26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Madiwani Kalambo kuwafukuza kazi watendaji

Na MWANDISHI WETU-KALAMBO

MWENYEKITI wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Daudi Sichone ametangaza kuwafukuza kazi pamoja na kuwapeleka mahakamani watendaji wa vijiji wanaokusanya mapato na kutoyawasilisha benki kwa utekelezaji wa matumizi mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki mjini hapa.

Sichone alisema kuwa tabia hiyo ilianza kwa watendaji wachache kutumia fedha wanazokusanya hali iliyosababisha na watendaji wengine kuiga tabia hiyo na matokeo yake kuwa desturi kutumia fedha za makusanyo huku ikisomeka kuwa ni wadaiwa.

Alisema jambo hilo halikubaliki na kwamba watendaji hao sio wadaiwa bali ni wezi wa fedha za halmashauri na hivyo wachukuliwe hatua kama wezi.

“Imekuwa shida, kuna watendaji ambao sasa hivi wanaona kuwa Takukuru nako ni kama nyumbani, na sisi njia nyingine ambayo tunayo, nguvu yetu tuliyonayo ni ya kuwafukuza tu na kuwapeleka mahakamani, kwa sababu hatuna namna, tumewapeleka kwenye vyombo ambavyo ndio tunavitegemea, vimefanya kazi yake kwa nguvu zote, tumekwenda hivyo lakini bado,” alisema Sichone.

Aliongeza kuwa kuna baadhi ya watendaji wadaiwa ambao wameshajiandikisha ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kalambo ili ifikapo Mei 30, mwaka huu wawe wamemaliza kulipa fedha hizo na kushauri kuwa wasisubiriwe hadi ifike tarehe hiyo.

“Kuna watendaji ambao madeni yao ni makubwa na hivyo hawataweza kulipa fedha hizo kwa pamoja na kuitaka ofisi hiyo kuweka utaratibu wa watendaji hao kulipa kidogo kidogo,” alisema Sichone. 

Awali akichangia hoja ya kuchukuliwa hatua za kufukuzwa watendaji hao, Diwani wa Kata ya Mambwenkoswe, Edwin Msipi (CCM), alisema kuwa halmashauri hivi sasa inasota kutokana na fedha nyingi kuwemo katika mifuko ya watendaji na hivyo kusababisha miradi mingi kushindwa kutekelezeka na hivyo kulitaka baraza hilo kuwa na mkakati wa kuwashughulikia.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, alisema kuwa jukumu la kwanza la madiwani ni kusimamia ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na kuongeza kuwa hao wadaiwa ni wa kwao na wapo ndani ya uwezo wao na kuwathibitishia kuwa endapo watahitaji msaada wa Serikali, ofisi yake na ofisi ya mkuu wa wilaya zipo tayari kusaidia.

“Kwahiyo tunataka kwa mkoa mzima milioni 450/- ziwe zimeshakusanywa na kulipwa waheshimiwa madiwani, kufikia mwisho wa mwezi huu, kwahiyo ni lazima tupambane kufa na kupona na hawa ‘defaulters’, sio tu kuwafunga, lakini kwanza wairudishe hiyo hela ili tupate hela ya kuwalipa madiwani, halafu hatua nyingine itafuata hiyo ya kisheria, wengine wameanza wizi wa reja reja baadae utakuwa wizi wa kudumu, sasa ili kuwakomesha hawa ni lazima tuanze kufunga wawili watatu kama ninyi wenyewe mlivyopendekeza hapa,” alisema Wangabo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles