Na Derick Milton, Busega
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, wameazimia kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo la kukusanya zaidi ya asilimia 100 ya bajeti ya Sh bilioni 32.39 kwa mwaka wa fedha 2022/23 ili kuweza kupata fedha za kuhudumia wananchi.
Kwa mwaka wa fedha 2021/22 Halmashauri ya Wilaya ya Busega imekusanya asilimia 99 ya mapato yake ikilinganishwa na asilimia 74 walizokusanya mwaka 2020/21.
Wakizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana mjini Nyashimo, madiwani hao walisema kuwa katika maelengo ambayo wamejiwekea ya kukusanya zaidi ya asilimia 100 watahakikisha wanafikia lengo hilo.
Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya, Sundi Mniwe amesema kuwa kazi kubwa kwao kama madiwani ni kuhakikisa kila chanzo cha mapato kwenye halmashauri yao lazima kikusanywe kwa alisimia kubwa.
“Kwa mwaka wa fedha uliopita tulifikia asilimia 99, na hii imetokana na usimamizi wa kila mtu, watu hatukulala, hatukupumzika ilikuwa ni kucha kucha watu kazini, tunategemea mwaka huu kazi iwe hiyo hiyo tunataka tuvuke kiwango cha mwaka huu zaidi ya asilimia 100,” amesema Sundi.
Naye, Christopher Bukalashaambaye ni Diwani Kata ya Malili, amesema kuwa kazi kubwa iliyopo mbele yao ni kuhakikisha wanawasimamia kwa karibu watumishi kwenye ngazi zote ambazo wamepewa dhamana ya kukusanya kwenye vyanzo vyote vya mapato.
Katika mwaka wa fedha 2022/23 halmashauri hii imejiwekea malengo ya kukusanya zaidi ya asilimia 100 ya bajeti yake ya kukusanya na kutumia Sh bilioni 32.39.
Aidha, wamewataka watendaji wote ambao wamepewa dhamana ya kukusanya na kusimamia ipasavyo vyanzo vya mapato na ukusanyaji, kuhakikisha wanatekeleza jukumu hilo kwa kiwango kikubwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Veronica Sayore ameweka bayana mikakati waliyojiwekea ili kufikia matarajio hayo, ambapo ameeleza ofisini yake imeweka mkakati shirikishi na jamii kuhakikisha wanafikia lengo la makusanyao.
“Tumeweka mkakati wa kushirikisha jamii ambayo ndiyo walipa huo ushuru, ambapo tutawaunganisha na wataalamu wetu ambao ndiyo wakusanya mapato na tumedhamilia mwaka kuhakikisha tunavuka asilimia 100,” amesema Sayore.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Gabriel Zakaria amesema kuwa ikiwa vyanzo vyote vya mapato vitasimamiwa ipasavyo, halmashauri itakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wake.