30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Madiwani Igunga wamkataa Ofisa Utumishi, Mweka hazina

Na Allan Vicent, Igunga

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora na wabunge wawili wa jimbo la Manonga na Igunga wilayani humo wamemwomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu kuwaondoa Mweka Hazina Hassani Kisenge na Ofisa Utumishi, Alice Erio kwa kushindwa kusimamia mapato na kutowapa ushirikiano madiwani.

Madiwani hao wametoa maombi hayo juzi katika kikao kilichohudhuriwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Katibu Tawala, Wabunge wawili, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Wakuu wa Idara na madiwani wa kata zote 35 za halmashauri hiyo.

Akitoa taarifa kwa Waziri wa TAMISEMI kwa niaba ya madiwani wote, diwani wa kata ya Ugaka, Emmanuel Cheyo alisema tangu waapishwe na kuanza majukumu yao utendaji wa watumishi hao umekuwa hauridhishi kwani hata maazimio yanayotolewa kwenye vikao halali yamekuwa hayafanyiwi kazi.

Alisema Idara ya fedha imekuwa haitekelezi majukumu yake ipasavyo ikiwemo kutosimamia vizuri suala zima la ukusanyaji mapato hivyo kupelekea kushuka kwa mapato ya halmashauri hivyo kupelekea kukosekana fedha za kupeleka kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.

Aidha, alisema ni jambo la kusikitisha na kushangaza kuona baadhi ya mashine za kukusanyia fedha za mapato yaani POS zikipotea pamoja na fedha zilizokusanywa kutopelekwa benki ndani ya masaa 24 kama sheria inavyoelekeza.

Aliongeza kuwa Mhasibu huyo amekuwa hapeleki taarifa ya fedha Ofisi ya Mkurugenzi wala kuiwasilisha katika baraza la madiwani licha ya kumtaka kufanya hivyo mara kwa mara.

Diwani Cheyo alibainisha kuwa katika kikao cha baraza kilichoketi Juni 3, 2021 waliazimia kumsimamisha kazi ili apishe uchunguzi kutokana na tuhuma hizo aidha baraza maalumu lililoketi Juni 10, 2021 kujadili taarifa ya CAG pia liliazimia kuchukuliwa hatua watumishi waliosababisha halmashauri kupata hati chafu akiwemo Mweka hazina.

Aidha alisema madiwani wamekuwa wakipunjwa maslahi yao zikiwemo posho za kulala kwa wale wanaotoka kata za mbali na kupunguziwa nauli na viongozi wa halmashauri ambao wanasimamia stahiki hizo akiwemo Ofisa Utumishi.

Walimwomba Waziri kumwondoa Ofisa Utumishi huyo kwa kuwa ameshindwa kusimamia maslahi ya madiwani na pia hana mahusiano mazuri nao, hivyo hawawezi kufanya kazi na watumishi hao wawili.

Aidha madiwani hao walimwomba Waziri kuwapelekea watendaji wa vijiji kwa baadhi ya vijiji ambavyo havina watendaji na kuongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo katika vijiji hivyo .

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Manonga Seif Gulamali alimweleza Waziri Ummy kuwa halmashauri hiyo ina vyanzo vingi vya mapato na ina uwezo wa kukusanya zaidi ya sh bil. 5 kwa mwaka lakini watumishi hao hawasikilizi ushauri wa madiwani hali inayopelekea halmashauri kupata fedha kidogo na kushindwa kupeleka asilimia 40 za maendeleo kwa wananchi.

Alisema amekuwa akilipigia kelele suala hilo kwa muda mrefu lakini utekelezaji wake umekuwa hakuna hivyo akamwomba Waziri aiangalie halmashauri hiyo kwa jicho la huruma ili iweze kupata watumishi wenye weledi mkubwa.

Aidha alilalamika kuwa kiasi cha Sh milioni 220 zilizoletwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika zahanati 10 za Iborogelo, Mwasunho, Mwanzugi, Mbutu, Ibutamisuzi, Ziba, Nanga, Nyandekwa, Mwabubele na Ngulu na kila zahanati ilitengewa Sh milioni 22 lakini tangu Julai mwaka jana lakini hadi sasa hakuna matundu yaliyokamilika.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Lucas Bugota alisema madiwani wamefikia maamuzi hayo baada ya kuona kila wanapoomba taarifa mbalimbali hawapewi ushirikiano na kubainisha kuwa hatakubali kuona mapato ya serikali yakipotea au kutumiwa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Igunga Nicholous Ngasa alisema bila hatua za haraka kuchuliwa kwa baadhi ya watumishi, halmashauri hiyo itaendelea kubaki nyuma katika shughuli za maendeleo.

Kufuatia hali hiyo Waziri Ummy alimwuliza Mweka Hazina kuwa halmashauri ina POS ngapi ambapo alijibu kuwa zipo 120 lakini 57 hazifanyi kazi jambo ambalo halikumfurahisha, aidha alishangaa kutoona taarifa ya sh mil 800 zilizoletwa na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Alilazimika kumwinua Ofisa Mipango Joel Nkesela ili aeleze kwa nini fedha zinazotolewa na serikali hazipo kwenye taarifa yao ambapo aliomba radhi kwa kwa kushindwa kuweka taarifa hiyo.

“Waheshimiwa madiwani na wabunge ombi lenu nimelipokea nitalifanyia kazi kwani nimeona hapa kuna shida,” amesema.

Alitoa wito kwa madiwani na matumishi kufanya kazi kama timu 1 ili fedha zote zinazokusanywa ziweze kurudi kwa wananchi ili zifanye shughuli za maendeleo na kuongeza kuwa hatasita kuchukua hatua kali kwa mtumishi yoyote atakayebainika kula fedha zinazokusanywa kupitia POS.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles