa za Mauritius zimekuwa zikimilikiwa na takribani watu wale wale.  Miaka 48 kati ya 50 ya Uhuru wa Mauritius imeongozwa na ama Seewoosagur Ramgoolam au Anerood Jugnauth au watoto wao Navin and Pravind.

Pamoja na kwamba hali hii imetokea katikati ya maendeleo makubwa ya kiuchumi na uvumilivu mkubwa uliopo katika medani ya siasa, kuna dalili kwamba watu wa Mauritius wameanza kuchoka hali ya kuongozwa na watu wa familia mbili tu.

Januari 2017 Anerood Jugnauth alirithisha madaraka ya uwaziri mkuu kwa mtoto wake bila ya ridhaa ya wapiga kura. Ikitambua kwamba hatua hii ilizidisha hali ya kuchukiwa kwa serikali ya pamoja hasa katika masuala ya ufisadi na uswahiba (cronyism) chama kikuu katika umoja huo Mouvement Socialiste Militant (MSM), kiliamua kutoshiriki uchaguzi mdogo ulioitishwa hivi karibuni.

Pamoja na tofauti zao nyingi za kisiasa kuna suala moja linalowaunganisha wananchi wote wa Mauritius – suala la Visiwa vya Chagos.

Visiwa hivi vilikuwa sehemu ya Mauritius tangu 1814. Lakini miaka michache kabla ya Mauritius kupata uhuru wake kutoka Uingereza, visiwa hivyo vilimegwa na kuwa sehemu ya ardhi chini ya himaya ya Uingereza – British Indian Ocean Territory (BIOT).

Na baadaye Uingereza iliikodisha kisiwa kimoja – cha Diego Garcia – kisiwa kikubwa miongoni mwa Visiwa hivyo kwa Marekani ambayo ilikifanya kuwa kituo kikuu cha kijeshi katika Bahari ya Hindi. Katika kufanikisha azma hiyo wakazi wapatao 1,500 wa Diego Garcia walihamishwa kwa nguvu na kuachwa katika bandari ya Port Louis – Mji Mkuu wa Mauritius na wengine kupelekwa Visiwa vya Shelisheli (Seychelles).

Suala hilo lilizua mzozo mkubwa baina ya Uingereza na Mauritius na mwaka huu au ujao Mahakama ya Kimataifa ya Haki (International Court of Justice) inatarajiwa kutoa uamuzi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles