Madiwani wapewa maagizo ya madarasa

Na AMINA OMARI, MUHEZA
 
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Bakari Mhando, ametoa siku 90 kwa madiwani wa halmashauri hiyo, kuhakikisha wanaandaa mpango wa kutatua tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa wilaya ni humo.
 
Mhando alitoa agizo hilo jana wakati wa kikao cha baraza la madiwani. Katika maelezo yake, mwenyekiti huyo wa halmashauri alisema baada ya kipindi hicho, madiwani wote watatakiwa kueleza idadi kamili ya vyumba vya madarasa walivyojenga na vyumba ambavyo havijajengwa.
 
Katika utekelezaji wa agizo hilo, aliwashauri madiwani hao kushirikiana na wananchi kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kutekeleza agizo hilo kwa haraka.
 
“Tunajua shule zetu nyingi majengo yake yamechakaa na yanahitaji ukarabati. Kwa hiyo madiwani msitegemee Serikali iwakarabatie majengo au iwajengee kwa sababu ina majukumu mengi,” alisema Mhando.
 
Katika hatua nyingine, aliwataka watendaji wabuni vyanzo vya kudumu vya mapato ili halmashauri yao iweze kujiendesha yenyewe kwa kuwa hadi sasa inajiendesha kwa asilimia nne.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Luiza Mlelwa, alisema uwepo wa vyanzo vya uhakika vya mapato ndiyo suluhisho la halmashauri hiyo kujiendesha yenyewe.
 
“Kuitegemea Serikali Kuu kutatucheleweshea maendeleo yetu. Kwa hiyo, hatuna budi kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani ili yatuwezeshe kutekeleza miradi yetu,” alisema Mlelwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here