Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto amewataka madiwani kushirikiana na wenyeviti wa serikali za mitaa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi ili jiji hilo liendelee kukua kwa kasi.
Akizungumza leo Machi 6 wakati wa zoezi la usafi katika Mtaa wa Kivule na Soko la Kivule amesema baadhi ya miradi ya maendeleo imekuwa ikikwamishwa kwa sababu ya chuki za kisiasa.
“Ninaloliona sasa hivi kwenye jiji letu baadhi ya wenyeviti na madiwani hawashirikiani, tutakapoona hamuelewani na kuna miradi mimi naingilia kati. Sitakuwa meya wa kukaa ofisini kupigwa kiyoyozi na kula korosho nitakuwa ‘site’ kutatua kero za wananchi.
“Kwa muda wa miaka mitano hatotokea mtu wa kumpinga Magufuli katika maendeleo, mimi nitaingilia kati,” amesema Kumbilamoto.
Meya huyo amewataka wafanyabiashara wote kulitumia soko hilo badala ya kwenda kando ya barabara ili wajikwamue kiuchumi.
“Nitakutana na ofisa biashara na mkuu wa wilaya tuone tutatumia njia gani kuwavuta wafanyabiashara kuja hapa (sokoni) pasipo kutumia nguvu. Kitendo cha kukaa barabarani hakileti nguvu na ikiwa mnapakimbia hapa maana yake mnayakimbia maendeleo,” amesema Kumbilamoto.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Soko la Kivule, Kassim Ndogoro, amesema lilianzishwa mwaka 2000 lakini halijafanya kazi kama ilivyokusudiwa kwa sababu ya mivutano ya kisiasa iliyokuwepo awali.
“Kuna hujuma nyingi watu hawaingii sokoni wanafanya biashara barabarani na wengine wanatengeneza fitina za kuzuia watu wasiingie sokoni. Tunaomba watu waje hakuna anayemiliki kizimba na hili soko halijai ni kubwa sana,” amesema Ndogoro.
Wafanyabiashara hao pia wamemuomba meya huyo kuwasaidia kuchimba kisima na kuhakikisha daladala zote zinaishia sokoni hapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule, Amos Hangaya, amemuomba meya huyo kuupa kipaumbele Mtaa wa Kivule katika awamu ijayo ya Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ili barabara za mitaa ziweze kuwekwa lami na taa.
Meya huyo amekubali kuwa mlezi wa Kata ya Kivule na kuahidi kufanya ziara hivi karibuni kukagua ujenzi wa miundombinu sambamba na kuleta greda kusafisha eneo la soko na kutafuta wadau kuchimba kisima sokoni hapo.