Na MWANDISHI WETU
-MOSHI
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi limesema litafanyia kazi tuhuma za ukiukwaji wa taratibu katika mradi wa ukarabati wa Kituo cha Afya cha Pasua unaotajwa kusababisha upotevu wa fedha .
Kauli hiyo ilitolewa jana na Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya wakati wa ziara ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwenye Kituo cha Afya cha Pasua kujionea ukarabati unavyoendelea.
“Kuna matatizo na hayo matatizo nimesema nije kwanza kuangalia kwa kuwa bado hili suala liko kwenye vikao vya ndani tutatoa taarifa yakikamilika kwenye vikao kwanza.
“Ni kwamba kuna taratibu hazijakaa vizuri kwenye mchakato mzima wa ukarabati wa kituo cha afya,” alisema Meya Mboya .
Alisema fedha zilizotumika katika ukarabati wa kituo hicho ni fedha za serikali zinazotokana na kodi inayokusanywa kutoka kwa wananchi.
“Zinapotumika ni lazima baraza la madiwani kufuatilia na kujiridhisha kama zimetumika kwa utaratibu uliokusudiwa.
“Hizi fedha ni kodi zetu ambazo wakati mwingine zinaitwa fedha za serikali sasa zinapotumika hapa ni lazima tuhakikishe zinatumika kwa utaratibu uliokusudiwa na kwa utaratbu ambao hautaleta shaka wala tatizo kwa hiyo tusubiri mchakato na taratibu za vikao zitakapokamilika tutawajulisheni,” alisema Mboya
Mboya alisema hakuna mradi unaofanyika mahali popote bila kupitishwa katika vikao halali vya baraza la madiwani na hadi kuanza ukarabati kwa kituo hicho taratibu zilifuatwa.
“Tangu mwaka 2013 tulikuwa tunatenga fedha kwenye bajeti ya ujenzi wa vituo vya afya kikiwamo Kituo cha Afya cha Pasua na ilikua ni sehemu ya upasuaji, wodi ya kujifungulia kina mama, chumba cha mionzi ya X-ray na chumba cha kuhifadhi maiti,” alisema Mboya .
Diwani wa Kata ya Pasua, Juma Raibu alisema ukarabati wa vituo vya afya ni mpngo mkakati wa taifa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na kupunguza changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta ya afya nchini.
“Mimi kama diwani nilipewa maelekezo kwa barua kwamba niunde kamati mbalimbali za kuweza kusaidia ukarabati wa kituo hiki uweze kuendelea.
“Kamati ya kwanza niliambiwa niunde ya ununuzi, kamati ya mapokezi na kamati ya ujenzi wazawa wa eneo hili wawe sehemu ya wasiamamizi wa mradi huu,”alisema Raibu.
Katika ziara hiyo, MTANZANIA ilishuhudia wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwa wamoja katika kukagua maeneo mbalimbali ya kituo hicho .