*Ni ndani ya Halmashauri ya Buchosa
*Takukuru yaagizwa kuwasaka wahusika popote walipo
*Watakaobainika kufilisiwa
Na Clara Matimo, Buchosa
Wakati Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikipambana kutafuta fedha ili kuwanufaisha wananchi wake, imebainika kuwa katika Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza zaidi ya Sh bilioni moja imepigwa na wajanja.
Ubadhilifu huo umebainika Juni 23, mwaka huu katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani uliolenga kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 na utekelezaji wake ambapo hoja kubwa iliyojitokeza ni matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa haraka ili kuwabaini watumishi wote ambao wamehusika na ubadhilifu huo hata kama wameondoka ndani ya halmashauri hiyo wasakwe popote walipo ili wajibu hoja na endapo itajulikana pasinashaka hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Mbali na agizo hilo kwa Takukuru pia amemuagiza Katibu Tawala wa mkoa huo, Ngusa Samike, kuunda kikosi maalum wakiwemo wakaguzi wa ndani na wataalamu wa majengo ili wachunguze kwa kina maeneo yote na miradi ambayo inaongoza kwa hoja za CAG ili waangalie thamani halisi ya miradi inayotekelezwa na kubaini fedha hizo zilitumika kufanya nini wakati bajeti iliishaandaliwa kutoka serikali kuu.
“Hoja kubwa iliyojitokeza ni matumizi mabaya ya fedha za umma na ofisi ya manunuzi kuna fedha asilimia 40 kutoka mapato ya ndani ambazo inatakiwa halmashauri izipeleke kusimamia miradi ya wananchi na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi(CCM) zilikuwa zinakatwa na kupelekwa upande wa utawala zirudi kwenye miradi ya maendeleo zikatekeleze miradi iliyokusudiwa.
“Viashiria vya wizi ni vikubwa, Takukuru hakikisheni wote ambao wamehusika na matumizi mabaya ya fedha za umma wanachunguzwa kwa haraka na mchunguze mambo mawili tupate majibu ya fedha zilizopotea na hao watumishi wakati mchakato wa uchunguzi ukiendelea mchunguze mali wanazomiliki ili wakibainika kuhusika na ubadhilifu huo tutawafilisi warudishe fedha hizo za umma,” amesema na kuongeza.
“Tunauwa vibaka barabarani wameiba simu ya tochi wakati tunamamilioni ya fedha yanapotea hata kumfunga mtu ni jibu, kumfilisi mtu ni jibu ni mwizi, vielelezo hamna aturudishie fedha zetu, kuanzia sasa Mtendaji atakayetumia fedha za serikali kinyume na taratibu tutamsimamisha kazi lakini kwa sababu tunazingati utawala wa sheria basi wataalamu wa sheria waendelee kuchakata maeneo hayo,”amesema Mhandisi Gabriel.
Hayo yanajiri ikiwa ni siku chache zimepita tangu Mhandisi Gabriel alipomuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, Ngusa Samike, Mei 30, mwaka huu amuandikie barua CAG, Charles Kichere kwenda mkoani humo kufanya ukaguzi wa kina kutokana na upotevu wa zaidi ya Sh Bilioni 3.15 zinazotolewa na serikali kwa makundi maalum katika Halmashauri ya Jiji hilo.
Aidha, amewashauri madiwani kutokaa kimya wanapoona kuna dalili mbaya katika kutekeleza miradi kwani inatekelezwa kwenye kata zao nao ni wenyeviti wa kamati za maendeleo katika maeneo yao kisheria hivyo wanahaki kujua miradi hiyo, thamani yake, utaratibu uliopangwa na kuangalia utekelezaji wake kama una tija au hauna kwa maslahi mapana ya wananchi, halmashauri, mkoa na taifa.
“Changamoto ipo pia ofisi ya mhandisi, wahandisi mmekuwa mkisimamia majengo ya hapa kwa gharama ya juu sana kulinganisha na maeneo mengine kama Wilaya ya Sengerema wanajenga nyumba ya mtumishi two in one kwa Sh milioni 50 nyumba za familia mbili za watumishi, hapa nyumba ya mtumishi mmoja Sh milioni 65 na zingine hazijakamilika tuna mgogoro ndani.
“Ni fedha nyingi kila mkaguzi akisema leteni ushahidi wa uhalali wa matumizi ya fedha hakuna ndiyo maana hoja zimekuwa za muda mrefu halafu tukiondoka hapa tunazunguka hatujibu hoja mimi nimekuja na timu yangu ya mkoa mwaka huu hakuna hoja ambayo itakosa majibu,” amesema Mhandisi Gabriel.
Mkaguzi Mkuu wa Ndani Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoa wa Mwanza, Abyud Sanga, amesema uongozi wa halmashauri hiyo kutokujibu mapungufu ambayo waliwaelekeza kabla ya uhakiki ikiwemo kuwasilisha vielelezo imesababisha hoja tatu tu kati ya 37 za mwaka wa fedha 2020/2021 zijibiwe huku hoja zote za nyuma kukosa majibu.
“Tuliwaomba tupate nafasi hata kama ni siku ya Jumamosi ili tukae na timu sisi kama RS kuona tatizo ni nini pia tusaidiane kwa kushauri na kusimamia zoezi la kujibu hoja lakini uongozi wa halmashauri haukutoa ushirikiano wa dhati kwa hiyo tukashindwa kuja.
“Kimsingi tunasema mwisho wa kikao hiki cha Baraza ndiyo mwanzo wa vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa, kwa hali hii halmashauri hii itatuletea shida kwenye mkoa kwa maana mkoa ulikuwa na nia ya dhati kabisa kuhakikisha hoja zinapungua,” amesema Sanga.
Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Nje (CAG) Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani, amesema katika halmashauri hiyo jumla ya hoja 55 sawa na asilimia 68 hazijatekelezwa kikamilifu nakwamba ziko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
“Tano sawa na asilimia 18 hazijatekelezwa kabisa na sababu kubwa ya hoja kutokufungwa ni majibu ambayo yanatolewa na Menejimenti kukosa vielelezo na ushahidi wa kutosha pia uongozi kutoweka mikakati thabiti na ya dhati katika kujibu hoja kikamilifu.
“Mimi siji kwenye hii Halmashauri ya Buchosa kutafuta hoja, nakuja kuwahakikishia wananchi kwamba fedha zote ambazo zimekusanywa kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato na zilizotolewa na serikali kuu kuja kwenye halmashauri hii kwa ajili ya kutkeleza miradi ya maendeleo zimetumika vyema, hiyo ni sifa kwa halmashauri, wakaguzi na mkoa wetu,” amesema Shabani.
Nao baadhi ya madiwani waliohudhuri mkutano huo, akiwemo Masumbuko Bupamba, Peter Mbundu, Joshua Kabika na Isack Mashimba wote wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wakizungumza na Mtanzania Digital kwa nyakati tofauti wamesema ili kukomesha tabia za ubadhilifu wa mali za umma kwa watumishi serikali iwachukulie hatua za kinidhamu watakaokutwa na hatia ikiwemo kuwafukuza kazi badala ya kuwahamisha vituo vya kazi.