Madudu tena Hospitali ya Muhimbili

0
629
Profesa Lawrence Museru
Profesa Lawrence Museru
Profesa Lawrence Museru

Na Veronica Romwald – Dar es Salaam

KWA mara nyingine matabibu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wamefanya madudu kwa kutoa taarifa zisizokuwa sahihi za mwenendo wa tiba na kifo cha marehemu Rehema Joseph.

Tukio hili limetokea wakati matukio mengine mawili ya kuchanganya miili ya marehemu yaliyotokea karibuni katika chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari) cha MNH yakiwa hayajafutika vichwani mwa Watanzania.

Tofauti na matukio hayo yaliyowaondoa kazini kwa muda watumishi wawili wa kitengo hicho kupisha uchunguzi, jana ndugu wa marehemu, Rehema Joseph, waliokwenda kuchukua mwili wa ndugu yao kwa ajili ya mazishi waliukuta ukiwa na hali tofauti na jinsi matabibu walivyotoa ripoti ya kifo chake.

Mmoja wa ndugu wa marehemu Rehema aliyezungumza na MTANZANIA Jumamosi (jina lake tunalihifadhi), alisema walielezwa na matabibu kuwa ndugu yao alifariki baada ya kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua lakini walipokwenda kuuchukua mwili kwa ajili ya mazishi walikuta hajafanyiwa upasuaji wala kichanga kilichotolewa tumboni hawakukiona.

“Marehemu ni binamu yangu, alikuwa mjamzito na mimba yake ilikuwa ya miezi minane, lakini kwa mujibu wa madaktari alikuwa na kifafa cha mimba na juzi mumewe alimpeleka hospitalini pale Mbagala Zakheim ambako alipewa rufaa ya kwenda Temeke.

“Alipofikishwa Temeke kwa hali aliyokuwa nayo walimpa rufaa ya kuja Muhimbili. Taarifa hizo mumewe alitueleza usiku ule ule,” alisema.

Alisema asubuhi ya Agosti 31, alifika Muhimbili kumjulia hali ndugu yake lakini alizuiwa na wauguzi kwa maelezo kuwa mgonjwa alikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

“Nikakubaliana nao, akaingia mume wake kwanza mimi nikabaki nje baadaye nikaitwa lakini nikaambiwa niingie kwanza ofisini nikakataa… lakini baadaye nikakubali. Nilipoingia baada ya kupewa maelezo nikagundua kuwa binamu yangu ameshafariki na ameshapelekwa mochwari,” alisema.

Alisema walitakiwa kulipia gharama za matibabu yaliyojumuisha gharama za upasuaji kwa sababu taarifa ya matabibu ilieleza kuwa marehemu alijifungua kwa njia ya upasuaji.

“Nikasema ni sawa lakini wakatueleza tufike kulipa siku inayofuata (jana) kwa sababu mhasibu hakuwepo, walikuwa wanafanya ‘famigation’ kwenye vile vyumba.

“Leo (jana) kulipokucha tukaja… kaka zangu wakawa wanafanya ‘process’ za malipo na baada ya kulipa tukapewa kibali cha kwenda kuchukua maiti. Tulipokwenda mochwari nikawaomba nimkague ndugu yangu ili kujiridhisha.

“Nikaruhusiwa, nikamfunua na kumshika tumboni nikashangaa kuona hakupasuliwa, hapo nikagundua alijifungua kwa njia ya kawaida na si kwa kupasuliwa kama nilivyoelezwa, nikauliza mwili wa mtoto wake upo wapi. Wale wa mochwari wakanijibu haupo na kwamba waliletewa maiti moja tu.

“Nikawaambia ninavyoelewa na si kwamba nasimuliwa mimba ya marehemu ilikuwa kubwa na wodini matabibu wamesema alifanyiwa upasuaji saa sita usiku kumtenganisha na mtoto wake ila baada ya kutenganishwa mtoto naye alifariki baadaye.

“Nilivyowaeleza hivyo wale watumishi wakawa wakali kidogo na mimi nikabadilika na kuwaambia si wote wanaowahudumia hawajui kila kitu wengine ni waelewa, nimeshapewa ripoti na mdogo wangu alikuwa mjamzito,” alisema.

Alisema aliwaita kaka zake kuwaambia alichobaini baada ya kumkagua marehemu na kwa pamoja waliamua kulifikisha suala hilo utawala lakini kabla hawajachukua hatua hiyo waliitwa na matabibu ambao waliuchukua mwili wa marehemu na kuuchana tumboni.

“Nikawaambia kaka zangu kuwa maiti tumepewa lakini hakuna mtoto, ndipo wale wahudumu wakatuita na kumchukua marehemu wakamlaza na kumchana tumboni wakatuambia hakuna mtoto, wakatuonesha na kutuambia angalieni kulivyovimba, mimi  nikawajibu hiyo ni uterus na huwa inavimba baada ya kutoka mtoto.

“Tukawaacha tukaenda kuonana na Mkurugenzi, akaitwa daktari aliyemhudumia ndugu yetu, bahati nzuri daktari yule alieleza ukweli kuwa marehemu alifikishwa akiwa mjamzito hapo tukapata faraja kwamba sasa tutapata maiti yetu maana tulishaleta gari na tayari tulikuwa tumeandaa makaburi mawili ya kuzikia.

Wakati huo katika wodi ya Mwaisela ambako marehemu alifikishwa nao walikiri kumpokea lakini mochwari bado walikataa kupokea mwili wa mtoto.

“Tunamshukuru Mkurugenzi maana aliita timu yote iliyomhudumia marehemu na hatimaye ukweli ukawekwa wazi na tukapata maiti zetu zote mbili, tunashauri wawe makini zaidi hasa huku mochwari maana walichokuwa wamekifanya sikukipenda kabisa,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Museru, alipoulizwa alikiri tukio hilo kutokea.

“Ni kweli tumepatwa na changamoto hiyo lakini katika hili tunaona tatizo lipo pande mbili. Muhimbili huwa tunampatia taarifa yule aliyemfikisha ndugu na kuandikisha, sasa sijajua yule muuguzi aliyetoa hizo taarifa kwanini alisema amepasuliwa wakati hakupasuliwa.

“Lakini kiukweli yule dada aliletwa akiwa katika hali mbaya na kwa bahati mbaya pale katika wodi ya wazazi hatuna ICU sasa alipoonekana ana hali ile madaktari ilibidi wamhamishie huku ICU chumba namba moja na wakamwekea mashine ya kumsaidia kupumua.

“Daktari alimpa dawa ya kumwongezea uchungu ili aweze kujifungua na hilo lilifanikiwa, saa sita usiku alijifungua lakini kwa bahati mbaya akafariki saa chache baada ya kijifungua, alikuwa na kifafa cha mimba kwa hiyo mwili wake ulipelekwa mochwari. Mtoto alizaliwa alipelekwa wodi namba 36 ya watoto njiti lakini naye baadaye kidogo alifariki wakaandikisha jina la mama yake na wakamwekea lebo ndipo ukapelekwa mochwari.

“Sasa yule ndugu naona alijua angekuta mwili wa marehemu na mtoto kwa sababu walikuwa wodi moja hapo ndipo ulipotokea mkanganyiko,” alisema.

Alisema ili kuepuka tena kutokea kwa mkanganyiko wa aina hiyo, Muhimbili imepanga kujenga chumba cha ICU katika wodi ya wazazi.

“Tayari tumepata mzabuni na tunatarajia kuwa baada ya miezi miwili hivi tutakuwa tumekamilisha ujenzi na hivyo kuachana na adha hii,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here