28.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Madiwani Busega waeleza sababu vikundi kushindwa kurejesha mikopo

Na Derick Milton, Simiyu

Madiwani wa Halmashuari ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, wameitaka Ofisi ya Maendeleo ya Jamii katika halmashauri hiyo kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kuvichunguza vikundi vya vijana, walemavu na wanawake kabla havijapewa mikopo.

Wamesema kuwa vikundi hivyo vichunguzwe kama vinafaa kupewa mikopo na kama vipo halali ili kupunguza changamoto iliyopo kwenye halmashuari hiyo ambapo vikundi vingi hasa vya vijana kupewa mkopo kisha kugawana.

Madiwani hao wamezungumza hayo leo Februari 22, kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Halmashuari, ikiwa zimepita siku chache tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo kubaini madudu kwa vikundi vilivyopewa mikopo.

Taasisi hiyo ilibaini uwepo wa vikundi hewa ambavyo vilipewa mkopo na halmashuari hiyo, huku vingine wanufaika wakigawana fedha bila ya kutekeleza mradi walioombea mkopo na vingine vikikutwa havina ofisi.

Diwani kata ya Kiloleli, Vumi Magoti, amesema kuwa tatizo kubwa lipo kwenye ofisi ya Maendeleo ya jamii ambao wameshindwa kuvikagua vikundi ambavyo vimekuwa vikileta maombi kwao ya kupewa mkopo.

“Vikundi vingi haviko sawa, Ofisi ya Maendeleo ya jamii haifanyi uchunguzi kabla ya kuvipatia mkopo, vingine vimekuwa vikidanganya kuwa wana miradi wakati hawana, wakikaguliwa wanaonyesha maduka ya watu wengine, ukiwapatia mkopo wanagawana,” amesema Magoti.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Simon Songe, ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama katika Wilaya hiyo ikiwemo Takukuru, kusaidia katika kuvichunguza vikundi ambavyo vinaleta maombi ya kupatiwa mikopo.

“Changamoto kubwa hapa ni Ofisi ya Maendeleo ya Jamii kushindwa kuchunguza kwanza, lakini pia hata kushindwa kuvitembelea mara kwa mara kuangalia maendeleo yao mara baada ya kuvipatia mikopo, ndiyo maana vingi wamegawa pesa, na vimeshindwa kurejesha mikopo,” amesema Songe.

Mwenyekiti wa Halmashuari hiyo aliitaka Ofisi ya Maendeleo ya Jamii kufanya uchunguzi wa vikundi vyote, ikiwa pamoja na kuvitembelea mara kwa mara vile ambavyo vinapewa mikopo ili kuangalia maendeleo yao ikiwa pamoja na kusisitiza urejeshwaji wa mikopo ili kuweza kunufaisha wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles