29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

MADIWANI CHAMWINO WAGOMEA KIKAO, WATAKA MIKOPO WANAYODAIWA CRDB ILIPWE

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Madiwani wa Halmashari ya Wilaya ya Chamwino, leo wamegoma kujadili masuala yanayohusu halmashauri na kutaka kikao hicho kujadili madeni ya mikopo wanayodaiwa na Benki ya CRDB.

Madiwani hao waligoma kwa muda wa saa sita ambapo wamedai wametishiwa kunyang’anywa mali zao kufidia madeni hayo ambayo jumla ni Sh 270 ikiwa ni malimbikizo ya miezi 15.

Awali, kabla ya kugomea kikao hicho, iliwasilishwa taarifa ya kujadili rasimu ya bajeti na Ofisa Mipango wa halmshauri hiyo ambapo baada ya kumaliza madiwani hao waligoma na kuanza kutoa hoja zao wakidai wameitwa wadaiwa sugu kwa kulimbikiza madeni hayo huku maofisa wa Benki ya CRDB wakiwapatia barua za kuwafilisi mali zao kutokana na malimbikizo hayo.

Wamedai wamekuwa wanakatwa kwenye mshahara wao madeni hayo lakini Ofisi ya Mkurugenzi haifikishi benki ambapo katika mkopo huo kila Diwani alikopa Sh milioni 13.

“Hatujadili mipango ya wananchi wakati sisi wenyewe tunadaiwa mdhamini wetu alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri,” amedai mmoja wa madiwani hao.

Baada ya mjadala mkali baada ya saa sita madiwani hao walisitisha mgomo huo huku wakikubaliana kuwa Mkurugenzi aandike barua ya kujidhamini jinsi ya kumaliza deni hilo.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino, Athman Masasi amejibu kwa kifupi; “madeni hayo ni madeni kama madeni mengine ambayo tumekubaliana kuyalipa.”

Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Benki ya CRDB, Godwin Semunyu amesema si ruksa wala maadili ya kibenki, kuzungumzia madeni ya mteja.

“Hairuhusiwi kimaadili kwa sababu mkataba wa mtu anakopaje, analipaje au akaunti yake ina kiasi gani cha fedha ni siri baina ya benki na mteja.

“Ni watu ambao midomo yetu haiwezi kuongea lolote kuhusu biashara yetu na mteja, lakini kama wanasema mdhamini wao ni mkurugenzi basi nadhani mtu sahihi hapo ni yeye,” amesema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles